NA RAHMA KHAMIS
MAELEZO
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita amewataka wanahabari kufuatilia habari kwa uhakika ili wananchi waweze kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Hassan Khatib Hassan akizungumza machache wakati alipokuwa akimkaribisha mgeni rasmi kuzindua kongamano la wadau wa Habari lililofanyika Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani. (Picha na Yussuf Simai).
Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege wakati alipokuwa akifungua kongamano la siku mbili la kuadhimisha miaka 30 ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.
Amesema, habari ni kitu muhimu hivvyo wanahabari wana jukumu la kutoa taarifa sahihi kwa jamii na kujitahidi kufanya kazi zao kwa weledi zaidi ili kutekeleza fani hiyo kwa ufanisi.
Waziri Tabia ameeleza kuwa, lengo la maadhimisho hayo ni kulinda na kuangalia hali ya uhuru wa vyombo vya habari duniani pia Serikali inapata nafasi ya kukutana na na washiriki wake wa maendeleo na asasi za kiraia katika kukuza fani hiyo.
"Serikali ya Mapinduzi kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaahidi kuendelea kushirikiana na UNESCO ambayo ndio mfadhili kiongozi katika maadhimisho ya siku ya Uhuru wa vyombo vya habari duniani,"amesema Waziri huyo.
Waziri Tabia amesema kuwa, siku ya uhuru wa vyombo vya habari inatoa fursa kwa watu duniani kote hasa wanahabari kuonesha mshikamano wao kwa kutoa wito wa kuondoa vizuizi vya kupata habari.
Ameeleza kuwa, pia wanahabari wanaweza kudai uwajibikaji kutoka kwa viongozi na taasisi kwa kuwakumbusha watu kuhusu umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika kukuza maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
"Dunia hivi sasa inakabiliwa na uchafuzi wa mazingira ambayo chanzo chake ni wanadamu hivyo ni dhamira ya wazi kuwa maadhimisho hayo yameshirikiana kuhusu kukabiliana na tatizo hilo,"amesema.
Waziri huyo ameongeza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza miradi mingi ikiwemo habari ni vyema wanahabari waweze kutoa taarifa hizo kwa usahihi na kuwafikia wananchi kwa wakati.
Waziri amewasisitiza wanahabari kufuatilia changamoto za wananchi pamoja na kutoa taarifa za maendeleo ya nchi ili waweze kufahamu hatua na yanayoendelea nchini.
Waziri wa Habari,Vijana Utamaduni na Michezo, Mhe. Tabia Maulid Mwita akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa uchechemuzi LHRC Maduhu William wakati alipokua akitembelea maonyesho ya vitabu yaliokuwa nje ya Ukumbi wa Golden Tulip wakati alipofika kuzindua kongamano la wadau wa habari kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani huko Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema kuwa, maadhimisho ya siku hiyo yatatumika kama jukwaa muhimu katika kuibua changamoto za kisera pamoja na kuangalia uboreshaji wa mazingira ya uendeshaji wa vyombo vya habari nchini.
Waziri Tabia amewatoa wasiwasi wanahabari hao kuhusu kubadilishwa kwa sheria ya habari kwani Serikali inaendelea na mchakato huo na karibuni sheria hiyo itapelekwa katika vyombo vya kutunga sheria kwa hatua.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Hassan Khatib Khasan kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Mhe.Fatma Hamad Rajab akimkaribisha Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Mhe.Tabia Maulid Mwita amewashukuru wale wote walioshiriki kufanikisha shughuli hiyo.
Nao washiriki wa kongamano hilo wamesisitiza wanahabari wenzao kujifunza kitaaluma ili kukuza fani hiyo na kufanya kazi kwa weledi na ufanisi.
Maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari hufanyika kila ifikapo Mei 3, kila mwaka ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni KUUNDA MUSTAKABALI WA UHURU WA KUJIELEZA KAMA KICHOCHEO CHA HAKI ZA BINADAMU.