Rais Dkt.Samia awapa tano Yanga SC

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ameipongeza Klabu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam kwa kutinga Nusu Fainali katika Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ametoa pongezi hizo baada ya Aprili 30, 2023 katika Dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kuandika rekodi hiyo mbele ya Rivers United kutoka nchini Nigeria.

"Pongezi kwa Klabu ya Yanga kwa kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho (CAF Confederation Cup), na kila la kheri katika maandalizi mliyoanza sasa kwa mchezo ujao. 

"Mmeandika historia jalili. Mmetuheshimisha sana. Hamasa yangu inaendelea, na sasa imeongezeka. Kaifanyeni kazi,"ameeleza Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kupitia mitandao yake rasmi ya kijamii.
Awali, Yanga ya jijini Dar es Salaam katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam walitinga hatua hiyo baada ya kuambulia suluhu mbele ya wapinzani wao Rivers United kutoka nchini Nigeria.

Mtanage huo ambao ulikuwa wa kuvutia, kila pande ilionekana kutamani kuvuka hatua moja kwenda nyingine, lakini dakika 90 zilitamatika kwa pande zote ubao ukisoma 0-0.

Klabu ya Yanga wamefuzu kwenda Nusu Fainali kwa faida ya ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa kwanza wakiwa ugenini huko Nigeria, kupitia mabao ya mshambuliaji Mkongo, Fiston Kalala Mayele.
Yanga SC sasa itamenyana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambayo imeitoa Pyramids ya Misri kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Cairo na kushinda 1-0 dhidi ya Phokeng, NW.

Mechi ya kwanza Yanga na Marumo Gallants itafanyika jijini Dar es Salaam Mei 10, mwaka huu na marudiano yatafuatia Afrika Kusini Mei 17, mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news