BREAKING NEWS:Kukatika umeme mechi ya Yanga, Rivers United yang'oa vigogo saba

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewasimamisha kazi watumishi saba kutokana na changamoto ya kujirudia kukatika kwa umeme wakati mechi zikiendelea katika Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo umefikiwa na Waziri wa wizara hiyo, Mheshimiwa Balozi Dkt.Pindi Chana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt.Saidi Yakub kupitia taarifa iliyotolewa Aprili 30, 2023 na Eleuteri E.Mangi kutoka Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

"Itakumbukwa 28 Machi, 2023 kulikuwa na mechi baina ya timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda (Uganda the Cranes) kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON). Siku hiyo umeme ulikatika wakati mechi hiyo inaendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

"Kufuatia hali hiyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) alimuelekeza Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma, (Mb) kukaaa na wataalamu kuchunguza tatizo la kukatika umeme katika uwanja huo hasa wakati mechi zinaendelea kuchezwa na kupata suluhisho la tatizo hilo.

"Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) alipokea taarifa ya wataalamu wa umeme ambao walimueleza kuwa chanzo cha hitilafu ya kukatika kwa umeme Uwanja wa Benjamin Mkapa ni kutokana na mchanganyiko wa umeme wa jenereta na umeme wa gridi ya taifa katika kuwasha taa za uwanja huo na wakapendekeza kuwa taa hizo ziwashwe na umeme wa jenereta pekee.

"Mapendekezo hayo ya wataalam yalitekelezwa kama walivyoshauri. Hata hivyo, hitilafu ya kuzimika kwa taa imejitokeza tena usiku wa leo wakati ya mechi ya Yanga na Rivers United ya Nigeria ambayo ni mechi ya robo fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

"Kutokana na kujirudia kwa hali hiyo licha ya ushauri wa wataalam kufuatwa, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, (Mb) ameagiza hatua zifuatazo kuchukuliwa;

1. Kusimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi watumishi wanaohusika na uendeshaji wa uwanja. Kufuatia agizo hilo na kwa mamlaka aliyonayo, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amewasimamisha kazi watumishi wafuatao ili kupisha uchunguzi,
i. Salum Mtumbuka - Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
ii. Manyori Juma Kapesa – Mhandisi wa Umeme wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
iii. Tuswege Nikupala – Afisa Tawala Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Aidha, Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu amewasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi watumishi wafuatao ambao nao wanamajukumu ya uendeshaji wa Uwanja wa Benjamin Mkapa.
i. Gordon Nsajigwa Mwangamilo
ii. Gabriel Mwasele
iii. Yanuaria Imboru
iv. Dkt. Christina Luambano

Wakati huo huo, kufuatia hatua zilizochukuliwa, Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Saidi Yakubu amemteua, Bw. Milinde Mahona kuwa Kaimu Meneja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na uteuzi huo
unaanza mara moja kuanzia Mei 1,2023.

"Katibu Mkuu kuwasiliana na wadau wote husika ili mechi zitakazochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa zichezwe wakati wa alasiri/jioni badala ya usiku katika kipindi ambacho wizara ianakamilisha taratibu za kupata mzabuni atakayefanya ukarabati mkubwa katika uwanja huo kabla ya kuanza kwa msimu ujao wa ligi AU michuano ya kimataifa,"imeongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Pia, kwa mujibu wa taarifa hiyo,ameagiza mamlaka za nje ya wizara kufanya uchunguzi wa kukatika umeme katika uwanja huo na hatua za kuchukua.

"Wizara inaomba radhi mashabiki wa soka nchini hususan wa timu ya Yanga kwa kadhia iliyojitokeza. Wizara inawaahidi Watanzania wote kwamba itaendeea kufanya ukarabati mdogo na mkubwa ili Uwanja wa Benjamin Mkapa uendelee kutoa huduma na burudani stahiki kwa Watanzania pamoja na nchi jirani zinazotumia uwanja huo,"imeongez taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news