Nabii No.7 amshukuru Mungu kwa Kingdom of God Church kupata usajili

NA DIRAMAKINI

KANISA la Kingdom of God (Kingdom of God Church-K.O.G) lililopo Kibaoni, Ngaramtoni njia ya Shule ya Msingi Mringa jijini Arusha limefanya ibada maalumu ya kumshukuru Mungu kwa kupata usajili kutoka serikalini.
Chini ya Mtumishi wa Mungu, Moses Mollel (Nabii No.7), K.O.G ambayo ni huduma ya Neno na Maombi inatajwa kuwa msaada kwa maelfu ya watu ndani na nje ya Jiji la Arusha ambao wamekuwa wakifunguliwa katika vifungo mbalimbali vya kishetani.

Kupitia, huduma hiyo, Nabii No.7 ambaye amekirimiwa kipawa cha kipekee na Mungu amepewa mamlaka na nguvu ya kuwafungua vipofu wakaona, viziwi wakasikia, viwete wakatembea na wagonjwa wanaponywa katika jina la Yesu Kristo. 

Tangu kuanzishwa kwa kanisa hilo Novemba 3, 2015 pia huduma ya maombi na neno la Mungu imekuwa ndiyo msingi mkuu, na Mungu amekuwa akiachilia miujiza, ishara na unabii wa papo kwa papo.
"Mimi, tangu siku ile wamenipa usajili niliwashukuru sana na nilimshukuru Mungu sana na ninaendelea kumshukuru na hata katika kanisa langu waumini wanaendelea kutokwa machozi ya furaha kwa hatua hii. Na wanaendelea kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababau wametuonesha thamani na heshima ya hali ya juu.

"Hatukutegemea sana na sisi kupata usajili mapema,tulikuwa tu tunajua kwamba tutapewa tu kwa sababu ni haki yetu kupata kama Watanzania,kwa sababu hatukuwa na siku maalumu ambayo tulikuwa tunafikiria tunapata leo au kesho, lakini tulikuwa tunajitahidi kufuata sheria na pia kanuni na maelezo ambayo tulikuwa tunapewa na Serikali na pia tulikuwa karibu na jamii inayotuzunguka na tunahudumia watu mbalimbali. 

"Kwa hiyo, pia tunawashukuru viongozi wote kwa namna ambavyo wamekuwa karibu na sisi na kutushauru pale ambapo tunahitajika kufanya kwa ajili ya kuiboresha huduma yetu, kwa hiyo kwa kweli ninawashukuru sana,
"Tumejenga ukaribu sana viongozi wa ngazi za chini kuanzia mitaa na maono yetu ni kuendelea kuisaidia jamii bila kubagua, kadri Mungu anavyotubariki ndivyo tutaendelea kugusa jamii yetu.

Pia, amesema kuwa, ataendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake ili Mungu awazidishie hekima na marifa kwa ajili ya kuliongoza taifa letu kwa ustawi bora.

Wakati huo huo, Nabii No.7 amesema,wataendelea kuhubiri neno la Mungu na watahakikisha huduma hiyo inaenea nchi nzima ili kuwahudumia kiroho na mahitaji ya msingi Watanzania.
"Kwa hiyo, ninamshukuru Mungu sana kwa kanisa letu kupata usajili kilichopo mbele yetu kwa sasa ni kupanua huduma zaidi kwa kufungua matawi, halikuwa jambo rahisi sana.Lakini, Mungu amefanya,"amesema Nabii No.7.

Aidha, kanisa hilo limesema linaungana na Serikali na Watanzania wote kupiga vita mapenzi ya jinsia moja, uhalifu katika jamii, kwani mambo hayo yanapaswa kukemewa kuanzia ngazi ya familia, jamii hadi Taifa.

Nabii No.7 katika ibada hiyo ya shukrani alisimikwa rasmi na viongozi waandamizi wa makanisa akiwemo mlezi wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania,Askofu Dkt.Dastan Haule Maboya.
Dkt.Maboya ambaye pia ni mwanzilishi wa Calvary Assemblies of God (C.A.G) katika ibada hiyo aliwapongeza K.O.G kwa kupata usajili kutoka serikalini huku akiwasisitiza kuendelea kulihubiri neno la Mungu, kushirikiana na Serikali na kuiunganisha jamii.

Pia, aliiomba Serikali kufanya uchunguzi wa baadhi ya makanisa ili kujiridhisha na mahubiri yanayotolewa na viongozi wa dini hizo kuepuka madhara na imani potofu kama ilivyotokea hivi karibuni katika nchi jirani ya Kenya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news