Mawaziri wafunguka kuhusu bikoni wilayani Tarime

NA FRESHA KINASA

SERIKALI imesema kuwa, uwekaji wa vigingi ( bikoni) vya alama ya mipaka kwenye vijiji saba vya Wilaya ya Tarime vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mkoani Mara ni utekelezaji wa tangazo la Serikali namba 235 la mwaka 1968. 
Hivyo wananchi hawajaonewa kama ilivyokuwa ikisemekana.Vijiji hivyo ni pamoja na Nyandage, Kenyamosabi, Masanga, Karagatonga, Nyabirango, Gibaso na Kegonga. 

Hayo yamebainishwa Mei 6, 2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mheshimiwa Angellah Kairuki wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nyanungu kwenye mkutano wa hadhara ambapo mawaziri wa kisekta Kutoka Wizara tatu walifika kufuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Bungeni hivi karibuni ili kupata ukweli wa malalamiko ya Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliyedai zoezi hilo halikufuata utaratibu ikiwemo viongozi wa vijiji kutoshirikishwa. 
Mawaziri hao ni Waziri wa OR-TAMISEMI, Angellah Kairuki, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Mary Masanja. 

Mheshimiwa Kairuki amesema kwamba, katika uwekaji wa vigingi hivyo, hakuna jambo jipya lililoongezwa isipokuwa Serikali imeweka mipaka yake maeneo yale yale watu wavione na watambue mipaka halisi hata vizazi vijavyo vijue. Na hivyo amewataka wananchi kuheshimu sheria kwa kutoingilia katika eneo hilo.
Amesema, iwapo wananchi waliishi kwa mazoea ama kwa kufuata historia basi watambua kwamba Serikali imefanya hivyo katika kuhakikisha yanalindwa na hakuna mwananchi aliyeonewa bali ni utaratibu wa kisheria. 
Amewataka wananchi kutambua kuwa, vijiji vipo salama na kuwataka wanananchi waliolima katika maeneo ambayo mipaka hiyo imewekwa watakapovuna mazao yao, wasirudie tena kulima ama kufanya shughuli zozote kwani sheria za hifadhi haziruhusu.

Pia, ameongeza kuwa mipango bora ya matumizi ya ardhi lifanywe na wataalam katika maeneo hayo na pia TANAPA waendelee kujenga mahusiano mema na wananchi wanaopakana na hifadhi na kwamba Serikali kamwe haiwezi kuwaonea wananchi wake. 
Naye Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula, amemtaka mbunge wa Tarime Vijijini Mwita Waitara kuwa sehemu ya kuwaelimisha wananchi juu ya utunzaji wa alama za mipaka zilizowekwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Mary Masanja akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Gibaso amewataka kuheshimu sheria za nchi ikiwemo kutoingiza mifugo yao katika maeneo ya hifadhi, kwani ni kosa kisheria. 
Mheshimiwa Masanja amesema kuwa, Serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wale wanaovunja sheria kwa kuingiza mifugo yao katika maeneo ya hifadhi lengo ni kuhakikisha hifadhi zinatunzwa na kulindwa Kama rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi. 
Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mheshimiwa Mwita Waitara ametoa maombi kwa serikali kwamba, wananchi wa maeneo hayo wana changamoto ya maeneo ya kulima na kuchungia mifugo yao hivyo Serikali iwasaidie sambamba na GN itafisiriwe na wataalam kwa lugha ya Kiswahili waweze kuifahamu kwa urahisi. 
Aidha, Mheshimiwa Waitara ameomba jambo hilo litazamwe kwa busara sana, kwani lina tija katika kukifanya Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuchaguliwa na kuthaminiwa na wananchi hao. 
Awali Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee akitoa taarifa ya zoezi hilo, amesema limefanyika kwa amani na kwamba jumla ya bikoni 184 zimewekwa na imeonekana katika zoezi hilo kaya 87 zilikutwa ndani ya hifadhi pamoja na hekta za mashamba 408. 

Meja Suleiman Mzee amesema yapo maombi yaliyotolewa na Wananchi hao ni pamoja na Kuomba wachimbiwe mabwawa na visima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news