Nabii Dkt.Mjuni:Serikali ni vizuri ikachunguza mapato yetu watumishi

NA DIRAMAKINI

MTUMISHI wa Mungu wa Huduma ya Yerusalemu Pomerini Ministry iliyopo Kilolo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini mkoani Iringa, Nabii Dkt.Mjuni Kisha amesema, licha ya watumishi wa Mungu kufanya kazi nzuri na muhimu katika Taifa na Bara la Afrika kwa ujumla kuna umuhimu wa baadhi yao Serikali kuwatazama kwa jicho la kipekee.

Nabii Dkt.Mjuni ambaye ameendelea kuwaunganisha maelfu ya Watanzania kupitia neno la Mungu na maombezi ya kufunguliwa katika vifungo mbalimbali vya kishetani amekuwa akiendesha huduma zake huko vijijini ambako watumishi wengi wa Mungu huwa hawapendi kwenda kuhudumu.

"Matukio mengi sana ya watumishi wa Mungu kwenye bara letu yanaathiri pande zote mbili kwa maana ya waamini na wasioamini,mbali na kutumia vitabu vya Mungu kututia moyo kuyakabili hayo matukio hatari pia Serikali ni vizuri kuchunguza mapato yetu kama watumishi.

"Tusije kuwa wengine tunatumia madawa ya kulevya (dawa za kulevya) na kupitisha vitu haramu kwa mgongo wa huduma za ki-Mungu,kwa kufanya hivyo Serikali inaweza kuwa chombo cha kutusafisha,kutukuza na kututia nguvu na hayo yanaleta afya iwapo watumishi tutatanguliza uzalendo kwenye nchi yetu,"amefafanua Nabii Dkt.Mjuni.

Wito huo unakuja ikiwa siku za karibuni baadhi ya watu ambao wanajiita watumishi wa Mungu kwa kutumia neno la Mungu wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha na matendo ya kidunia ambayo hayampendezi Mungu, wanadamu na mamlaka (Serikali) jambo ambalo limekuwa likitia doa katika huduma.

Aidha, wamekuwa wkaifanya hivyo, licha ya neno la Mungu kupitia Biblia Takatifu kutoa mwongozo mzuri hususani kumrudia Mungu ili waendelee kuishi maisha matakatifu.

Rejea Waefeso 4:17-32, Biblia inaeleza jinsi mwenendo wetu unavyotakiwa kuwa na kwamba tusiwe kama watu wa mataifa wanavyoenenda bali tubadili mwenendo wetu yaani utu wa zamani ili roho zetu zifanywe upya kwa kuuvaa utu upya unaopatikana katika haki na utakatifu.

Vivyo hivyo,1Petro 4:2-5, Biblia inatueleza kubadili mwenendo wetu tutoke katika tamaa za wanadamu ili tuweze kujua mapenzi ya Mungu kwani muda wetu iliobaki ni mchache.

Pia, tunaambiwa kuacha mienendo mibaya kama dhuluma, ubadhirifu, ulevi,biashara haramu, tamaa, karamu za ulafi, vileo na ibada za sanamu ambazo ni chukizo mbele za Mungu,wanadamu na mamlaka.

Rejea, 1Yohana 2:15-17, Biblia inaeleza kuhusu kumpenda Mungu, kwamba kama unataka kumpenda Mungu lazima tuachane na mambo ya dunia na kama tutaipenda dunia haiwezakani hata kidogo kumpendeza Mungu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news