Prof.Muhongo aishauri Serikali kuwekeza katika uvuvi wa vizimba

NA FRESHA KINASA

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara, Prof.Sospeter Muhongo amesema kuwa, suluhisho la ukosefu wa samaki ndani ya maziwa makuu ni Serikali kuwekeza katika uvuvi wa vizimba (aquaculture) hatua ambayo itasaidia sekta ya uvuvi kutoa ajira kwa Watanzania, chakula cha kutosha na kuchangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi.

Prof. Muhongo ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma Mei 3, 202 wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kutoa ushauri huo ambapo pamoja na mambo mengi ameshauri utafiti ufanywe kwenye aina mbalimbali za samaki (species of fish) kwenye maziwa yetu makuu.

"Nitolee mfano Jimbo langu la Musoma Vijijini lenye kata 21, Vijiji 68, kata 18 ziko pembezoni mwa Ziwa Victoria na wananchi wanajishughulisha na uvuvi na katika hizi kata ni kata tatu tu. Hiki ni kithibitisho kwamba uvuvi lazima uchangie uchumi wetu kwa hali ya juu kabisa.

"Uvuvi tunaoufanya sisi watu wa Musoma na nadhani taifa zima kwanza unatoa chakuka, na kwa mambo ya kiuchumi uvuvi ni kwenye usalama wa chakuka (food security) ajira na unachangia uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa.

"Uchumi wa Tanzania kwa muda wa miaka mitatu hadi minne unakuwa kwa asilimia kati ya 5 na 6, waheshimiwa Wabunge kwenye hili Bunge la Bajeti kuna ushauri lazima tuutoe kwa serikali. Kusaidia uchumi wetu uweze kuondoa umaskini.

"Uchumi lazima ukue kwa asilimia 8 kwenda asimia 10 na ni sekta tano tu zinazoweza kufanya uchumi ukue haraka gesi asilia, madini, kilimo, inakuja mifugo na uvuvi na cha tano utalii. Hizi sekta tano kila moja ingechangia asilimia mbili ya ukuaji wa uchumi tungeweza kufikia hizo asilimia 8 hadi 10."

"Wataalam wa lishe wanasema kama unataka kupata lishe bora unapaswa kutumia gramu 280, kwa mara mbili kwa wiki yaani wiki ya kwanza gramu 140 na ya pili gramu 140.

"Tunaposema uvuvi ni muhimu tuangalie soko letu la kuuza, kwa Wananchi wote duniani wanataka kula kwa namna hiyo wako Bilioni 8, sasa hivi Tanzania ikiweza kuuza huko samaki hakika tutapata fedha nyingi ana. Kwa bara la Afrika sasa hivi tuko watu bilioni 1.43 tukiuza Afrika tutapata fedha nyingi sana.

"Lazima sekta ya uvuvi tuichukulie kibiashara, mwaka jana samaki waliozalishwa duniani walikuwa tani milioni 184.6, mzalishaji wa kwanza alikuwa China aliyezalisha tani milioni 67.5, na katika hizo tani, tani milioni 54.6, alizalisha kwa kutumia vizimba wa pili alikuwa India uzalishaji wake duniani asilimia 7.56, sasa maoteo ya mwaka huu ya biashara ya samaki duniani mapato yake yatafika Bilioni 612.

"Hapo ndipo tunapaswa kuishawishi na kuishauri Serikali iwekeze katika uvuvi wa vizimba, duniani wanaozalishwa ni tani milioni 180, mzalishaji namba moja ni China anatheluthi moja wa pili ni India anachuana na Egypt. Kwa Afrika anayeongoza ni Egypt kwa mwaka juzi alizalisha tani milioni 2.2, kati ya tani hizo, tani milioni 1.7 walizalishwa kupitia vizimba zaidi ya asilimia 77."

ASHAURI UVUVI WA VIZIMBA

"Hoja yangu hapa na ushauri wangu Mheshimiwa Spika, nitabaki kwenye uvuvi, wengi wamesema samaki wamekosekana Ziwa Nyasa, Tanganyika na Ziwa Victoria suluhisho lake ni uvuvi wa samaki wa vizimba."

"Tuiangalie Tanzania ilivyo ndugu zangu walikuwa wanalalamika niseme wanahaki ya kulalamika utafiti ambao ninamuomba Mheshimiwa Waziri Ulega na Maprofesa wake wafanye sio waliouripoti wakafikia hitimisho kwamba lazima zana zipatikane.

"Utafiti unaohitajika Mheshimiwa Waziri Ulega unachukua ziwa Tanganyika umri wake ni miaka milioni 10, maji ya ziwa Tanganyika ujazo wake ni cubic mita 18,880. Aina ya samaki waliopo ni zaidi ya 350 Sasa Wizara yetu tunataka wafanye utafiti hapa?.

"Ziwa Tanganyika mimi nikiwa Kigoma nimekaa Kipili nimekaa sehemu nyingi huko nafanya utafiti, lakini samaki ni aina mbili, tatu hizi 330 wengine wamepotea sisi bila kujua.

"Ziwa Nyasa umri wake ni miaka milioni 2, ujazo wake wa maji ziwa nyasa ni cubic kilometa 8,400, na lenyewe ndilo lina samaki wa aina nyingi kuliko lolote hapa duniani ni kati ya 800 na 1,000. ( spicies of Fish) sasa kwenye ripoti zetu hizi spicies 1000 kwenye ziwa Nyasa ziko wapi?.

"Tunakuja Ziwa Victoria, lenyewe ndilo changa kuliko yote umri wake ni miaka 400,000. Lakini ujazo wake wa maji ni cubic kilometa 2,423, aina ya samaki waliomo ni zaidi ya 500. "

PENDEKEZO LAKE KWA SERIKALI

"Kwenye haya maziwa makuu matatu yana maji ya kutosha, yana iana nyingi sana za samaki je, hawa samaki wote wako wapi? na wanavuliwa na nani?.

"Ziwa Victoria ukubwa wake Kenya wana asilimia 6, Uganda Wana asilimia 45, Tanzania asilimia 49, Kenya yenye asilimia 6 ina viwanda 48 vya samaki, Uganda yenye asilimia 45, ina viwanda 11 vya samaki, Tanzania ambao asilimia 49 na ripoti hapa Musoma hatuna hata kiwanda kimoja.

"Pendekezo langu tuwekeze kwenye uvuvi wa vizimba, tutoe kama hizi mikopo iliyokuja, nashukuru Waziri kaniambia wiki ijayo watu watapewa mikopo yao tuhamie kwenye uvuvi wa vizimba tutoe mikopo kwa wavuvi Watanzania waanzishe Viwanda kwa sababu samaki wa Vizimba watakuwa wengi, naunga mkono hoja,"amesema Prof. Muhongo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news