NA MWANDISHI WETU
IMEELEZWA kuwa elimu inapaswa kuendelea kutolewa katika jamii kupinga vitendo vya unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini ili kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya UKIMWI katika Taifa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt.Jim Yonazi mapema leo Mei 9, 2023 alipokutana na uongozi wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI nchini (NACOPHA).
“Afua mbalimbali za masuala ya UKIMWI zimeendelea kuonesha jitihada za Serikali katika mapambano haya, nitoe rai elimu iendelee kupewa kipaumbele ili kupinga unyanyapaa kwa WAVIU,”amesema Dkt.Yonazi.
Dkt.Yonazi ameongezea kuwa, ofisi yake itaendelea kutoa ushirikiano kwa NACOPHA ili kuhakikisha sifuri tatu zinafikiwa ifikapo 2030.
“Tutaendelea kushirikisha wadau mbalimbali lengo kuhakikisha tunayafikia malengo, na ofisi yangu ipo tayari kutoa ushirikiano wakati wote kuhakikisha masuala yote ya uratibu yanatekelezwa vizuri ili kuendelea kupambana na changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuhakikisha tunaondoa unyanyapaa katika jamii,”amesisitiza.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Bw.Deogratius Rutatwa amepongeza jitihada za Serikali kupitia uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu katika kurahisisha utendaji wa Baraza hilo.
“Hadi sasa tuna jumla ya wanachama laki sita na elfu sabini na mbili pamoja na vikundi vya WAVIU 3769 katika shughuli za kujipatia maendeleo yao ambavyo vinatoa fursa kushiriki katika shughuli mbalimbali na tunatumia kuhamasisha watu kuendelea kupima virusi vya UKIMWI na utumiaji wa dawa kwa wanaogundulika na maambukizi,”amesema Deogratius.