NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Jamhuri ya Kenya imeanza kampeni ya Kimataifa inayolenga kuvutia uwekezaji bora zaidi katika sekta mbalimbali nchini humo.
Hatua hiyo mpya, Rais Dkt.William Ruto amesema, itatoa faida nzuri kwa uwekezaji.Akizungumza wakati wa Kongamano la Wawekezaji wa Israel mjini Tel Aviv Jumatano, Rais Dkt.Ruto amesema Serikali ina nia ya kuifanya Kenya kuwa mojawapo ya vitovu vya juu zaidi vya biashara duniani.
"Tuna mfumo wa kisheria ambao unatoa ulinzi thabiti kwa haki za kumiliki mali na utaratibu thabiti wa utawala wa sheria,"amesema Dkt.Ruto.
Mbali na hayo,Mheshimiwa Rais Dkt.Ruto alibainisha, Kenya imetunga sheria za kulinda uwekezaji na kuweka huru mfumo wa kubadilisha fedha za kigeni.
"Sheria zetu zinaruhusu na kusaidia urejeshaji wa faida kwa makampuni ya kigeni," alisema. Rais Dkt.Ruto amesema kuwa, mfumo wa kodi nchini unakaguliwa mara kwa mara ili kuendana na mpango wa kukuza uwekezaji nchini.
Amewataka wawekezaji hao kuweka rasilimali zao nchini Kenya ikiwemo katika nishati mbadala, afya, maji na kilimo cha umwagiliaji pamoja na sekta za ICT.
"Pia tunafuata mpango wa ushirikiano katika utalii, utamaduni na urithi na utengenezaji wa filamu," aliongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Ruto.
Rais Dkt.Ruto alibainisha kuwa, Kenya ndio kivutio bora cha uwekezaji kwa biashara za kigeni kutokana na eneo lake la kimkakati, rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu na uthabiti.
"Kwa hiyo, niwaombe muelekeze nia yenu katika fursa za uwekezaji zenye manufaa makubwa nchini Kenya," Rais Dkt.Ruto alisisitiza alipokuwa akihitimisha ziara yake rasmi ya siku mbili nchini Israel.