Rais Dkt.Nabiijoshua: Halmashauri Kuu ya Baraza la Mitume na Manabii Tanzania itakutana siku mbili

NA DIRAMAKINI

HALMASHAURI Kuu ya Baraza la Mitume na Manabii Tanzania inatarajiwa kukutana mjini Morogoro Juni 7 hadi 8, 2023 kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali yanayohusiana na umoja huo ambao unawaleta pamoja watumishi wa Mungu kutoka pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo Mei 29, 2023 na Rais wa Baraza la Mitume na Manabii Tanzania (BACCT),Dkt.Nabiijoshua Aram Mwantyala wakati akizungumzia kuhusu maamuzi yaliyofikiwa na Kamati Kuu kupitia kikao kilichofanyika hivi karibuni.

Rais Dkt.Nabiijoshua amesema,kupitia kikao hicho wajumbe kwa kauili moja walikubaliana kikao hicho kifanyike mjini Morogoro ambapo kitajadili mambo mbalimbali yahusuyo baraza ikiwemo viongozi kupewa vitambulisho rasmi.

Pia, kupitia kikao hicho Rais Dkt.Nabiijoshua amesema, viongozi watapewa fomu za wananchama kujiunga na baraza ikiwemo kukabidhiwa katiba ya baraza hilo.

"Ni kikao muhimu sana, kwani mbali na hayo pia viongozi wote watakabidhiwa kopi ya usajili na nyaraka nyingine za baraza kwa ajili ya utambulisho kwenye mamlaka za Serikali katika maeneo yao ikiwemo kuandaa ratiba na makadirio ya bajeti ya mkutano mkuu,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.

Amesema,pia kamati kuu kwa kauli moja iliamua ili kujenga taasisi yenye nguvu na inayoheshimika ni lazima viongozi wa ngazi zote ambao mienendo yao inaonesha hawana uuadilifu,nidhamu na sifa njema kuchukuliwa hatua.

""Kamati kuu kwa kauli moja iliamua kuwa ili kujenga taasisi yenye nguvu na inayoheshimika ni lazima viongozi wa ngazi zote ambao mienendo yao inaonesha hawana uadilifu, nidhamu na sifa njema kama watumishi wa Mungu ikiwa ni pamoja na makosa mengine ya kinidhamu waondolewe kwenye nafasi zao za uongozi kwa mujibu wa katiba ya baraza letu,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.

Wakati huo huo, Rais Dkt.Nabiijoshua amesema, pia kwa kuwa katiba ya baraza inataka makamu wa rais wa baraza wawe wawili ana wajibu wa kufanya uteuzi.

"Hivyo Rais wa baraza anawajibika kuteua makamu wa pili wa rais wa baraza, naibu katibu mkuu na nafasi zingine za uongozi zinazohitajika kama katiba inavyoeleza. Na kamati kuu kwa kauli moja tulikubaliana kuwa mkutano mkuu wa baraza utafanyika Oktoba 25 hadi 26, 2023 ambayo ni siku ya Jumatano na Alhamisi jijini Dodoma,"amefafanua Rais Dkt.Nabiijoshua.

Rais Dkt.Nabiijoshua ameendelea kufafanua kuwa, "Kamati kuu inawapongeza na kuwashukuru viongozi na wana Baraza la Mitume na Manabii Tanzania wote kwa mshikamano mliioonesha tangu tumalize mkutano wa mashangilio. Mungu awabariki sana,tunawatakia mafanikio mema kwa yote yaliyopo mbele yenu katika kumtumikia Mungu wetu ndani ya Kristo Yesu Bwana wetu,"amefafanua.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

  1. Mungu AWABARIKI WOTE PENDANENI KAMA YESU KRISTO ALIVYOWAPENDA NINYI Amen DR.PROPHET DANIEL MWEBRANIA

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news