NA DIRAMAKINI
JESHI la Polisi mkoani Arusha limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa Isack Robertson (45) mkazi wa Sombetini jijini Arusha kwa tuhuma za kumpiga na kumjeruhi mke wake, Jackline Mkonyi (38) mkazi wa Sombetini jijini humo.
Tunaomba radhi iwapo picha hii inaweza kuwasababishia usumbufu wasomaji wetu. Picha ni Jackline Mnkonyi (38) mkazi wa Sombetini jijini Arusha ambaye alijeruhiwa na mumewe. (Picha na a24habari).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 28, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Justine Masejo, mtuhumiwa alikamatwa Mei 27, 2023 huko katika maeneo ya Himo mkoani Kilimanjaro.
ACP Masejo amesema, mtuhumiwa huyo anaendelea kuhojiwa na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.
Hayo yanajiri ikiwa ni juzi a24habari blogu iliripoti kuhusu tukio hilo ikieleza kuwa, mwanamke huyo aliyetambulika kwa jina la Jackline Mnkonyi(38) mkazi wa Sombetini jijini Arusha amejeruhiwa vibaya kwa kipigo kikali kutoka kwa mume wake,Isaac Mnyagi ikiwa ni pamoja na kung’olewa jino la mbele na kutobolewa jicho kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Mtuhumiwa Isack Robertson (45) mkazi wa Sombetini jijini Arusha.
Akizungumza kwa tabu na waandishi wa habari nyumbani kwa wazazi wake eneo la Sinoni huko Daraja Mbili jijini Arusha,Jackline ambaye ana mtoto mchanga alidai kuwa, baada ya kipigo hicho mume alimpakia kwenye gari yake akiwa hajitambui na kwenda kumtupa getini nyumbani kwa wazazi wake Sinoni.
Jackline alidai kuwa,mchana wa Mei 23, mwaka huu alitembelewa na mjomba wake ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Simiyu ,Vicenti Matai kwa lengo la kumsalimia.
Alidai, mume wake huyo aitwaye,Isaack ambaye ni mwalimu aliyezaa naye watoto wawili amekuwa na tabia ya kumpiga pindi anapofika nyumbani kwake baada ya muda wa zaidi ya miezi mitatu na siku ya tukio alikuja ghafla majira ya usiku.
Pia, alisema siku ya tukio mumewe alifika nyumbani kwake majira ya saa 4.45 usiku na kugonga mlango na kufunguliwa na watoto, lakini hakutaka salamu na mkewe ila aliingia chumbani na alipomfuata alitoka chumbani.
Jackline alipoona hivyo alimuuliza kulikoni na alichoambulia ni maneno mazito na matusi na kuulizwa mchana alikuwa na nani na kumjibu kuwa alikuwa na mjomba wake, hatua ambayo alikana ndipo alipoanza kumshambulia kwa ngumi,mateke na mkanda na baadaye alichukua praizi na kumng'oa jino kwa nguvu.
"Nilijitahidi sana kujieleza, lakini ilishindikana alianza kunipiga kwa mateke na ngumi na alichukua praizi na kuniamuru nifungue mdomo na kuning’oa jino moja ambapo damu zilianza kuchuruzika na kuanguka chini."
Jackline alidai kuwa, licha ya kipigo hicho pia alichukua kitu chenye ncha kali na kumtoboa jicho moja ambalo hadi sasa hawezi kuona huku akimwambia maneno mazito na kumtishia kumuua.
Alidai kuwa,hakujua jinsi alivyofikishwa nyumbani kwa wazazi wake Sinoni, Daraja Mbili na kutupwa getini, kwani alishtukia akiwa hospitali.
‘’Nimetobolewa jicho na kung’olewa jino na praizi, nina maumivi makali sana, naiomba Serikali ichukue hatua dhidi ya mume wangu, kwani amenifanyia unyama wa hali ya juu sana,’’alidai.
Kwa upande wake baba mzazi wa Jackline,Elimilis Mnkonyi alisema, siku ya tukio wakiwa nyumbani majira ya saa saba usiku walipokea simu kutoka kwa mwanaume huyo akiwataka wakachukue mzoga wao hapo nje.
Alisema, akiwa na mke wake,walienda hapo getini na kumkuta mtoto wao Jackline akiwa hajitambui na kuamua kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru na baadaye alienda kutoa taarifa kituo cha polisi kupitia jalada namba ARS/RB/5416/2023.
"Baada ya kutoa taarifa polisi tulienda kumtafuta mtuhumiwa, lakini ametoroka na polisi wanaendelea kumsaka."
Picha ni Jackline Mnkonyi (38) mkazi wa Sombetini jijini Arusha kabla hajafanyiwa ukatili.
Mkonyi mwenye watoto nane na wajukuuu 16, alifafanua kwamba mtoto wake alikuwa ameolewa na mume wa ndoa lakini walitengana na kuamua kuishi na mwanaume huyo ambaye hata hivyo hakuwahi kujitambulisha kwake licha ya kusikia malalamiko ya ugomvi wa mara kwa mara.
Pia, Mkonyi alisema kuwa mtoto wake,Jackline aliwahi kumweleza mama yake kuwa mwanaume huyo amekuwa na tabia ya kumpiga mara kwa mara, lakini yeye hajawahi kuelezwa kwani mtoto wa kike.(Tanpol/a24habari).