Dkt.Mwinyi aendelea kukiimarisha chama Zanzibar, UVCCM wampa saluti

NA DIRAMAKINI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameendelea na ziara zake za kukiimarisha chama.

Sambamba na kutembelea miradi mbalimbali ya CCM ikiwemo kufanya mikutano ya ndani na kuzungumza na viongozi wa CCM,mabalozi,wajumbe wa halmashauri za CCM majimbo,wilaya na mikoa.

Katika mwendelezo huo Mei 13, 2023 katika ukumbi wa Amani Mkoa, Wilaya ya Mjini, Unguja alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya shina hadi mkoa amesisitiza kuwa,umoja miongoni mwa wanachama wa CCM ni muhimu katika kupata ushindi wa kushika dola.

Pia, Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar amelaani wanachama wanaoleta viashiria vya makundi ndani ya chama hicho.

Dkt.Mwinyi ameelekeza kuanza kwa mafunzo kwa viongozi wa CCM ngazi zote, kuingiza wanachama wapya, wanachama kujiunga na CCM na kuhamasisha wananchi waliotimiza miaka 18 kujiandikisha katika daftari la Wakaazi.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa Serikali kutimiza ahadi zilizotolewa kwa wananchi kupitia ilani ya uchaguzi.

Amegusia pia suala la uchumi ndani ya chama, akisisitiza umuhimu wa kutumia rasimali zilizopo kwa kuongeza vipato na kuepuka hali ya chama kuwa ombaomba. Akihimiza vikao vya chama kufanyika kikatiba kwa ngazi zote, ameelekeza Sekretarieti ya CCM kusimamia hilo.

Rais Dkt.Mwinyi amesema, Serikali itajenga Barabara za Juu Flyover Zanzibar, ukarabati wa Uwanja wa Amaan kuwa wa kisasa kwa viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), ujenzi wa ukumbi wa kisasa wa Kimataifa wa Mikutano Zanzibar na uwekezaji wa eneo la CCM Amani Mkoa.

Wakati huo huo, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amekabidhi kadi 500 kwa wanachama wapya waliojiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika ukumbi huo.

Mbali na hayo, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Zanzibar umempongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Mwinyi kwa juhudi endelevu za kuimarisha sekta ya michezo nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Mussa Haji Mussa, amesema kuwa Rais Dkt.Mwinyi ameendelea kuimarisha sekta ya michezo ili vijana wapate nafasi ya kuonyesha uwezo wa vipaji vyao kupitia sekta hiyo.

Mussa alieleza kwamba juhudi hizo za kuwekeza katika michezo ni hatua kubwa na muhimu inayotakiwa kuthaminiwa na kupongezwa kwani, vijana wengi watapata nafasi ya kujiajiri wenyewe kupitia sekta hiyo.

"UVCCM Zanzibar tunampongeza kwa dhati Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Mwinyi, kwa maamuzi yake sahihi ya kuendelea kuwekeza katika sekta ya michezo kwa kujenga miundombinu rafiki ya michezo katika maeneo mbalimbali nchini,"alisema Naibu Katibu Mkuu Mussa.

Alifafanua kwamba ukarabati wa viwanja vya michezo mbalimbali katika viwanja vya Taifa vya Amaan cha Unguja na Gombani kwa upande wa Pemba, ni hatua kubwa ya kimaendeleo katika sekta hiyo itakayotoa nafasi ya kuendelea kuchezwa ligi mbalimbali nchini katika mazingira rafiki.

Pamoja na hayo Naibu Katibu Mkuu Mussa, alisema dhamira ya kufanya mapinduzi ya kimaendeleo katika michezo ilianza kustawi pale Rais Dkt.Mwinyi, alipofanya harambee ya kuchangia ligi kuu,ujenzi wa viwanja vya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini.

Sambamba na hayo Naibu Mussa,alieleza kwamba hatua hizo sio za kufikirika bali ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 ukurasa wa 245,ibara ya 187 kipengele cha michezo vifungu vidogo vya (a) hadi (k) vinavyoeleza kwa kina dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ya michezo.

Aidha, aliwasihi vijana wa makundi yote nchini kuheshimu,kuthamini,kushiriki kikamilifu masuala ya michezo pamoja na kutunza miundombinu ya michezo ili iweze kudumu na kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news