NA MWANDISHI WETU
RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt Jakaya Kikwete ametembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Seoul, Korea Kusini na kuzungumza na wafanyakazi.
Akiwa na mwenyeji wake Balozi Togolani Mavura, Dkt.Kikwete amewahimiza kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na kuunga mkono kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education) - GPE) yuko Seoul, Korea Kusini kwa ajili ya kukutana na viongozi wa Serikali na mashirika Mbalimbali ya Korea Kusini.
Lengo la kukutana na viongozi wa Serikali na mashirika ni kwa ajili ya kujadili mikakati ya kuendelea kuboresha elimu katika nchi zinazoendelea.
GPE ambayo ilianzishwa na nchi za G7 miaka 20 iliyopita, imeendelea kupigania elimu kwa ajili ya mtoto wa kike na wa kiume kwa kuomba kuungwa mkono na nchi na taasisi zinazoweza kuchangia katika elimu duniani.