Binti wa Kitanzania kutoka Lushoto ashinda tuzo ya Mfalme Charles III

NA MWANDISHI WETU

MSICHANA wa Kitanzania, Zamana kutoka Kijiji cha Irente Juu, Kata ya Magamba Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga ameshinda tuzo ya Mfalme Charles III wa Uingereza ijulikanayo kama "Prince’s Trust Award". 
Bi. Zamana (kulia) na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro wakiwa na tuzo iliyotolewa na Mfalme Charles III.

Tuzo hii ilianzishwa mwaka 2015 na Mfalme Charles III, wakati huo akiwa bado ni mwana wa Mfalme (Prince of Wales), kupitia taasisi yake tanzu iitwayo, Prince’s Trust International. 

Zamana amepata tuzo hiyo katika eneo la uwezeshaji wanawake lijulikanalo kama Amal Clooney Women’s Empowerment Award. 

Bibi Amal Clooney ni mwanasheria wa kimataifa mwenye mafanikio makubwa katika fani yake, ambaye ndiye alimkabidhi Zamana tuzo hiyo.

Taasisi hiyo ya Mfalme Charles III inalenga kuwajengea uwezo vijana wa kike na wa kiume kujifunza, kufanya kazi na kustawi. Tuzo ya Zamana imetokana na kampeni yake ya “Niache Nisome”. Kampeni hii ni ya kuwahamasisha wazazi, jamii na watoto wa kike watumie fursa zilizopo kusoma kwa bidii, kujitunza na kuzingatia masomo kwa ajili ya kujijengea misingi imara ya maisha.

Mei 17, 2023, Zamana alikutana na Mfalme Charles III katika Kasri la Buckingham, wakati Mfalme huyo alipofanya dhifa ya kuwapongeza washindi wa tuzo hiyo. 
Bi. Zamana (wa kwanza kushoto) katika picha ya pamoja na Mfalme Charles III (wa kwanza kulia) wakati wa hafla ya kuwapongeza waliopata tuzo iliyoandaliwa na Mfalme huyo.

Aidha, Mei 19 mwaka huu, Zamana alipokelewa Ubalozi wa Tanzania, London na kufanya mazungumzo na Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro na maafisa wengine wa Ubalozi huo. 

Zamana anakuwa kijana wa kwanza wa Kitanzania kupata tuzo hiyo adhimu ya kimataifa inayotolewa na taasisi hiyo ya Mfalme Charles III.

Bi. Zamana (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro (wa pili kushoto) na maafisa wengine wa Ubalozi huo.

Taasisi iliyompendekeza ni Asante Africa Foundation yenye makao yake jijini Arusha, kwa kushirikiana na Prince’s Trust International. 

Taasisi ya Asante inajishughulisha na uwezeshaji wa vijana katika maeneo ya elimu, stadi za dijitali, ujasiriamali, uongozi na stadi nyingine za maisha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news