Anaaandika PhD Dkt.Ahmad Sovu
JANA tarehe 4, Mei, 2023 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge mbalimbali katika wizara yake, Mheshimiwa Abdallah Ulega ameonesha kwa vitendo kwa kutumia falsafa ya R4 ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa uamuzi kuwa serikali haitafunga shughuli za uzalishaji na uvuvi wa Samaki katika Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Ulega alisema na hapa ninanukuu,...Waambieni Wanatanganyika, Wavuvi wa ziwa Tanganyika waendelee na shughuli zao."
Kauli hii iliibua makwasa mengi, vifijo na nderemo kutoka kwa waheshimiwa wabunge kwa hatua hii maridhawa ya serikali kama ilivyotangazwa na Mheshimiwa Waziri, Abdallah Ulega.
Mheshimiwa Ulega hakuishia hapo aliendelea kusema;Jambo kubwa ambalo Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amekuwa akilisisitiza kwetu sisi wasaidizi wake ni kuto kuleta taharuki na amejenga msingi imara Dkt.Samia Suluhu Hassan wa zile ARA 4 kila mmoja anazijua hapa."
Aliendelea kusema...ikiwa yeye mwenyewe Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefungua milango anakaa na kila mtu anazungumza naye, anapata kufanya nae Reconciliation hata yale tulodhani ni magumu kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan yamekuwa ni mepesi Sasa mimi Abdallah Ulega ni nani nisijifunze."
..._alisema huku aki 😄😄👏👏👏
Naam huyu ndio Mheshimiwa Ulega akiidadavua na kuileza kwa utondoti na kwa mifano iliyo bayana falsafa ya R4 ya Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Kadhia ya Kutaka kufunga Ziwa Tanganyika ilivyokuwa
Ilielezwa kuwa Serikali ya Tanzania ina nia ya kutaka kufunga Ziwa Tanganyika, na kusudio hilo lilitokana na na vikao vya kikanda kwa nchi zinazolizunguka ziwa hilo.
Jambo kubwa lilielezwa kuwa nia yake ni kulifunga ziwa Tanganyika na kusimamisha shughuli zote za uvuvi kwa muda wa miezi 3 kuanzia mwezi wa 5 hadi wa 8 ili kuruhusu samaki wazaliane kwa wingi na masuala mengine ya kitaalamu.
Hali hiyo iliibua taharuki na sintofahamu kubwa kwa wana Kigoma na maeneo yote yanayolizunguka Ziwa Tanganyika.
Hali hyo ilimuibua juzi Mheshimiwa Ulega waziri mwenye dhamana ambapo alipoongea na Runinga ya TBC kuwa, amewasikia Wabunge wa Mkoa wa Kigoma na Katavi ambao ni wawakilishi wa wananchi kuwa sio Kuwa hawataki Ziwa kufungwa bali Ushirikishwaji wa wadau ili kupata uelewa wa pamoja na tija ya jambo hilo haukufanyika.
Hivyo, Mheshimiwa Ulega amewatoa hofu wana Tanganyika na kusema kuwa ziwa halitafungwa.
Awali, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini Mheshimiwa Kilumbe Shaaban Ng'enda alisema serikali hadi sasa haikuleta njia mbadala ya wananchi kukabiliana na jambo hilo.
Mheshimiwa Kilumbe alisema, mwanzo ilielezwa kuwa suala hili mbadala wake utakuwa ni ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ila hadi sasa hakuna vizimba hivyo.
Vilevile, Mheshimiwa Aidah Kenan mbunge wa Nkasi alisema ziwa Tanganyika ndicho kiwanda alichowaruzuku Mwenyezi Mungu watu wa Mikoa ya Kigoma, Katavi na kwingineko.
Kufunga ziwa hilo kungeweza kuleta athari kubwa za kiuchumi na kijamii kwa wadau hao wa Ziwa Tanganyika.
Binafsi niliwahi kuzungumza na mwananchi mmoja katika mwalo wa Kibirizi mkoani Kigoma nilipokuwa na dodosa juu ya nia hiyo ya serikali.
Mwananchi yule alinijibu akiwa katika hali ya kusawajika sana;
...Dokta kama kweli ndio Ziwa litafungwa kwa miezi hiyo 3 Wallah zijui itakuaje? Hapa nilipo nimechukua mkopo na ndio nimeanza biashara na tegemeo langu ili biashara itoke ni shughuli za hapa ziwani dah! Sijui itakuaje tusaidieni nyie ndio mko huko juu."
Alimaliza kusema akiwa ameonesha kukata tamaa kabisa ikiwa uamuzi huo utachukuliwa.
Hiyo ndio hali ya wana Kigoma na Wana Tanganyika ilivyokuwa. Kwa kifupi kila mmoja alikuwa akinung'unika kwa namna yake kufuatia hatua hiyo.
Maoni yao baada ya kupokea uamuzi huo
Kufuatia uamuzi wa serikali chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia waziri wake Mheshimiwa Ulega kuwatoa hofu na kutamka kuwa Ziwa halitafungwa.
Wana Kigoma wamepokea jambo hili kwa furaha kubwa sana.
Mwananchi wa 1 alisema;Nitumie fursa hii kuwapongeza na kuwapa hongera waheshimiwa wabunge wa Kigoma, Katavi na Rukwa kwa kulinenea jambo hili na hatimaye serikali sikivu na yenye huruma chini ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kusitisha jambo hili,kwa kweli ni kama uamuzi huu umetupatia ari mpya nasi tumejiona hasa serikali yetu inatusikia na inatujali.
Aliendelea kusema kuwa;Jambo hili lingeleta taharuki kubwa sio tu kwa wavuvi na wafabiashara bali pia kwa sisi wananchi wa kawaida wa mikoa hii alisema;
... Hapa Kigoma vipo vijiji kama vile Nyansimbi, Kasibamba, Mgondozi, Herembe, Mtanga, Kanyasi* n.k hawana shughuli yoyote ile ya kiuchumi na ya uzalishaji mali zaidi ya Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika ndio ofisi yao, ndio shamba lao, ndio duka lao, ndio barabara yao sasa sijui ingekuwaje_? Alisema mwananchi huyo.
Hivyo, anamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu kwa kusitisha jambo hilo.
Kwa upande wake mwananchi mwingine alisema:
_Wana Kigoma ambao kiutamaduni mtu kula chakula kwa siku japo tatu bila kupata kitoweo cha samaki au shombo😄😄 aaah! Ni muhali anaweza hata kuumwa sembuse kukaa miezi 3 na ukizingatia na hali zetu za uchumi_
Alisema kwa kweli Urakhoze yaani, Asante Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa huruma zake.
Hivi ndivyo falsafa ya R4 ya Dkt.Samia Suluhu inavyoweza kuondoa taharuki na sintofahamu kwa wananchi, ambapo msaidizi wake Mheshimiwa Waziri mahiri mwenye sauti ya kimamlaka Mheshimiwa Ulega ameitekekeleza kwa vitendo katika kuondosha tandabeluwa hii kwa wananchi wake.
Ziwa Tanganyika na dhana ya Uchumi wa Buluu
Kule Zanzibar chini ya Rais Dkt.Hussein Mwinyi kuna dhana ya uchumi wa BULUU na aliunda wizara mahsusi ya suala hilo.
Dhana hiyo kwa ufahamu wetu inasisitiza kutumia raslimali zote muhimu zinazotokana na bahari.
Tanganyika si bahari ni Ziwa ingawa wakazi wake huiita bahari, nayo inaweza kunufaika na aina hiyo ya uchumi ukizingatia mazao yanayopatikana humo.
Ufahari wa Ziwa Tanganyika ni kuwapo kwa dagaa wenye bei ghali duniani maarufu kama dagaa wa Kigoma, samaki maarufu aina ya migebuka, Kuhe, nonzi, Sangara, Ntanga, Nyika n.k.
Ni imani yetu wataalamu wetu wa wizara badala ya kuja na njia za mkato na za muda mfupi zenye lengo la kuongeza uzalishaji wa samaki, watatafakari na kufanya tafiti za kina kuhusu nini cha kufanya ndani ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mbunge Kilumbe alisema ni hivi karibuni ndio serikali imefanya utafiti wa kujua idadi ya samaki waliomo katika ziwa hilo, yaani stock assessment tu na bado matokeo ya utafiti hayajadhihirishwa bayana.
Pia, yapo maelezo ya kawaida ya kimazungumzo ya Wazee wa Kigoma kuwa kuna samaki wakubwa na wengi bado hawajavuliwa ndani ya ziwa Tanganyika.
Hali ya uvuvi
Zana na vifaa duni za uvuaji wa samaki katika ziwa hilo zinatajwa huenda bado kuna samaki wengi sana na wakubwa wa ziwa Tanganyika.
Uvuvi mkubwa katika ziwa hilo hutegemea nyavu, vipe, free mayaa, makira, mkwabo, ndoano n.k hivyo uvuvi wa kutumia zana bora na za kisasa haujafanyika.
Wazee wanakumbusha kuwa hapo zamani kulikuwa na kampuni au ni kama taasisi tanzu chini ya Halmashauri za uvuaji kama vile Yorogwe samaki wakubwa walivuliwa kwa wingi.
Pengine kadhia hii itoe kama shime na hamasa kwa Mheshimiwa Ulega na wataalamu wake wa wizara kwa kufikiria na kuanza kufanya uwekezaji wa kina katika ziwa Tanganyika katika suala hili la uvuvi.
Wizara inaweza kufanya yafuatayo
-Kutoa mikopo mikubwa na midogo kwa wavuvi,
-Kupata zana bora za uvuvi na za kisasa
- Kujenga viwanda vya usindikaji minofu,
-Kuweka mkakati madhubuti wa ufugaji samaki kwa njia ya vizimba (cages) kama ilivyofanya Mwanza katika Ziwa Victoria
-Kuwa boti zaidi za ulinzi na usalama,
-Kufanya tafiti za kuwapo kwa mafuta ndani ya ziwa hilo n.k
Haya yanaweza kuleta natija kubwa kwa serikali na kuleta nafuu zaidi ya maisha kwa wananchi wa Mikoa hii.✍️✍️ na hatimaye ile dhana ya UCHUMI WA BULUU Ikawa na manufaa kwa wananchi wa mikoa hii pia na Tanzania kwa ujumla.
Kwa sasa dagaa wa Kigoma mathalan, ni biashara kubwa duniani. Wadau wengi wananufaika na usafirishaji wa dagaa hawa pendwa duniani.
Ipo haja ya serikali kufanya majambo zaidi kwa ziwa Tanganyika licha ya juhudi kubwa zinavyofanya na Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kujenga meli mpya 2, kukarabati meli kongwe za Liemba na Mwongozo, kufikisha umeme wa gridi ya Taifa ili kuwa na viwanda vya uhakika, kuboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege n.k.
Falsafa ya Dkt.Samia ya 4R
Msingi wa falsafa hii umekitwa katika wazo lake aliloliasisi mwenyewe la falsafa ya 4R, yaani Reconciliation (maridhiano), Resilience (ustahamilivu), Reform (mabadiliko) na Rebuilding (kujenga upya).
Falsafa hii adhimu ya Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan ambayo shabaha yake kuu ni kuhimiza wakati mwingine kutokutumia nguvu badala yake kufanya siasa za kistaarabu na kuendesha mambo ya watu kwa njia shirikishi na kuwaweka watu pamoja, kujenga hoja na ushawishi na kujenga zaidi njia za kimajadiliano katika uendeshaji wa nchi.
Falsafa hii ni muhimu sana na nitoe mwito kwa viongozi wetu kuienzi na kuitumia kadri wawezavyo ili kuweza kuondosha sintofahamu, taharuki au tandabeluwa yoyote ile kwa jamii.
Heko kwa Mheshimiwa Waziri Ulega kuizingatia falsafa hii kwa kadhia hii ya Wana wa Kigoma, Katavi na Rukwa kwa kuondosha taharuki ya kufungwa kwa Ziwa Tanganyika.
Leo wananchi wana furaha na buraha kwa uamuzi huu maridhawa kwao wao.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aghalabu amekuwa akisisitiza kuacha vitisho na kuepuka kulewa madaraka na kujisahihisha.
Kwamba viongozi ni watumishi kwa wananchi. Wasiache kushuka chini na kuendelea kusikiliza kero zao.
Mwandishi ni Mhadhiri na Mshititi kutoka
Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi Kivukoni.
sovu82@gmail.com
0713400079