NA DIRAMAKINI
MBUNGE wa Momba, Mheshimiwa Condester Sichalwe (CCM) ameitaka Serikali kuwasaidia wabunifu wa pombe za kienyeji ikiwemo gongo kwa kufanya utafiti na kuzifungasha vizuri ili ziweze kupata soko.
Ameyasema hayo leo Mei 5,2023 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka 2023/24.
“Viwanda vinaanza na mtu wa chini wa kawaida, tuheshimu mawazo yanayotolewa na watanzania wenzetu, wanatengeneza K-Vant,”amesema.
Pia,ameitaka Serikali iwatumie wabunifu wa pombe wakiwemo ambao wamekuwa wakitengeneza vinywaji vinavyokaa siku tatu kwa kuwasaidia kuziboresha ili kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja.
“Najiuliza kwa nini pombe za gongo zinamwagwa, ubunifu si unaanza na wazo. Sio ndio maana wanatengeneza gongo?Kwa nini asipewe usaidizi wa ubunifu, kwani ubunifu unataka ni nini,"amehoji Mbunge huyo.