Michezo inahitaji afya njema

NA ADELADIUS MAKWEGA

MUUGUZI Mkuu wa Chuo Maendeleo ya Michezo Malya, kilichopo Kwimba mkoani Mwanza, Sonia Kabadi amesema ili kufanikiwa katika michezo na kupata tija, lazima suala la lishe na afya bora kwa wanaoshiriki michezo lizingatiwe.

Hayo yamesemwa leo Mei 5, 2023 kandoni mwa mafunzo wakati wakufunzi kadhaa wakifundisha wakurufunzi wa michezo katika chuo hicho pekee nchini Tanzania kinachotoa astashahada na stashahada. “Si unaona huyu binti ameumia, amefika hapa, tumempaka dawa ya na kumchua, sasa maumivu yale aliyougulia yatakwisha na pale alipoumia atapona na kesho atashiriki vizuri mafunzo na michezo yote, hilo litamtia moyo na ari ya kushiriki tena tena michezo. Hilo linamjenga kuwa mvumilivu na kujiamini. Kwa namna wanavyocheza kama hauna afya bora, utapigwa kikumbo na kudondoka, michezo inahitaji afya njema yenye lishe bora.”

Muuguzi huyu akiwa kando ya kiwanja cha Mpira wa Mikono, uwanjani hapo walionekana wakurufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya wakiendelea na mafunzo yao kwa vitendo yalidumu kwa dakika 120 katika somo la kuucheza Mpira wa Mikono (Hand Ball). 

“Ninakimbia hatua kati ya moja hadi tatu, alafu ninapaswa kuutupa mpira na yule mwenzangu anaupokea na yeye atakimbia hizo hatua kati ya moja hadi tatu na yeye atautupa kwa mwingine. Usipofanya hivyo utakuwa umekosea kanuni za Mpira wa Mikono.” Haya yanasema mkurufunzi Salehe Hamza anayesoma Stashahada ya Michezo chuoni hapa. Mkufunzi Idd Luswaga ambaye ndiye anayelifundisha somo hilo katika darasa lenye wakurufunzi 94 alisema, 

“Mafunzo haya ni ya hatua kwa hatu, somo ya Mpira wa Mikono linapokamilika baada ya majuma kadhaa mkurufunzi wangu atakuwa na uwezo wa kuucheza mchezo huo, kuuchezesha mchezo huo na mwisho kuufundisha mchezo huo popote ulimwenguni.” 

Wakati somo la Mpira wa Mikono likiendelea, darasa la Mpira wa Meza (Table Tennis) lilifanyika katika Viwanja vya Ndani chuoni hapo chini ya mkufunzi Somo Kimwaga aliyejimwaga katika kuufundisha mchezo huu kwa wakurufunzi wake 105. 
“Ninawaelekeza wakurufunzi wangu mambo mawili; kwanza kuupiga mpira kwa kuanzia nyuma (Back Ball) na kuupiga mpira kwa kuanzia mbele (Fore Ball), wakurufunzi wangu wengi ndiyo kwanza wanaucheza mpira huu kwa mara ya kwanza lakini nimewaondoa shaka baada ya majuma kadhaa watakuwa wajuzi wa Mpira wa Meza.” 

Mwandishi wa ripoti hii akiwa katika maeneo ambayo masomo ya Mpira wa Meza na Mpira Wa Mikono yakifundishwa amekutana na misamiati kadhaa ya michezo hiyo kama vile Ohhh ! Ahaaaa! Waaaa ! Usiniumizie ! Kaza msuli ! ambayo nayo inapamba mandhari ya michezo katika viunga vya chuo hili bila ya kusahau na kuyaweka kando mavazi ya michezo yanayomvutia mno mtazamaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news