NA DIRAMAKINI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema vyombo vya habari vinaweza kutoa mchango mkubwa endapo waandishi wa habari watazingatia uzalendo, weledi na maadili ya taaluma kinyume chake inaweza kufifisha jitihada za maendeleo, kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka waandishi wa habari watambue kuwa hakuna uhuru usio na mipaka, wala hakuna uhuru bila wajibu hivyo kwa kuadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari ni muhimu kutambua uzalendo wa nchi.
Ameyasema hayo leo katika siku ya mwisho ya Kongamano la Miaka 30 ya Uhuru wa vyombo vya Habari katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ametoa wito kwa waandishi wa habari watumie fursa ya siku hii kuweka mkazo katika uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu.
Vilevile, amewataka jumuiya na wadau mbalimbali wa vyombo vya habari watumie siku hii kusherehekea na kuungana na mashirika yanayotangaza masuala ya mazingira, haki za wanawake, haki za watoto, haki za asili, haki za kidijitali, vita dhidi ya ufisadi na mengineyo.