Makamu wa Rais afungua Hospitali ya Wilaya ya Karatu, Ngorongoro Oldeani Mountain Lodge

NA MWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango tarehe 16 Mei, 2023 akiwa ziarani mkoani Arusha amefungua rasmi Hospitali ya Wilaya ya Karatu iliogharimu shilingi bilioni 3.37.
Akihutubia mara baada ya kufungua hospitali hiyo, Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuhakikisha huduma bora za afya zinasogezwa Jirani na wananchi pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika kila vituo vya kutolea huduma za afya. 
Ameagiza uongozi wa Wilaya na hospitali kusimamia kwa uaminifu dawa zinazoletwa na serikali kwa ajili ya matumizi ya wananchi ambapo kinyume na hapo serikali itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya kiongozi yeyote atakayebainika kukiuka sheria na miongozo iliyotolewa na serikali ya uendeshaji wa maduka ya dawa ya hospitali.

Makamu wa Rais amesema hospitali hiyo inalenga pia kusaidia watalii kuwa na uhakika wa kupata huduma ya kwanza na ya dharura kwa haraka katika mazingira salama pale itakapo hitajika. Pia ametoa wito kwa wananchi wa Karatu kutunza hospitali hiyo ili iweze kusaidia wananchi kwa miaka mingi ijayo.

Vilevile Makamu wa Rais ametoa wito kwa madaktari na wahudumu wa afya katika hospitali hiyo, kuwahudumia wananchi kwa upendo na uadilifu. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha vitendea kazi vinapatikana ili majengo yote yaanze kufanya kazi kama ilivyokusudiwa. 
Pia ametoa wito kwa wananchi, kushirikiana na uongozi wa Wilaya ili kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo na kuagiza viongozi katika ngazi ya vijiji na kata kuendelea kuimarisha kamati za afya za vijiji na kata ili zisaidie kuhamasisha afya ya wananchi.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais amefungua Hoteli ya kisasa ya hadhi ya nyota tano ya Ngorongoro Oldeani Mountain Lodge yenye uwekezaji wa shilingi bilioni 12 iliopo Karatu mkoani Arusha inayomilikiwa na kundi la Wellworth Hotel and Lodges ambayo ni kampuni watanzania.
Makamu wa Rais amewapongeza wamiliki wa Hoteli hiyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha utalii kwa kujenga miundombinu ya hoteli katika eneo la Karatu lenye idadi kubwa ya watalii. Pia amewapongeza wamiliki wa hoteli hiyo kwa kutoa ajira kwa watanzania na kuwajali kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya hoteli hiyo.
Pia amewaasa vijana wanaopata nafasi kufanya kazi katika hoteli za kitalii kuendelea kuwa waaminifu na mfano katika jamii kwa kuwa waadilifu na wachapakazi kila wanapopata fursa.

Aidha ametoa wito kwa wadau hao wa utalii kuendelea kushirikiana na jamii ikiwemo kuwasaidia wafugaji kuhakikisha wanafanya ufugaji wenye tija katika maeneo yao.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara ya kikazi mkoani Arusha yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news