MAONESHO YA NACTVET ARUSHA, FURSA KWA WAZAZI NA WANAFUNZI KUJIFUNZA

NA MWANDISHI MAALUM

MKURUGENZI wa Mawasiliano na Masoko wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Mohamed Maguo, amesema Maonesho ya Pili ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), yamekuwa ni fursa kwa wazazi na wanafunzi wa mikoa ya Kaskazini kujifunza na kuelewa huduma, programu zinazotolewa, mifumo na utendaji kazi wa vyuo mbalimbali nchini.
Dkt. Maguo, ameyasema hayo Mei 17, 2023 wakati akitoa tathmini ya maonesho hayo kwa wageni waliotembelea banda la chuo hiki katika maonyesho hayo yanayoendelea katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Ameendelea kusema kuwa, maonesho hayo yamekuwa na mwitikio mkubwa tofauti na ilivyodhaniwa hasa baada ya kuwepo kwa hali ya mvua katika jiji la Arusha na kubwa zaidi ni kumiminika kwa wageni kutoka mikoa jirani na Arusha ya Manyara na Kilimanjaro.
“Banda letu la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, limekuwa ni miongoni mwa mabanda yanayopokea wageni wengi mpaka sasa na wanafika kujifunza kuhusu huduma, programu za masomo na mifumo ya ufundishaji na ujifunzaji ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania hali kadhalika kufanya maombi ya kujiunga na kozi mbalimbali. Kwa mwitikio huu ni dhahiri kuwa mwamko wa elimu hivi sasa hapa nchini umekuwa mkubwa,"alimaliza kusema Dkt. Maguo.

Akizungumzia maonesho hayo Mkurugenzi wa Kituo cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Mkoa wa Arusha, Dkt. Nangware Msofe, amesema kupitia maonyesho haya kumesaidia vyuo na taasisi mbalimbali zinazoshiriki kujitangaza katika ukanda wa Kaskazini na kujisogeza zaidi kwa jamii.
“Watu wengi hupata ugumu wa kutembelea vyuo moja kwa moja kutokana na vyuo husika kuwa katika mikoa mingine ambapo ni mbali na gharama ni kubwa kuvifikia hivyo kupitia maonyesho haya wananchi wamepata kuvifahamu vyuo vingi ambapo sasa watakuwa na uelewa wa huduma na kozi zinazotolewa na vyuo husika,” amesema Dkt.Msofe.

Aidha, Dkt. Msofe amewarai wageni wanaofika kutembelea maonesho haya kufika katika banda la Chuo kikuu Huria cha Tanzania kujionea mambo mazuri yanayofanywa na chuo hiki.
Maonesho ya Pili ya Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), yaliyoanza Mei 16, 2023 yanatarajiwa kumalizika Mei 22, 2023 katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, mwaka huu yamebeba kauli mbiu ya “Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa Nguvu kazi mahiri”, yamekutanisha vyuo na taasisi mbalimbali za elimu ya kati na juu hapa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news