NA MWANDISHI WETU
MWAKILISHI Mkazi kutoka Shirika la UNICEF, Bi. Shalini Bahuguna ameagana na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu leo baada ya kumaliza muda wake nchini Tanzania.
Katika tukio hilo la kuagana, Waziri Ummy amesema, atamkumbuka Shalin katika utendaji wake wa kazi hasa kwa kuisaidia Sekta ya Afya katika utoaji wa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano.
Aidha, katika tukio hilo wamejadili mambo mbalimbali yanayohusu uboreshaji katika Sekta ya Afya ambapo Shirika la UNICEF litaendelea kushirikiana na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuendelea kuweka kipaumbele katika kuhakikisha watoto chini umri wa miaka mitano wanaendelea kupata chanjo pamoja na lishe kwa watoto wadogo.
Pia, wamezungumzia juu ya kuendelea kuimarisha usafi wa mazingira pamoja na kufanya upembuzi yakinifu kwa wanafunzi wenye udumavu.
Bi. Shalini alihudumu katika shirika la UNICEF kama Mwakilishi Mkazi kwa muda wa miaka Minne kuanzia mwaka 2019 hadi Mwaka 2023.
Katika kipindi chake cha miaka Minne Bi. Shalini ameweza kufanikisha katika uboreshaji wa huduma za chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano, utoaji wa lishe bora pamoja na kuimarisha mfumo wa huduma za dharula kwa kushirikiana na watoa huduma za afya katika ngazi ya jamii.