NA MWANDISHI WETU
MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Mhe. Thobias Andengenye ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kwa jitihada inazozifanya za kuwezesha wananchi kurasimisha biashara zao na namna inavyotoa huduma katika Maonesho ya sita (6) ya Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uwezeshajii Wananchi Kiuchumi (NEEC) Prof. Aurelia Kamuzora, akisaini katika kitabu cha wageni alipotembelea banda la Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), leo tarehe 27 Mei, 2023, kwenye Maonesho ya Sita (6) yaliyoandaliwa na Baraza hilo katika uwanja wa Mwanga, mjini Kigoma.
Pongezi hizo amezitoa leo Mei 27, 2023 alipotembelea banda la BRELA kabla ya kufunga maonesho hayo ambayo yamefanyika katika uwanja wa Mwanga, Mjini Kigoma.
Afisa Usajili wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Stanslaus Kigosi (kulia), akielezea kuhusu huduma zinazotolewa na BRELA, kwa Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye (kushoto), alipotembelea banda hilo katika Maonesho ya (6), yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), katika uwanja wa Mwanga, mjini Kigoma. Maonesho hayo ya siku saba yamehitimishwa leo tarehe 27 Mei, 2023.
Mhe. Andengenye amesema ameridhishwa na namna BRELA inavyotekeleza majukumu yake, wakati akipatiwa maelezo na Afisa Usajili wa BRELA Bw. Stanslaus Kigosi, juu ya ushiriki wa BRELA katika maonesho hayo.
Akitoa maelezo hayo kwa Mkuu wa mkoa, Bw. Kigosi, ameeleza kuwa katika maonesho hayo mbali na kutoa elimu pia wamekua wakitoa usaidizi kwa wadau mbalimbali kwenye Mfumo wa Usajili kwa njia ya Mtandao, pamoja na kutoa huduma za usajii za papo kwa papo.
“Huduma zote za BRELA zinazotolewa kwa njia ya mtandao, hivyo baadhi ya wananchi wamekuwa wakipata changamoto katika kupata huduma hizo, uwepo wetu hapa ni kuwawezesha kupata huduma hizo zikiwemo Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Makampuni na Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi "A" papo kwa papo,”amesema Bw. Kigosi.
Maafisa wa Wakala wa Usajili Biashara na Leseni (BRELA), waliovaa fulana zenye nembo ya Wakala, wakikabidhi vyeti vya Usajili wa Majina ya Biashara kwa wadau waliokamilisha taratibu za usajili katika banda la BRELA, kwenye Maonesho yaliyoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC). Maonesho hayo yamefungwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye katika uwanja wa Mwanga, mjini Kigoma.
Aidha Bw. Kigosi amezitaja huduma zingine zinazotolewa na BRELA kuwa ni pamoja na Usajili wa Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Viwanda na huduma baada ya usajili.
Katika maonesho hayo pia maafisa wa BRELA wamepata fursa ya kutembelea mabanda ya washiriki wengine na kuwahamasisha kurasimisha biashara zao.Maonesho hayo ya siku saba yalianza tarehe 21, Mei, 2023 na yamehitimishwa leo tarehe 27 Mei, 2023.