NA MWANDISHI WETU
ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bernard Kamilius Membe, amefariki dunia leo asubuhi Ijumaa Mei 12, 2023 akiwa katika Hospitali ya Kairuki Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Kairuki, Arafa Juba amethibitishia Mwananchi taarifa za kutokea kwa kifo hicho akieleza kuwa kimetokea saa mbili asubuhi.
“Ni kweli Membe aliletwa asubuhi hapa akapatiwa matibabu na wataalam kama ilivyo kawaida mgonjwa anapokuja hospitali, lakini Mungu alimpenda zaidi akafariki saa mbili asubuhi,” amesema Arafa.
Kuhusu ugonjwa uliokuwa unamsumbua, Arafa amesema ugonjwa ni siri ya mgonjwa na daktari hivyo undani wa hilo unaweza kutolewa na familia na si hospitali.
Katika hatua nyingine, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za rambirambi kwa familia kutokana na msiba huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Ndugu Bernard Membe. Kwa zaidi ya miaka 40, Ndugu Membe alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi yetu kwa weledi. Pole kwa familia, ndugu, jamaa & marafiki. Mungu amweke mahali pema. Amina.”(MWANANCHI)