NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itapandisha pensheni kwa wastaafu kwa asilimia 100 akitolea mfano wa mstaafu wa kima cha chini anayepokea shilingi 90,000 atapanda mpaka shilingi 180,000. Mheshimiwa Rais ametekeleza ombi la wastaafu hao walilolitoa mwaka jana .
Ameyasema hayo leo Mei 1,2023 katika kilele cha Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika Viwanja vya Skuli ya Nungwi, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Rais Dkt. Mwinyi amesema, Serikali itapandisha pensheni jamii kwa asilimia mia moja na hamsini kwa wazee kuanzia miaka 70 ambapo kwa sasa wanaopata elfu ishirini watapanda hadi shilingi elfu hamsini.
Utekelezaji wa mabadiliko hayo utaanza mwezi Julai mwaka mpya wa bajeti utakapoanza.
Pia,Serikali imeshukuru kwa namna Wafanyakazi walivyopokea kwa furaha mabadiliko ya mishahara yaliyofanyika.
Vilevile, Rais Dkt.Mwinyi amesema,mipango na mikakati ya Serikali ni kuimarisha uwajibikaji kwa kuzingatia namna ya kuboresha mazingira ya kufanyia kazi yakiwemo mishahara bora na stahiki nyingine za watumishi.
Dkt. Mwinyi amesema serikali ipo hatua za mwisho za kuanzisha mfumo wa Bima ya afya kwa wafanyakazi wote umma Zanzibar.
Amesema, Serikali imepokea ombi la Wafanyakazi kupatiwa fedha za nauli kuwawezesha kwenda kazini na kurudi nyumbani nje ya mishahara yao.