NA MWANDISHI WETU
JKCI
WANANCHI wa Mkoa wa Manyara wameishukuru Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuwapeleka wataalam wa afya mabingwa wa moyo kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo.
Fundi sanifu wa moyo (Cardiovascular technologist ) wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Paschal Kondi akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi mkazi wa Manyara wakati wa kambi maalum ya siku tano inayofanywa na wataalam wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH).
Hayo yamesemwa na wananchi mbalimbali waliojitokeza katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) kwa ajili ya kupima moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano iliyoanza leo ikifanywa na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkazi wa Babati vijijini Andrea Tluway alisema ujio wa mabingwa kutoka JKCI kwake imekuwa fursa ya kuchunguza moyo wake kwani hakuwahi kupimwa moyo na amekuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu.
“Niliposikia matangazo ya kambi hii sikupuuzia hii nafasi, tofauti na kuwa na shida ya shinikizo la damu pia nimekuwa nikiona dalili tofauti tofauti katika mwili wangu kama mapigo ya moyo kupiga kwa haraka, maumivu makali upande wa kushoto wa kifua na moyo kuuma hivyo nikaona nivizuri leo nikapima moyo wangu kufahamu kama nina shida ya moyo,”alisema Andrea.
Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) Dkt. Yesiga Mutajwaa akizungumza na wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa MRRH kabla ya kuanza kwa kambi maalum ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo leo mkoani Manyara.
Aidha, Andrea amewashauri wananchi wa mkoa wa Manyara na mikoa ya jirani ambao bado hawajafika katika Hospitali hiyo kutumia nafasi hiyo yakipekee ambayo Serikali ya awamu ya sita imewapa wananchi wa Manyara kufikiwa na huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo.
Agnes Hamad mkazi wa Manyara alisema miaka mitatu iliyopita alivimba sehemu mbalimbali za mwili wake ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi ilionekana kuwa upande mmoja wa moyo umejaa maji na kupatiwa dawa ambazo baada ya kuzitumia na kurudi Hospitali aliona nafuu tofauti na alivyokuwa mwanzo.
Agnes anasema baada ya kusikia ujio wa Madaktari bingwa wa moyo wa JKCI akaone ni wakati sasa kufanyiwa vipimo vya moyo na mabingwa hao ili aweze kupata uhakika zaidi kama tatizo alilokuwa nalo mwanzo limeisha au anahitaji matibabu zaidi.
Wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) wakiwapima wananchi shinikizo la damu, sukari mwilini na mzunguko wa tumbo wakati wa kambi maalum ya siku tano inayofanywa na wataalam wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa MRRH.
“Naishukuru sana Serikali yetu kupitia Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kutuletea wataalam karibu ili tuweze kutumia gharama kidogo kuchunguza afya zetu tofauti na kama tungezifuata Dar es Salaam,"alisema Agnes.
Kwa upande wake Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Johnstone Kayandabila alisema JKCI imeweka utaratibu wa kuwafuata wananchi mahali walipo kusogeza huduma karibu na wananchi kuwasaidia wale ambao wasingeweza kupata nafasi ya kufuata huduma hizo JKCI kupata huduma.
Dkt. Johnstone alisema wakazi wa Manyara wamejitokeza kwa wingi na tayari siku ya kwanza wameshakutana na wagonjwa ambao wanahitaji kupewa rufaa kwenda JKCI kwa ajili ya matibabu zaidi.
Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Manyara wakiwa katika foleni ya kupata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo wakati wa kambi maalum ya siku tano inayofanywa na wataalam wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara.
“Kwa siku ya leo hadi mchana huu tumeshawapa rufaa watu wazima wawili mmoja akiwa na maumivu ya kifua na mwingine mfumo wake wa umeme wa moyo kuwa na hitilafu, pia watoto wawili ambao wana matundu kwenye moyo tumewapa rufaa waweze kufika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo,"alisema Dkt. Johnstone
Naye kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Manyara (MRRH) Dkt. Yesiga Mutajwaa alisema Hospitali hiyo inatamani kuwe na muendelezo wa ushirikiano baina ya JKCI na MRRH kwani MRRH bado ina changamoto katika ufanyaji wa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiogram – Echo)
Dkt. Yesiga alisema kupitia kambi hiyo wanaenda kuboresha mashirikiano kwani MRRH ikipata wagonjwa hasa wale wanaohitaji upasuaji wa moyo huwa hawana maamuzi nao zaidi ya kuwapa rufaa kufika JKCI kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo.“Kwa wiki hii moja naamini wataalam wetu watapata nafasi ya kujifunza lakini pia itatusaidia kufanya maamuzi kama tutawaomba JKCI warudi tena kwa ajli ya kutufundisha au sisi tupeleke wataalam wetu JKCI kupata uzoefu”, alisema Dkt. Yesiga