SALAMU ZA JUMAPILI:Una nini mkononi?

NA LWAGA MWAMBANDE 

UKISOMA neno la Mungu, utaona awali mtumishi wa Mungu, Musa hakufahamu kabisa kwamba watu kumuamini na kumsikiliza kunategemea na alicho nacho. 

Watu kuamini kwamba ana Mungu kulikua kunategemea na matumizi ya kile alicho nacho. 

Rejea,Biblia Takatifu kitabu cha Kutoka 4:1-3 kinasema, "Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, Bwana hakukutokea...

Bwana akamwambia, Ni nini hiyo uliyo nayo mkononi mwako? Akasema, Ni fimbo. Akamwambia, Itupe chini; akaitupa chini, nayo ikawa nyoka; Musa akakimbia mbele yake." 

Pamoja na kuwa na fimbo mkononi mwake lakini Musa hakujua thamani ya ile fimbo. 

Thamani ya fimbo aliyokua nayo Musa ilikua imejificha kwa Mungu. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema,m wenye kuitambulisha thamani ya ulicho nacho ni Mungu peke yake. Endelea

1. Una nini mkononi, sema kama una kitu,
Hicho kitu cha thamani, chaweza kufanya mtu,
Kwani Mungu wa mbinguni, baraka zaka kwa kitu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

2. Kawaida wanadamu, hujiona siyo kitu,
Mbele kukiwa kugumu, aingia kwa msitu,
Neno hili ufahamu, una nini wewe mtu?
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

3. Kitu kilimpa kazi, Musa kwenda fanya vitu,
Wala hakuwa mdwanzi, kutembea bila kitu,
Akapata uongozi, wa kuwaongoza watu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

4. Kutokea kwa Farao, fimbo ilimpa utu,
Nyoka wa wachawi hao, walitaka leta kitu,
Musa kawapiga bao, wakatoka bila kitu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

5. Kwa Neno tunafahamu, muhimu kuwa na kitu,
Hata Mungu akizumu, aone washika kitu,
Huo ni utaalamu, utaheshimika mtu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

6. Elisha alipopita, akalialia mtu,
Mwanamke atateta, wanavyomdai watu,
Watoto aliopata, wachukuliwe na watu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

7. Kuulizwa ana nini, akasema hana kitu,
Ila mafuta nyumbani, ndiyo yamebakia tu,
Baraka toka mbinguni, zikafanya awe mtu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

8. Sasa wewe una nini, kile cha thamani kitu,
Hebu kagua moyoni, na mwilini una kitu?
Ni chema madhabahuni, au ni cha kihuni tu?
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

9. Pengine kipawa chako, ndiyo hicho chako kitu,
Kwa hiyo talanta yako, maisha yasiwe butu,
Inuka anza kivyako, mafanikio yapo tu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

10. Ni katika kila kazi, ambayo afanya mtu,
Faida ni waziwazi, ambazo wachota watu,
Hata zile duni kazi, wanafaidika watu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

11. Una nini mkononi, usikae bila kitu,
Maarifa ya nyumbani, hata kwingine kwa watu,
Chota yawe maishani, mbele yatakutoa tu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

12. Shika kitu mkononi, huo hasa ndiyo utu,
Upite barabarani, kule kuliko na watu,
Uwe nacho kibindoni, mbele kitakufaa tu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

13. Una akili timamu, jitambue una kitu,
Kujua uwe na hamu, acha kujikalia tu,
Uchukue yako zamu, miongoni mwao watu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

14. Mungu akikuuliza, wewe una nini kitu,
Kujibu uwe waweza, kwako atafanya kitu,
Usijekujilegeza, kwamba kitu siyo kitu,
Musa ile fimbo yake, ilimpa ujasiri.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news