NA DIRAMAKINI
SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imewataka wananchi kuendelea kupokea vema miundombinu ya nishati vijijini ambayo imewekeza fedha nyingi ili kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma hiyo.
Wito huo umetolewa na Mhandisi Ernest Makele ambaye ni Mhandisi wa Miradi ya REA katika Mkoa wa Mwanza na Mara wakati akitoa ufafanuzi kwa kina kuhusu miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa Mkoa wa Mwanza.
"Miradi yetu tunapoitekeleza, sio fedha kutoka mahali kwingine popote ni Serikali imejitoa na imeahirisha matumizi mengine yoyote yale ya msingi, kumbuka Serikali ina mambo mengi ya kufanya.
"Rais wetu mpendwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amejitoa kwa upendo kabisa kuhakikisha kwamba usambazaji wa uneme vijiji unafanyika kwa wananchi tena kwa gharama nafuu kabisa yaani shilingi elfu 27,000. Ni muhimu kutambua Serikali imegharamia gharama zote.
"Serikali imezitoa hizi fedha kwa ajili ya mradi huu, inakatisha tamaa wakati mwingine miundombinu inapofanyika kwenye kijiji watu hawaipokei 'positively' tunatamani kadri Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anavyotoa hizi fedha za miradi hii wananchi waipokee kwa upendo na kuunganisha haraka iwezekanavyo,"amefafanua Mhandisi Makele.
Amesema, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliundwa ili kuhakikisha wananchi vijijini wanafikishiwa nishati ya umeme kwa gharama nafuu.
"REA ni Wakala wa Nishati Vijiji anayepeleka nishati vijijini ili kuwafikishia wananchi kwa gharama nafuu, zoezi hili lilianza mwaka 2007 mara tu REA ilivyoundwa mpaka sasa kwa Mkoa wa Mwanza wenye vijiji 544, vijiji vyote vimefikiwa.
"Sasa hivi tunakamilisha mradi wa REA 'three round two' ambayo inakwenda katika vijiji 174, kwa gharama ya shilingi bilioni 42.6.
"Mradi huu ni mkubwa na unagharimu fedha nyingi na mkandarasi anayetekeleza mradi huu ni Sengerema Engineering Group Limited vijiji 113 vimeshawashwa na vijiji vingine 20 viko hatua ya mwisho kwa sababu transforma zimeshakuwa installed.
"Lengo ni kuunga wateja 3,860, mpaka sasa wateja waliounganishwa ni 1,308, ukilinganisha na kazi iliyofanyika. wateja ni wachache sana, kwa hiyo REA na wadau wengine tuko katika ziara ya kuhamasisha uunganishaji wa wateja zoezi hili lilianza tarehe 24 kwa kuzifikia wilaya mbalimbali za Mkoa wa Mwanza.
."Tulianza na Wilaya ya Magu, Kwimba na sasa Sengerema na zoezi limeonesha matokeo chanya kwa sababu wananchi wamekuwa wakionesha mwitikio mkubwa. Wapo ambao wameuza kuku na hazina zao. Na leo tumekuwa eneo la wavuvi wameuza samaki ili iwe kama kianzio na wamesema wanafanya wiring.
"Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni wananchi kutofanya wiring kwa wakati, mradi umeanza Julai 2021 ndipo mkandarasi aliingia saiti, lakini mpaka sasa wananchi wanasema wanajipanga kitu ambacho sio kweli. Wamekuwa na miaka zaidi ya miwili.
"Nitumie nafasi hii kutoa wito wananchi, wanapoona miradi yetu ya REA inaingia kwenye maeneo yao mara moja tu wafanye wiring. Hii itasaidia kuharakisha kuunganishiwa kwenye nyumba zao.
"Lakini niseme tu kwamba, baada ya zoezi la uhamasishaji mwitikio umekuwa mkubwa sana tunayo timu ya mkandarasi inapita kuunganisha kwa Wilaya ya Magu,wateja waliounganishiwa baada ya zoezi hili ni asilimia 138 ya wateja waliokuwepo kabla.
"Zoezi hili linaendelea pia kwa Wilaya ya Kwimba, na sasa Wilaya ya Sngerema, niwaombe wananchi watumie muda huu kabla mradi haujafungwa ili waunganishiwe. REA iko tayari kushirikiana na TANESCO na wadau wengine.
"Gharama ni nafuu yaani elfu 27,000 tu, hii ni gharama ya kuingiza umeme katika nyumba zetu. Maombi yote yanayohitajika katika majumba yetu, wananchi wanahitajiwa kuwa na namba ya NIDA, ni hitaji ambalo ni mubimu.
"Sasa tulikopita, kuna changamoto Serikali kupitia NIDA iko kila wilaya na sasa hivi hakuna scramble ukienda wilayani utapata NIDA na kutumia katika shughuli zako mbalimbali ikiwemo katika zoezi hili. Lakini kuna wananchi wengine hawana NIDA wanataka kutumia za wengine, jambo ambalo halishauriwi kwa hiyo hilo ni moja.
"Jambo jingine ambalo ni changamoto ni pale wananchi wanatumia wakandarasi wasiofahamika. Wakandarasi wote wanaofanya majumbani wiring, wamepitishwa na EWURA ndio wana mamlaka ya kupitisha wakandarasi hao wa majumbani.
"TANESCO mradi wetu unapoanza, huwatambulisha hawa wakandarasi kwa hiyo viongozi wa vijiji wanawafahamu,wengi wametapeliwa na unapotapeliwa unarudishwa nyuma kufanya zoezi hili la uunganishaji kwa hiyo wananchi wawe makini kuepuka kutapeliwa.
"Kingine ni kwamba, utaratibu wa wiring sio jukumu la REA ni mwananchi mwenyewe anahitaji kulinda mali yake na haki yake,"amefafanua kw akina Mhandisi Makele.