SERIKALI kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imesema imejipanga kumaliza tatizo la uraibu wa dawa za kulevya nchini.
"Nilizungumza awali kuhusu mikakati ya mamlaka ile minne, ambayo niliizungumzia na katika hiyo mikakati tumejikita na Serikali imejipanga inatoa huduma za tiba kwa waraibu wa dawa za kulevya pamoja na huduma za utengamao.
"Na katika eneo hilo utakuta kwamba sisi tunatengeneza miongozo, tunatoa mafunzo kwa watoa huduma za afya hasa katika vitengo vyote vya afya ya akili katika hospitali za wilaya na mikoa, kwa hiyo mtu yeyote ambaye ana tatizo la dawa za kulevya kwenye vitengo vya afya akili, wanaweza wakaenda wakapata huduma.
"Lakini pia tuna huduma maalumu kwa ajili ya waraibu ambao wameathirika na dawa maalumu mfano tuna usaidizi wa tiba ya Methardone (MEDICALLY ASSISTED THERAPY-MAT).
"Hii ni huduma ambayo inatolewa kwa wale waraibu ambao wameathirika na dawa za kulevya aina ya heronie na dawa zingine aina ya afyuni na hadi sasa hivi tumeweza kupanuka tuna kliniki zaidi ya 15 nchini, na kwa upande wa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika, sisi Tanzania ndiyo tunaongoza kwa kuwa na huduma hii.
"Kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na sehemu nyingine. Na watu wengi wanakuja kujifunza kutoka kwetu kwa hiyo Serikali imepambana katika hilo,"amefafanua kwa kina Dkt.Nyandindi.
VITUO VYA TIBA SAIDIZI KWA WARAIBU KWA KUTUMIA DAWA (MEDICALLY ASSISTED THERAPY - MAT)
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), vituo hivi husimamiwa na serikali na huhudumia waathirika wa dawa ya kulevya aina ya afyuni kama vile heroin na baadhi ya dawa tiba zenye asili ya kulevya.
Waathirika wanaotibiwa kwenye vituo hivi hutibiwa kwa kutumia dawa mfano Methadone. Waathirika wanatakiwa kuhudhuria matibabu kila siku mpaka watakapomaliza matibabu. Huduma ya MAT hutolewa bure chini ya uangalizi wa wataalamu.
HUDUMA ZINAZOTOLEWA KATIKA VITUO VYA TIBA SAIDIZI KWA WARAIBU KWA KUTUMIA DAWA (MAT)
- Kupatiwa dawa aina ya methadone
- Kupatiwa Elimu juu ya UKIMWI na Kupima VVU
- Kupatiwa dawa za kufubaza VVU (Antiretroviral therapy)
- Kupatiwa elimu ya Kinga, Kupima na kutoa matibabu kwa wagonjwa wa Kifua kikuu.
- Kupatiwa elimu ya Kinga na kutibu Magonjwa ya zinaa
- Kupatiwa Ushauri nasaha
- Kupatiwa matibabu ya magonjwa ya Akili
- Kupatiwa Elimu juu ya maambukizi ya Homa ya ini B na C
ORODHA YA VITUO VYA METHADONE NA MAHALI VILIPO
Na | JINA LA KITUO | JINA LA HOSPITALI | MKOA |
1. | Kliniki ya MAT Muhimbili | Hospitali ya Taifa Muhimbili | Dar es Salaam |
2. | Kliniki ya MAT Mwananyamala | Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Mwananyamala | Dar es Salaam |
3. | Kliniki ya MAT Temeke | Hospitali ya Mkoa ya Rufaa Temeke | Dar es Salaam |
4. | Kliniki ya MAT Mbeya | Hospitali ya Rufaa ya Kanda | Mbeya |
5. | Kliniki ya MAT Mwanza | Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Sekou Toure | Mwanza |
6. | Kliniki ya MAT Itega | Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe | Dodoma |
7. | Kliniki ya MAT Bagamoyo | Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo | Pwani |
8. | Kliniki ya MAT Tanga | Hospitali ya Mkoa ya Rufaa ya Bombo | Tanga |
9. | Kliniki ya MAT Tumbi | Hospitali ya Rufaa yaMkoa ya Tumbi, Kibaha | Pwani |
10. | Kliniki ya MAT Arusha | Hospitali ya Mkoa ya Rufaa yaMkoa, Mount Meru- Arusha | Arusha |
11. | Kliniki ya MAT Tunduma | Kituo cha Afya cha Tunduma | Songwe |
12. | Kliniki ya MAT Segerea | Kituo cha Afya cha Segerea | Dar es Salaam |
13. | Kliniki ya MAT Tegeta | Kituo cha Afya cha Tegeta | Dar es Salaam |
14. | Kliniki ya MAT Mbagala | Zahanati ya Round Table-Mbagala | Dar es Salaam |
15. | Kliniki ya MAT Kigamboni | Hospitali ya Vijibweni-Kigamboni | Dar es Salaam |
- Ili uweze kujiunga na vituo hivi, lazima upitie kwenye asasi za Kiraia CSOs zilizo kasimiwa kupeleka waraibu katika vituo hivyo vya Methadone.
- Waraibu watapatiwa elimu juu ya matibabu ya methadone na baadaye kuunganishwa na jamaa zao ili waweze kuwasaidia.
- Mafunzo huchukua takribani majuma mawili
- Baada ya mafunzo, Waraibu watapelekwa kwenye vituo vya Methadone kuanza dawa.
- Jamaa zao watatakiwa kuwasaidia waraibu kwa kuwapatia nauli ya kuhudhuria matibabu, chakula na malazi. Hatua hii inasaidia katika uponaji wa muraibu.
NINI FAIDA YA TIBA YA METHADONE
- Inaondoa utegemezi wa dawa za kulevya aina ya heroin
- Inapunguza hatari ya mtegemezi kuwa katika hali ya kupata maambukizi ya HIV, homa ya ini na kifua kikuu.
- Inaimarisha mwili na kumfanya mgonjwa kurudi katika hali yake ya kawaida
- Inaboresha mfumo wa mwili na kupunguza hatari za matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa kuzidisha kiwango
- Kuimarisha mfumo wa uzazi
- Kupunguza vifo vya ghafla vitokanavyo na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.
- Inasaidia kupunguza mzunguko wa pesa chafu kwa wauzaji na wasambazaji
- Huleta mabadiliko chanya ya tabiana kupunguza vitendo vya kihalifu na uvunjaji wa amani.
"Hizi ni nyumba ambazo waraibu wanaenda, halafu wanapatiwa huduma ili waache utegemezi wa dawa za kulevya ambazo wamekuwa wanazitumia. Lakini pamoja na hiyo kuna huduma ya counseling (ushauri) ambazo zinafanyika na tuna asasi mbalimbali za kiraia ambazo zimekuwa zikifanya kazi pamoja na sisi kama Serikali na kama mamlaka tumezitengenezea miongozo na tunazisimamia ili huduma hizo ziweze kuwafikia Watanzania wote kwa ujumla.
"Kwa hiyo, hayo ndiyo maeneo ya msingi ambayo tumekuwa tukiyafanya na sasa hivi Serikali imejikita kwa maana kwamba imeanza kusaidia waraibu waliopata nafuu waweze kupata mafunzo ya mbinu za kujitegemea kiuchumi, kupitia mafunzo ya ufundi stadi, kwa hiyo wanakwenda wanapata mafunzo ili kusudi waache matumizi ya dawa za kulevya na wawe watu wema waingie katika kuzalisha na kuongeza pato la Taifa. Kwa hiyo ni maeneo ya msingi ambayo tumekuwa tukishughulika nayo,"amefafanua Dkt.Nyandindi.