Kamishna David Kafulila afunguka kuhusu PPP mbele ya wahariri

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) chini ya Wizara ya Fedha na Mipango, David Kafulila amesema, Serikali inatarajia kufanya marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership (Amendment) Act, No. 9 of 2018) iliyofanyiwa maboresho mwaka 2018 ili kuongeza kasi ya kuvuta mitaji, teknolojia na weledi katika miradi na huduma mbalimbali nchini.

Miongoni mwa majukumu ya Idara ya PPP kulingana na Sheria ya PPP Sura 103 ni kusimamia, kuchambua na kuzishauri mamlaka za Serikali katika uanzishwaji, uchambuzi na utekelezaji wa miradi ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi na kuratibu maandalizi na mapitio ya sera, sheria,mikataba na miongozo ya utekelezaji wa PPP.
Ameyabainisha hayo leo Mei 16,2023 alipokutana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi kilicholenga kueleza majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake nchini.

Sifa za PPP

Kamishna Kafulila akifafanua amesema, PPP ina sifa zake, kwamba Serikali ina majukumu fulani fulani ambayo inaweza ikayaacha yakafanywa na sekta binafsi na yenyewe ikafanya baadhi ya majukumu ambayo sekta binafsi haiwezi kuyafanya.

"Sasa PPP au huu ubia una sifa zake, sifa ya kwanza ni mkataba wa muda mrefu, lakini sifa ya pili ni kwamba kuna risks sharing, kuna mambo kwa sekta binafsi ikiyafanya kuna risks inazibeba na kuna risks ambazo inaziachia Serikali, risks kwa maana ya vihatarishi.

"Lakini, vile vile ni performance base, kwa kawaida mikataba ile ni performance base unapofanya vizuri unalipwa kwa kadri unapofanya. 

"Sasa, jambo hili la PPP kwa nchi yetu limeanza kutamkwa tangu Awamu ya Nne,kwa maana ya practice, practice ipo tangu Awamu ya Kwanza. Tangu Awamu ya Kwanza tumekuwa na huduma fulani fulani ambazo Serikali ina ubia na Sekta Binafsi, ubia kwa maana ya Serikali na mamlaka zingine, huduma ambazo zinatolewa kwa ubia.

"Sasa hizo huduma kwa maana ya elimu au afya katika Serikali ya Awamu ya Kwanza zilikuwa zinafanywa kwa taratibu pasipokuwa na sheria mahususi ambayo inasimamia ubia huo, lakini pia kwenye Serikali ya Awamu ya Pili,tuliendelea na kufungua uchumi wa soko, kwa hiyo hiyo dhana ya ubia ikatanuka zaidi, tukapata mitaji kutoka nje na kutoka ndani kwa maana ya sekta binafsi ikaingia kwenye kufungua uchumi wa soko, dhana ikatanuka zaidi.

Awamu ya Tatu ikafanya mageuzi makubwa, ikatengeneza taasisi nyingi ili kuratibu ubia baina ya Serikali na sekta binafsi, Awamu ya Nne ikaendelea, Awamu ya Tano na sasa Awamu ya Sita. Sasa, Sera Mahususi ya Ubia imetengenezwa mwaka 2009 kwenye Awamu ya Nne, Rais wa Awamu ya Nne ndiye ambaye alileta Sera ya Ubia kwamba tuwe na Sera Mahususi.

"Moja wapo ya sababu ni uzoefu mbaya ambao tuliupata kwenye baadhi ya mikataba ambayo ilitangulia huko nyuma, kwa hiyo tukaona tuwe na Sera Mahususi ili kusimamia dhana ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. 
"Tukatunga sheria mwaka 2010 na tukatunga kanuni mwaka 2011, lakini baadaye sheria hiyo ya ubia ikaja ikafanyiwa marekebisho ya kwanza mwaka 2014 na kanuni zake zikatungwa mwaka 2015, lakini baadae kutokana na mahitaji na mabadiliko ya Dunia, Sheria ikafanyiwa marekebisho ya pili mwaka 2018 na marekebisho ya tatu ndiyo tunayafanya sasa.

"Mtu anaweza kujiuliza kwa nini mnafanya marekebisho kila wakati pengine ni kutokana na nature ya sheria yenyewe ambayo inahusu ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi.

"Kwa hiyo, msingi mkubwa ni kuvuta mtaji, kuvuta teknolojia, kuvuta weledi katika uendeshaji wa huduma za Serikali katika baadhi ya maeneo, sasa kwa sababu mitaji duniani inagombaniwa, sasa nchi zinazoshindana kutafuta hiyo mitaji, pia zishindane katika kutengeneza mazingira. Wewe unaweka kifungu hiki, mimi ninaweka kifungu hiki, mwenzako anaweka kingine anavuta zaidi mtaji kuliko wewe, kwa hiyo mabadiliko haya msingi wake ni huo. 

Sasa hivi tunafanya mabadiliko makubwa na miongoni mwa maeneo ambayo yanafanyiwa marekebisho ni pamoja ni kifungu cha sheria ambacho kiliwekwa kikawa kinazuia ukitokea mgogoro baina ya sekta binafsi na Serikali, maamuzi lazima yafanywe kwa sheria za ndani na vyombo vya ndani.

"Sasa kwenye ushindani huko duniani, mambo hayapo hivyo, kwenye ushindani huko duniani ni kwamba ili mwekezaji aje nchini hata kama ni wa ndani ya nchi anahitaji comfort kwa sababu anaweka mtaji mkubw, na anaweka mtaji mkubwa pengine miaka 15, 20, 30 na hata pengine, kwa sababu hiyo anahitaji mazingira ya kisheria ambayo yanampa dhamana,"amefafanua kwa kina Kamishna Kafulila. 

Eneo linaotazamwa

Kamishina Kafulila amefafanua kuwa, "Kwa hiyo miongoni mwa maeneo ambayo yalikuwa yakisumbua ni pamoja na kifungu hiki cha kulazimisha kwamba ukitokea mgogoro baina yake na Serikali, lazima maamuzi yafanywe kwa sheria za ndani na vyombo vya ndani. 
"Wakati huo Dunia tuliyopo kuna vyombo vya Kimataifa ambavyo vinahusika na usuluhishi wa migogoro ya kibiashara, kwa hiyo kama nchi, tumekuwa mwanachama wa vyombo hivyo tangu mwaka 1992, 

"Tanzania ni mwanachama wa International Centre for Settlement of Investment Disputes (ICSID) tangu mwezi 5 mwaka 1992, kwa hiyo tangu tunaingia katika mfumo wa vyama vingi tulikuwa tayari tulikuwa tumeshakubaliana kujenga uchumi ambao unaruhusu kujenga usawa wa kufanya biashara kati ya sekta binafsi na Serikali,"amesisitiza Kamishna Kafulila.

ICSID nini?

ICSID ndiyo taasisi inayoongoza duniani inayojishughulisha na utatuzi wa migogoro ya uwekezaji wa kimataifa. Ina uzoefu mkubwa katika nyanja hii, ikiwa imesimamia kesi nyingi za uwekezaji wa kimataifa. 

Mataifa yamekubaliana kuhusu ICSID kama jukwaa la utatuzi wa migogoro ya wawekezaji na Serikali katika mikataba mingi ya kimataifa ya uwekezaji na katika sheria na mikataba mingi ya uwekezaji.

ICSID ilianzishwa mwaka 1966 na Mkataba wa Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji kati ya Mataifa na Raia wa Nchi Nyingine (Mkataba wa ICSID). 

Mkataba wa ICSID ni mkataba wa kimataifa ulioundwa na Wakurugenzi Watendaji wa Benki ya Dunia ili kuendeleza lengo la benki la kukuza uwekezaji wa kimataifa. 

Pia, ICSID ni taasisi huru, isiyo na siasa na yenye ufanisi ya utatuzi wa migogoro. Upatikanaji wake kwa wawekezaji na mataifa husaidia kukuza uwekezaji wa kimataifa kwa kutoa imani katika mchakato wa kutatua mizozo. 

Inapatikana pia kwa mizozo ya serikali chini ya mikataba ya uwekezaji na makubaliano ya biashara huria, na kama sajili ya kiutawala.

ICSID inatoa utatuzi wa migogoro kwa upatanishi, usuluhishi au kutafuta ukweli. Mchakato wa ICSID umeundwa kuzingatia sifa maalum za migogoro ya kimataifa ya uwekezaji na wahusika wanaohusika, kudumisha uwiano makini kati ya maslahi ya wawekezaji na nchi mwenyeji. 

Kila kesi inazingatiwa na Tume Huru ya Upatanisho au Mahakama ya Usuluhishi, baada ya kusikiliza ushahidi na hoja za kisheria kutoka kwa wahusika. 

Timu iliyojitolea ya kesi ya ICSID imepewa kila kesi na hutoa usaidizi wa kitaalamu katika mchakato mzima. Zaidi ya kesi 900 kama hizo zimesimamiwa na ICSID hadi sasa.

ICSID pia inakuza ufahamu zaidi wa sheria za kimataifa kuhusu uwekezaji wa kigeni na mchakato wa ICSID. Ina programu pana ya machapisho, ikijumuisha Jarida kuu la Sheria ya Uwekezaji wa Kigeni wa ICSID na huchapisha mara kwa mara taarifa kuhusu shughuli na kesi zake. 

Wafanyakazi wa ICSID hupanga matukio, kutoa mawasilisho mengi na kushiriki katika makongamano kuhusu utatuzi wa migogoro ya uwekezaji wa kimataifa duniani kote.

Kafulila tena

Pia Kamishna Kafulila amesema, kutokana na umuhimu wa sekta binafsi, Serikali lazima itafute njia ili kuhakikisha sekta hiyo inaondolewa vikwazo.

“Lazima Serikali itafute njia ambazo inaweza kuhakikishia sekta binafsi inakuwa, ndio maana imekuwa ikifanya marekebisho ya sera yake mara kwa mara,”amesema Kamishna Kafulila.

Amesema, ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi kwa kiwango kikubwa, unasaidia kupunguza msongamano, mvutano na migogoro kati ya sekta za Serikali, pia kusaidia watu kupata huduma kwa urahisi na haraka zaidi.

Akizungumzia Tanzania na ujenzi wa miradi mikubwa, Kamishna Kafulila amesema, bado Tanzania inayo nafasi nzuri ya kuendela na ujenzi wa miradi ya namna hiyo kulinganisha na nchi nyingi za Afrika.

“Katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, Tanzania ipo vizuri kwenye kupima uzito wa deni, na tuna afadhali kubwa,"amebainisha.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema, kuna umuhimu mkubwa wa kulinda sekta binafsi kwa kuwa ndio inaendesha uchumi wa nchi.

Balile amesema, ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi unapaswa kuimarishwa na kuondolewa vimelea vyovyote vya uadui ambavyo vitachelewesha mipango mbalimbali.

Majukumu mengine ya PPP

Aidha, majukumu mengine ya idara hiyo ni kuchambua masuala ya kifedha kwenye miradi ya PPP inayohitaji fedha, msaada wa Serikali au masuala yoyote ya kisera.

Pia kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa vihatarishi na masuala mengine ya kifedha katika utekelezaji wa miradi ya PPP.5. Wakati huo huo, idara hiyo inahusika kuandaa kanuni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya ubia kwa mujibu wa Sheria ya PPP.

Kuandaa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini katika miradi ya PPP,kuratibu ufuatiliaji na tathmini ya miradi inayotekelezwa na mamlaka za Serikali kwa utaratibu wa PPP na kuandaa na kutekeleza programu ya kujenga uwezo wa PPP.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news