NA FRESHA KINASA
JESHI la Polisi nchini limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 21 katika Mkoa wa Polisi wa Tarime Rorya na Mkoa wa Mara kwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya kihalifu ikiwemo wizi wa kutumia silaha, kupora mali za watu na kufanya matukio ya mauaji.
Kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na opereshi zilizofanywa na jeshi hilo mkoani humo kufuatia uwepo wa matukio mbalimbali yaliyotokea siku za hivi karibuni na kupelekea Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kutuma kikosi kazi kutoka makao makuu kuja kuendesha opereshini ili kutokomeza uhalifu na wananchi waishi salama na mali zao na wafanye shughuli zao za kiuchumi.
Hayo yamebainishwa leo Mei 26, 2023 na Awadhi Juma Haji, Kamishina wa Polisi Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Musoma mkoani Mara kuelezea mafanikio ya opereshini hiyo.
"Katika kipindi cha mwezi Mei 2023 Mkoa wa Mara na Mkoa wa Polisi Tarime Rorya kulijitokeza matukio ya mauaji na unyang'anyi wa kutumia silaha yaliyozua taharuki kwa Wananchi. Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Polisi limechukua hatua stahiki na za haraka kukabiliana na hali hiyo kwa lengo la kuhakikisha kuwa hali ya utulivu na amani inarejea katika maeneo hayo.
"Hatua zilizochukuliwa zimeleta mafanikiko makubwa ambapo mpaka sasa jumla watuhumiwa 21 waliokuwa wanajihusisha na matukio hayo wamekamatwa na taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao.
"Mnamo tarehe 21/05/2023 majira ya 08:20 usiku huko Kijiji Cha Nyankanga Kata ya Nyakanga Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara ambapo Nickson Gisili (42) mjasiriamali na mkazi wa Nyakanga alivamiwa nyumbani kwake kisha kujeruhiwa kwa risasi na kusababisha kifo chake.
"Pia wahalifu hao walimjeruhi mke wake aitwaye Miriam Jumanne (34) kwa kumshambulia kwa silaha za jadi na kisha kuporwa fedha taslimu shilingi 3,000. Sola Tv moja nchi 32, na simu tano ndogo."
Kamishina Awadhi Juma Haji amesema kuwa, kabla ta tukio hilo wahalifu hao waliwajeruhi watu 8 wakazi wa Kijiji cha Mmazame Kata ya Bukabwa Wilaya ya Butiama kwa kuwashambulia kwa silaha za jadi sehemu mbalimbali za miili yao na kwamba, majeruhi hao wanaendelea vizuri na wameruhusiwa kutoka hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara isipokuwa majeruhi mmoja amepelekwa hospitali ya rufaa Bugando.
Kutokana na matukio hayo amefafanua kwamba, Jeshi la Polisi kwa kutumia makachero wake wabobezi na mahiri katika ufuatiliaji wa matukio ya kihalifu kwa kushirikiana na Wananchi limeweza kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa sita kuhusiana na matukio hayo. Mahojiano yanaendelea na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
TARIME RORYA
"Aidha mnamo 14/05/2023 huko katika Wilaya ya Polisi Sirari Mkoa wa Polisi Tarime Rorya kulitokea matukio mawili ya mauaji ya Ramadhan Mussa Keryoba (23) Mkazi wa Kijiji Cha Gwitiryo aliyejeruhiwa kwa risasi kichwani na wahalifu na kufariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu,"amesema nakuongeza kuwa.
"Katika tukio hilo, wahalifu hao walipora fedha Shilingi 500,000. na simu mbili, pia baada ya tukio hilo wahalifu hao walimshambulia Otieno Sore Chacha (50) Mkulima mkazi wa Kijiji cha Nyabisaga kwa kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali kichwani Kisha kupora simu moja aina ya Tecno. Jeshi la Polisi linapenda kuwajulisha kuwa watatu waliofanya mauaji hayo na uporaji wamekamatwa ikiwa ni pamoja na aliyekuwa amekimbilia nchi jirani ya Kenya," amesema na kuongeza kwamba.
"Mtakumbuka mnamo tarehe 15/05/2023 Jeshi la Polisi lilitoa taarifa juu ya mauaji ya Isack Daniel ambaye ni Daktari wa kituo Cha afya Kerende katika Mkoa wa Kipolisi wa Tarime Rorya ambaye aliuawa tarehe 03/05/2023 na kuelezwa kwamba watuhumiwa watatu waliofanya tukio hilo wamekamatwa. Juhudi zaidi zimefanyika na kuweza kumkamata mtuhumiwa mmoja na kukamilisha idadi ya watuhumiwa wote wanna waliohusika katika tukio hilo,"amesema.
Pia amesema jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 8 wa matukio ya unyang'anyi wa kutumia silaha yaliyotokea tarehe 04/05/2023 majira ya saa 10:00 alfajiri katika Kijiji cha Nyangoto Kata ya Matongo ambapo Consolata Christopher aliyevamiwa na kuporwa bastola aina ya Browning ikiwa na risasi 12 fedha taslimu 20,000. Radio moja aina ya Sabufa na simu moja aina ya Itel.
"Katika tukio jingine, mnamo tarehe 05/05/2023 majira ya saa 7:40 usiku Katika Kijiji cha Kangarieni Kata ya Itiryo Petro Nyangi akiwa dukani kwake alivamiwa na kujeruhiwa kwa risasi shingoni kisha kuporwa bidhaa mbalimbali za dukani na simu moja ndogo. Vile vile mnamo tarehe 10/05/2023 majira ya saa 7:30 usiku katika Kijiji cha Kangarieni Kata ya Itiryo Mwita Daniel Nyanokwe alivamiwa na kujeruhiwa kwa panga na kuporwa fedha taslimu 2,800,000,"amesema Kamishina Haji.
Ambapo amesema,matukio yote hayo yametokea Wilaya ya Polisi Nyamwaga Mkoa wa Polisi Tarime Rorya na kwamba watuhumiwa wote wamekamatwa na upelelezi ukikamilika watafikishwa mahakamani.
"Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa wahalifu na watu ambao wanajihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja na watambue kuwa wakifanya uhalifu wowote ule na kwa namna yoyote ile watakamatwa popote pale walipo hata kama ni nje ya nchi,"amesema Kamishina Awadhi Juma Haji.
Aidha, amesema kwamba wananchi wanapaswa kuendelea kutoa taarifa na ushirikiano kwa kufichua watu wote wanaojihusisha na uhalifu na uvunjifu wa amani. Na kwamba hali ya usalama nchini kwa ujumla ni shwari na opereshini zinaendelea kufanyika maeneo mbalimbali kudhibiti uhalifu na wahalifu.