Kamati ya PIC yaguswa na ufanisi wa miradi ya NHC, Morocco Square wafikia asilimia 97

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) imeonesha kuguswa na kuridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) huku ikitoa wito kwa watumishi wa shirika hilo wakiwemo wale ambao wanaajiriwa kwa kipindi fulani kufanya kazi kwa bidii,uadilifu na ubunifu.
Hayo yamebainishwa Aprili 30, 2023 na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Jerry Silaa baada ya kamati hiyo kutembelea miradi inayoendelea kutekelezwa na shirikia ukiwemo ukamilishaji wa majengo ya makazi na vitega uchumi ya Morocco Square, Samia Housing Scheme na 7/11 Kawe yaliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. 

"Kwanza tumpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuifufua miradi hii, kwani mahitaji ya nyumba kwa Tanzania bado yako juu sana, la pili shirika hili la nyumba (NHC), ndio shirika mkombozi la nyumba kwa Watanzania, zipo njia mbili za kumiliki nyumba.
"Kutafuta kiwanja chako mwenyewe na kujenga mwenyewe kuishi au kutafuta nyumba, Shirika la Nyumba la Taifa ambao watakuwa wamekufanyia kazi zote wewe ni kuchukua funguo na kuishi ili muda wako wa kusimamia mafundi ufanye kazi zako za kukuingizia kipato.

"Kazi hizi zinaenda vizuri sana, tumeona kama hama NHC wanajenga wenyewe gharama za ujenzi ziko chini. Tumemuona Engineer Grace anafanya kazi, kina mama wengine pia wapo wanafanya kazi hapa na wafanya kazi wote kwa asilimia 100 zaidi ya vijana 300 wanafanya kazi hapa ni Watanzania.

"Wito kwenu watumishi ni kuhakikisha mnafanya kazi kwa uadilifu, uadilifu sio tu kutokuiba nondo hata unapofuma ile nondo kwa makosa maana yake unatengeneza hasara ya miaka 50, baadae kama nyumba ilipaswa ikae miaka 100 inaweza ikaa miaka 90 na miaka 10 ikapotea kwa kutoonyesha uadilifu.
"La pili, kwenye kila kazi unayoifanya hapa uifanye kwa bidii, kama utafanya kazi kwa masaa yaliyopangwa maana yake na mradi utakamilika kwa wakati.

"Muda wa kazi tuchape kazi, tunaposema NHC mkandarasi wa NHC ni yeye mwenyewe ni mkandarasi na wafanyakazi wazawa, lazima tufike wakati tuoneshe kazi ya mzawa ni nzuri kuliko kazi ya mgeni. Mkikosea hasara itakuwa kubwa.

"Niwapongeze sana, niwatie moyo tuchape kazi, tuendelee kujenga taifa mradi huu una jina la Rais wetu Dkt.Samia Suluhu Hassan ukiisha uishe kwa wakati na ufanane na sifa na heshima anayoifanya Rais wetu kwenye kujenga taifa letu.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Silaa ametoa wito kwa Serikali kuhakikisha miradi inayotekelezwa na mashirika au taasisi za umma za kibiashara kuendelea kuiunga mkono.

"Wito wetu pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha miradi kama hii na mashirika kama haya ya kibiashara yakiwa yanafanya mipango yake Serikali iunge mkono. 
Pia, Mheshimiwa Jerry Silaa amebainisha kuwa, kamati imefurahishwa na utekelezaji huo wa miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwani ndani ya Morocco Square ambao ni mradi mkubwa na kisasa uliofikia zaidi ya asilimia 97 mambo yaliyotendeka huko ndani ni makubwa.

"Mradi wa Morocco Square ni wa kisasa, wenye jengo la makazi, ofisi, hoteli na shopping mall kazi imefanyika nzuri sana, lakini mradi wa 7/11 Kawe ambao ni maarufu sana tumeona maghorofa yamekaa muda mrefu na tunatarajia utekelezaji utaanza karibuni.
"Ziara hii chimbuko lake ni shirika lilifika kwenye Kamati ya Bunge na baadhi ya mambo tuliyoyaona ni hii miradi iliyokaa kwa muda mrefu, lakini sasa miradi hii imeanza kutekelezwa mradi wa Morocco mmeona mkandarasi anaendelea na kazi, mradi wa 7/11 unakaribia kuanza na mradi wa Samia Housing Scheme unaendelea kujengwa."

"Kwa hiyo, mara nyingine mashirika haya ya umma yameundwa kufanya kazi ya kutengeneza faida, kwa hiyo tunapounda shirika tunaweka wakurugenzi, bodi wakati mwingine tuyaaamini tuache yafanye mipango yao kwa sheria ya Bunge ili wafikie malengo bila kuingiliwa.
"Intervasion ya 7/11 Kawe na Morocco Square yameligharimu taifa na mambo kama haya lazima yasemwe ili baadae na sisi viongozi tukiwa tunafanya maamuzi tuwe tunafanya kwa umakini ili kutowaingizia Watanzania wa kawaida hasara kwa sababu haya mashirika ya umma mwenye mali yake ni Mtanzania, faida ni ya Mtanzania na hasara ni ya Mtanzania,"amefafanua Mheshimiwa Silaa.

Mkurugenzi NHC

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Taifa (NHC),Hamad Abdallah ameishukuru Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa kutenga muda wa kutembelea miradi ambapo wameonesha wanathamini majukumu yao ya kusimamia utekelezaji wa miradi.
Pia, Abdallah amesema wamekuwa wakipokea ushauri mzuri kutoka kwa kamati kwa ajili ya kuboresha utekelezaji wa miradi ya nyumba ili iweze kuwa tija.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, awali walikuwa na majadiliano ya utendaji wa Shirika la NHC na kamati ambapo wamejadili miradi mitatu ikiwemo Morocco Square ambao ni mradi wa kipekee ndani ya Tanzania na Afrika Mashariki.
"Kwa niaba ya Menejimenti ya Shirika la Nyumba la Taifa vile vile na Bodi ya shirika niwashukuru kwanza Kamati ya Bunge kwa kutenga muda wao leo ni siku ya Jumapili wangekuwa kwenye ibada, lakini wamethamini majukumu ambayo wamepewa na taifa hili ya kusimamia mashirika ambayo yanafanya uwekezaji.

"Kwetu sisi kwa kweli tunashukuru sana, na tumekuwa tunapata mawazo chanya kutoka kwenye kamati tulikutana nao Dodoma walipotembelea mradi wetu wa Iyumbu tulipata mawazo mazuri sana ambayo tunayafanyia kazi.
"Pia tumekuwa na majadiliano kuhusina na utendaji wa shirika vile vile tuliangazia kwenye miradi mitatu. Morocco Square ambao ni mradi wa kipekee kabisa Tanzania na East Africa huwezi kukuta mradi mkubwa ambao una sehemu ya shopping mall, sehemu ya hoteli ya kisasa, sehemu za ofisi na sehemu za makazi katika msingi mmoja, ni jengo la kipekee kabisa pia lina ubora wa hali ya juu.

"Wameweza kuona viwango ambavyo tumevifikia kama shirika ni mradi mkubwa wa kutolea mfano na tunatarajia ndani ya muda si mrefu tutaanza kuruhusu wapangaji katika maeneo ya shopping mall wataanza kukamilisha maeneo madogo yaliyosalia na kuweka shelfu zao kwa ajili ya kuanza biashara.
''Ukiwa unapita nje unaweza ukadhani hakuna kitu kinachofanyika,lakini mradi umeshakamilika kwa asilimia 97, asilimia tatu ni vitu vidogo vidogo tu ambavyo tunavimalizia."

Kwa upande wa Mradi wa Samia Housing Scheme, Mkurugenzi Mkuu wa NHC amesema kuwa, "Pia mradi wa Samia Housing Scheme tumetoka foundation, sasa hivi tunakwenda ghorofa ya kwanza, matarajio yetu ambayo ndio commitiment tunayo kutoka kwa makandarasi wetu wa ndani kila floor moja tutakuwa tunajenga kwa siku 15, yaani ile slabu na wakati huo tunamwaga slabu chini tutakiwa tunafanya finishing ili tuweze kumaliza ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, mradi ambao ni nyumba takribani 560 uweze kukamilika.
"Lakini kwa taarifa tu ya awali na pia ni vizuri Watanzania wakaanza kuchangamkia hizi fursa, niseme tayari huu mradi mnaouona tumeshauuza kwa asilimia 80 maana yake kuna kiu kubwa sana ya makazi kwa Dar es Salaam na maeneo mengine ya Tanzania.

"Kwa hiyo niwahakikishie tu wanunuzi ambao tumeshawapata kwa asilimia 80 mradi tutaumaliza kwa wakati, lakini kwa viwango ambavyo tumekubaliana,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa NHC.
Akizungumzia Mradi wa 7/11 Kawe, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema, "Lakini tuna mradi wa Seven-Eleven Kawe, ni mradi ambao ulikuwa umesimama toka mwaka 2017, bahati nzuri tumepata sapoti kubwa sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita wameweza kukwamua hiyo miradi na matarajio yetu itakapofika mwezi wa saba, mwaka huu mkandarasi atakuwa amerudi saiti na kuendelea na ule mradi.

"Ni moja ya miradi ya vielelezo vile vile ni mradi wa nyumba 422 za makazi na tutakuwa na maeneo ya biashara sehemu ya chini, lakini sehemu ya mbele tutakuwa na maeneo kwa ajili ya michezo maeneo ya kisasa kabisa.
"Kwa hiyo Mwenyekiti wa Kamati nikushukuru na nikuhakikishie miradi hii tutaisimamia kwa gharama sahihi kama ulivyoona hapa materials tunayanunu moja kutoka viwandani, lakini pia tumeajiri Watanzania hii ni awamu ya kwanza ya Watanzania 300.

"Lakini karibuni tutaanza kwenda usiku na mchana, maana yake mchana tunaweza kuwa na watu takribani 500 usiku takribani 500. Na mwisho wa siku tunaweza kuwa na ajira 1000 ambazo zitakuwa zimezalishwa kutokana na mradi huu.
Kupitia miradi hiyo hususani ule wa Morocco Square ambao umefikia asilimia 97 kwa sasa, DIRAMAKINI imeshuhudia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa ambapo mbali na ujenzi kuzingatia ubora na viwango vya Kimataifa, pia wameimarisha mifumo yote ya kutolea huduma kisasa ikiwemo njia za kubaini na kukabiliana na majanga mbalimbali.
Uwekezaji huo, ndio uliowafanya wajumbe wengi wa kamati kuvutiwa zaidi na mradi huo huku kila mmoja akionesha utayari wa kutaka kununua nyumba ya makazi kupitia mradi huo ambao unampa mkazi wa eneo hilo hadhi ya kipekee na kumrahisishia kupata mahitaji yote ya muhimu katika sehemu moja.

Pia, NHC wameonesha dhamira ya kuhakikisha wanaunganisha miradi yake na gesi asilia ikiwemo Mkongo wa Taifa ili kuwezesha wakazi husika kuneemeka zaidi.
"Mpango wetu tutafanya provision kwa ajili ya gesi ndio Dunia inavyokwenda, ukienda nchi nyingine duniani zilizoendelea huwezi kuona vidishi juu ndio maana Serikali imeweka Mkongo wa Taifa sio ubaki tu umewekwa lazima utumike na gharama zake ni za chini sana.

"Kupitia Mkongo wa Taifa utaunganishwa na intaneti, simu na vitu vingine na sisi vile vile mradi huu tutafanya kazi na watu wa TTCL kuhakikisha nyumba hizi zinaunganishwa na Mkongo wa Taifa, kwa hiyo ukifika baada ya miaka 10 haya madishi yatakuwa yameondoka.
"Tutaingia kwenye ulimwengu ambao kila kitu unahitaji intaneti, hizo provision zipo tunatambua pia kazi inayofanywa na Serikali kusambaza gesi asilia, sasa isiishie kusambaza lazima tuwafikishie kabisa watumiaji. 

"Tunaangalia pia kitu gani kipya kila siku kinaingia kwenye real state, hivyo navyo tutaendelea kuvifanya kadri inavyowezekana,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu wa NHC.

PIC tena

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya PIC,Mheshimiwa Jerry Silaa amesema, kamati yake imefarijika zaidi kuona kuwa, miradi mingi inayotekelezwa na NHC inaajiri wazawa na kutumia malighafi za ndani kwa wingi.
"Mbali na kutatua changamoto ya makazi jijini Dar es Salaam, vile vile mradi umeajiri Watanzania wazawa tunaye project manager (meneja mradi),Engineer (mhandisi) Grace ambaye ni mwanamke ambaye anauendesha mradi huu wa Samia Housing Scheme vizuri sana.

"La pili tumeona suala la kujali afya za wafanyakazi lipo vizuri sana, kuna shirika tuliwahi kulitembelea tukakuta wafanyakazi wana helmemt mpya, buti mpya sasa tukashangaa...lakini hapa ukiangalia hakuna usanii, hivi vifaa watu wanavitumia kila siku.
"Kwanza mradi huu umeleta ajira, wako wa miezi minne ambao wanamsaidia engineer, wako wa skilled work wanasuka chuma na nyingine na wapo Watanzania wanapata riziki kutokana na mradi huu.

"Kwa hiyo Samia Housing Scheme itatatua tatizo la nyumba, lakini wapo watu wanapata riziki kupitia mradi huu wako 300, lakini mradi huu tunaamini utakuwa na awamu ya pili, uzoefu mtakaoupata hapa kwanza mtautumia mtaani na kufanya kazi, pili mtautumia kupata kazi eneo lingine.
"Niwapongeze NHC kwa sababu mradi huu ni wa Shirika la Nyumba la Taifa, lakini mkandarasi ni wa Shirika la Nyumba la Taifa. Mnapoona materials yananunuliwa moja kwa moja kiwandani maana yake gharama zinapungua.

"Sisi wote ni viongozi, moja kati ya mambo ambayo mashirika mengi ya umma yanafanya fanya michezo ni sehemu ya manunuzi, kwa hiyo unapokuta cement inetengenezwa sehemu nyingine, lakini anauza mtu mwingine na analeta mtu mwingine maana yake kwa mchezo huo huo gharama zitaongezeka na gharama hizo atazibeba Mtanzania wa kawaida.
"Hapa NHC kila kifaa wananunua kwa mzalishali moja kwa moja na matokeo yake gharama zinapungua. Pia tumeona form work zenu mnaform work za chuma maana yake zitajenga floor zote 10 na zitabaki kwenye shirika na mneniambia vile vile hata form work za slab ni za chuma, hiyo peke yake inaonesha jinsi gani Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi mko makini kwenye matumizi ya fedha za walipa kodi.

"Shirika la umma maana yake nini, ni shirika ambalo lina pesa ya Watanzania sisi Kamati ya Uwekezaji wa Umma tunaangalia mitaji yenu umma na umma ndio huu, watu wote fedha ambayo Serikali inapata inawekeza kwenye mashirika haya kwa hiyo pesa zinazotimika hapa ni pesa zetu yaani Watanzania,"amefafanua Mheshimiwa Jerry Silaa huku akiwapongeza NHC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news