NA DIRAMAKINI
MTUMISHI wa Mungu wa Huduma ya Yerusalemu Pomerini Ministry iliyopo Kilolo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa, Nabii Dkt.Mjuni Kisha amesema, watumishi wa Mungu wana nafasi kubwa ya kuhakikisha wanashirikiana na Serikali wakiwemo wadau wengine wa maendeleo kusaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili jamii.
Dkt.Mjuni ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwahudumia kwa maombi na neno la Mungu wananchi huko vijijini pia amejiwekea utaratibu wa kushirikiana na mamlaka za Serikali za mitaa wakiwemo wananchi wengine kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali ikiwemo kuwezesha mahitaji muhimu kwa ajili ya wanajamii wenye uhitaji.
Amesema, hali hiyo imesababisha Mungu kuachilia baraka nyingi kwake na hata wale ambao wanafikiwa kwa nyakati tofauti.
"Hivyo,ukiona Mungu amekupa kitu,amekupa kwa ajili ya kizazi kijacho kujifunza,hubarikiwi kwa ajili ya leo unabarikiwa kwa ajili ya kizazi kijacho ambacho hakijazaliwa.
"Sasa watumishi wa Mungu tumepewa vitu vingi,tena vya thamani na Mungu anataka wengine kujifunza namna Mungu anavyotaka tuishi kwa kutazamwa ,kabla hujawaonyesha njia na jinsi ya watu wanavyotakiwa kuishi kwanza lazima watu wakuone wewe.
"Kwa hiyo haingii akilini kuona mimi kama Mtumshi wa Mungu nachukua bilioni moja sadaka za watu nanunua gari la kifahari au najenga nyumba ya milioni miamoja wakati kuna kijiji hakina hata zahanati moja.
"Kuna wazee vijijini hata blanketi la kujifunika hawana,nchi za ukanda zina vita, watu hawana chakula,muda mwingine kuna mahali sisi kama watumishi wa Mungu, mfano Mungu amenipa milioni miatano kwa nini nusu nisitoe hata kununua ambulance (gari la kubebea wagonjwa) moja ili kuipunguzia mzigo Serikali.
"Serikali ina majukumu mengi sana haiwezi kumfanyia mwananchi kila kitu,tuonyeshe uzalendo kwanza sisi watumishi wa Mungu,"amefafanua Nabii Mjuni.