HAPPY BIRTHDAY BABA, HAPPY BIRTHDAY BABU

NA LWAGA MWAMBANDE

RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi leo anasherehekea miaka 98 ya kuzaliwa kwake, ikiwa ni miaka ya kumtukuza Mwenyenzi Mungu kwa kumpa afya na uzima tele katika kipindi chote cha maisha yake.

Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi ambaye alizaliwa mwezi kama wa leo 1925 huko Kivule, Mkuranga Mkoa wa Pwani kabla ya kustaafu aliwahi kuhudumu nafasi mbalimbali za utumishi wa umma nchini.

Aliwahi kuwa, mwalimu wa shule za msingi za Mangapwani na Bumbwini, Zanzibar. Kisiasa, mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alijiunga na chama cha Afro Shiraz (ASP) mwaka 1964 na kushika nyadhifa mbalimbali za Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Miongoni mwa nafasi hizo ni kama vile Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Zanzibar 1963, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1970 na kati ya mwaka 1982 hadi 1983 alikuwa Waziri wa Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Maliasili na Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Misri. Mwaka 1984 alichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande naye amejuika na Watanzania wote kumtakia maisha marefu, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi ambapo amesema ni umri wa kushiba na sote tunayo kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa maisha ya baba na mzee wetu. Endelea:


1.Happy birthday Baba, happy birthday babu,
Ni tisina nane baba, umefika taratibu,
Ni umri wa kushiba, sote tunayo sababu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

2.Tunamshukuru Mungu, ambaye kwako tabibu,
Akuzingira na wingu, siku zote yu karibu,
Na hajakuacha tangu, maisha ayaratibu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

3.Ni Ali Hassan Mwinyi, baba kwa wengine babu,
Rais wa pili Mwinyi, Ruksa jinale jibu,
Mpole wala hafinyi, wa mbali na wa karibu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

4.Huyu tena wa peke, hata katika vitabu,
Hadi sasa yuko peke, kwetu ameleta jibu,
Rais si hapa peke, Zanzibar aliratibu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

5.Malezi kwa wako wana, sisi tunayo sababu,
Ya kukushukuru sana, wanavyoleta majibu,
Walivyo vizuri sana, kazi zao ni majibu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

6.Ulikuwa ni Rais, kwa kazi si kujaribu,
Metuzalia Rais, Zanzibar kwao ni jibu,
Uchumi waenda kasi, wa Buluu ni ajabu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

7.Leo ukikata keki, na wakuitao babu,
Mungu tunambariki, jinsi alivyo karibu,
Akutunza unatiki, karne moja karibu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

8.Mungu tunakushukuru, na sisi uko karibu,
Watuangazia nuru, miaka twairatibu,
Zidi kutuweka huru, magonjwa yasitusibu,
Tunamshukuru Mungu, kwa maisha yako baba.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
Mei 8, 2023


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news