NA FRESHA KINASA
WANANCHI ndani ya vijiji 68 vya Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara wamekuwa na mwamuko mkubwa kushirikiana na Serikali wakiwemo wadau wa maendeleo kutatua matatizo mbalimbali yanayowakabili vijijini mwao katika kuyafikia maendeleo.
Hayo yamebainishwa Aprili 30, 2023 kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo.
Baadhi ya matatizo hayo kwa upande wa elimu ya sekondari ni umbali mrefu unaotembewa na baadhi ya wanafunzi kwenda masomoni na mirundikano ya wanafunzi madarasani.
Kijiji cha Wanyere ni moja ya vijiji vinne vya Kata ya Suguti yenye sekondari moja tu ya kata, Suguti Sekondari. Ambapo, wananchi wa kijiji hicho cha Wanyere wameamua kujenga Sekondari kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda masomoni.
Taarifa imeeleza kwamba, wanafunzi wa Kijiji cha Wanyere wanalazimika kutembea umbali wa takribani kilomita 18 kwenda masomoni kwenye Sekondari yao ya Kata (kwenda na kurudi kilomita 36).
Aidha, juhudi hizo zinaungwa mkono kwa dhati na Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo kwa kuanza kuchangia ujenzi huo kwa kutoa saruji mifuko 100. Huku wananchi kutoka vitongoji sita vya Kijiji cha Wanyere nao wameanza ujenzi wa sekondari yao.
Wananchi hao wameanza kazi mbalimbali ikiwemo kusafisha eneo la ujenzi, kusomba mchanga tripu sita na kusomba mawe tripu saba. Aidha, taarifa hiyo, imebainisha kuwa michango ya ujenzi huo inapaswa kupelekwa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Wanyere au Akaunti ya Serikali ya kijiji.
"Michango ya ujenzi ipelekwe kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Wanyere simu +255 787 295 178. Pia Akaunti ya Serikali ya Kijiji Benki: NMB na: 30302301050 Tawi: Musoma, Jina: Serikali ya Kijiji cha Wanyere."
Aidha, Wananchi wa Kijiji cha Wanyere wameiomba Serikali na wadau mbalimbali kuunga mkono juhudi zao kusudi kuwezesha ujenzi wa sekondari hiyo ukamilike mapema hatua ambayo itaondoa tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda masomoni.
"Kwa wananchi wote walioko sehemu mbalimbali na wakazi wa Kijiji cha Wanyere na wadau wote ndani ya Jimbo la Musoma Vijijini na walioko sehemu mbalimbali watuunge mkono katika ujenzi huu. Umoja wetu utawezesha ujenzi kuisha haraka, tunamshukuru Prof. Muhongo, Mbunge wetu kwa juhudi zake kutuunga mkono na Serikali pia ambavyo imekuwa ikituletea maendeleo," amesema Judith Chibunu.
...Tangu tumeanza ujenzi huu wa Sekondari, Mwitikio ni mkubwa sana wananchi wanajitokeza kufanya kazi mbalimbali, hii yote ni katika kuhakikisha wanafunzi wanasoma karibu kusudi waweze kutimiza ndoto zao,"amesema Khanifa.
"Sekondari mpya zinazojengwa kwa sasa jimboni mwetu, na tumepanga zifunguliwe mwakani (Januari 2024) ni za vijiji vya Muhoji, Wanyere, Kisiwa cha Rukuba. Jimbo lina Kata 21, Sekondari za Kata 25, na za Binafsi mbili," imeeleza taarifa hiyo.