NA FRESHA KINASA
WAKALA wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inaendelea kufanya kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya usambazaji wa maji ya bomba kwenye vijiji vya Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Hatua hiyo ni dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani katika kuchochea maendeleo.
Hayo yameelezwa Mei 5, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo. Ambapo Serikali imepongezwa na wananchi wa Musoma Vijijini kwa kuendelea kusambaza maji hayo ya bomba kwenye vijiji mbalimbali jimboni humo.
"Jimbo letu lenye kata 21, lina vijiji 68 vyenye vitongoji 374. Vijiji vyote vina miradi ya maji ambayo iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
"Bomba la Bujaga-Bulinga-Busungu maji ya bomba hili yanatoka Ziwa Victoria na mashine imejengwa Kijijini Bujaga (Kata ya Bulinga).
"Tenki la ujazo wa lita 200,000 limejengwa kijijini Busungu (Kata ya Bulinga) na lingine la lita 150,000 limejengwa kijijini Bulinga (Kata ya Bulinga).
"Maji kutoka kwenye matenki hayo ndiyo yanasambazwa kwenye Vijiji vya Bukima (Kata ya Bukima) na Kwikerege (Kata ya Rusoli)."
MRADI WA UPANUZI:BWASI-BUGUNDA-KOME.
"Upanuzi unafanyika ili maji ya bomba la Bujaga-Bulinga-Busungu yasambazwe na kutumiwa kwenye Kata ya Bwasi yenye Vijiji vitatu (Bugunda, Kome na Bwasi). Gharama ya mradi ni shilingi milioni 997,714,196.
"Urefu wa mtandao wa usambazajimaji ni kilomita 31.5 na vitekea maji 35.Tenki la ujazo la lita 150,000 linajengwa kijijini Bwasi na mradi huu umepangwa ukamilike kabla ya Juni 30,2023.
"Shukrani za dhati zinatolewa kwa Serikali yetu inayoongozwa na Mhe Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kusambaza maji safi na salama ya bomba vijijini mwetu," imeeleza taarifa hiyo.