Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje yapita kwa kishindo bungeni

NA MWANDISHI WETU

BUNGE la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 ya shilingi 247,971,524,000.
Kati ya fedha hizo, shilingi 230,083,916,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida yakijumuisha Shilingi 213,304,516,000 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo;.

Aidha, Shilingi 16,779,400,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara huku kiasi cha Shilingi 17,887,608,000 kimetengwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

Maombi ya Makadirio ya bajeti ya wizara yaliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) ambapo Bunge limepitisha kwa kishindo na kuipongeza Wizara kwa jinsi ilivyojipanga kutekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka 2023/2024 Mhe. Waziri Dkt. Tax aliwaeleza Wabunge kuwa ili kuendana na mabadiliko katika uhusiano wa kimataifa na mambo ya nje, Wizara imefanya tathmini ya Sera ya Mambo ya Nje ya mwaka 2001. 

Tathmini hiyo imebainisha kuwa misingi ya Sera iliyopo bado inakidhi matakwa ya sasa na kubaini kuwa yapo maeneo mapya yanayohitaji kujumuishwa katika Sera. Maeneo hayo ni diaspora; uchumi wa buluu; uratibu wa mikataba na itifaki za kikanda na kimataifa; mazingira na mabadiliko ya tabianchi; haki za binadamu, hususan kwa kuzingatia mila na desturi za taifa letu; na kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili.Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) akijibu hoja zilizowasilishwa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni Dodoma.

Mhe. Waziri aliliambia Bunge kuwa Serikali inashughulikia suala la Diaspora wa Tanzania ili wapate hadhi maalum ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana nchini na kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla kuwa mchakato wa jambo hilo unaendèlea vizuri na utakamilika hivi karibuni. 

Sanjari na hadhi maalum kwa diaspora, Mhe. Waziri alieleza kuhusu Wizara kukamilisha mfumo wa Kidigitali wa kuwasajili diaspora (Diaspora Digital Hub) ambao ulizinduliwa rasmi tarehe 22 Mei 2023. Aliongeza kuwa uwepo wa mfumo huo utaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za idadi ya diaspora, mahali walipo, ujuzi na uzoefu walionao. Aidha, mfumo utawawezesha Diaspora kupata taarifa kuhusu fursa na huduma mbalimbali zinazotolewa na sekta za umma na binafsi hapa nchini.Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Samwel Shelukindo (kushoto) pamoja na Naibu Katibu MKuu wa Wizara hiyo Mhe. Balozi Fatma Rajab wakifuatilia uwasilishwaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni Dodoma.

Waheshimiwa Wabunge walipongeza uamuzi wa Wizara wa kuandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi na kueleza kuwa mpango huo utawezesha wadau kutoka sekta za umma na sekta binafsi kutambua wajibu wao na kushiriki kikamilifu na kwa tija. 

Naye Mbunge wa Kilosa, Mhe. Profesa Palamagamba Kabudi (Mb.) ameipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuruhusu wana Diaspora kupewa hadhi maalumu huku akieleza ugumu uliopo wa serikali kukubali uraia pacha. 
“Suala la uraia pacha halina muafaka, siyo hapa nchini wala huko duniani, kwa hiyo tushikilie hili tulilo na muafaka nalo tulisukume kwa uharaka ili liende. Utafiti nilioufanya huko duniani ni asilimia 49 ya nchi duniani zinaruhusu uraia pacha, asilimia 51 haziruhusu duniani, pia zipo nchi zenye diaspora wengi duniani lakini haziruhusu uraia pacha badala yake zinawatambua diaspora kwa hadhi maalumu,” alisema Prof. Kabudi

Vile vile, hotuba ya Bajeti ya Mhe. Waziri imeainisha mafanikio mbalimbali ambayo Wizara imeyapata katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023. Mafanikio hayo ni pamoja na misaada na mikopo ya masharti nafuu, uwekezaji, masoko ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, miradi ya maendeleo ya mtangamano, uwekezaji kutoka nje na uwekaji saini wa mikataba na hati za makubaliano mbalimbali. 
Mafanikio hayo pia yamegusa uendelezaji wa viwanja vya balozi kwa ajili ya ofisi na vitega uchumi na taasisi za kimataifa ambazo nchi imesaini mikataba ya uenyeji. Katika hili, Wizara itakabidhi eneo la ujenzi wa Jengo la Ofisi la Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu jijini Arusha tarehe 01 Juni 2023 kwa mkandarasi kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news