Serikali yafanya maboresho vitambulisho vya Machinga

NA GODFREY NNKO

SERIKALI kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Taasisi ya kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC), Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA),wizara za kisekta pamoja na wadau imekamilisha maboresho ya Mfumo Jumuishi wa Kidijitali wa Usajili na Utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara ndogondogo nchini.

Mfumo huo upo kwenye hatua ya kufanyiwa majaribio na utaanza kutumika rasmi mwaka wa fedha 2023/24 katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Morogoro.

"Wizara imeendelea kuratibu na kusimamia mipango na programu mbalimbali za kuwezesha na kuendeleza kiuchumi makundi maalum.

"Makundi yanayolengwa ni wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo machinga, mama na baba lishe, waendesha bodaboda na bajaji ambao hupata changamoto kuzifikia fursa zilizopo kujikwamua na kukua kiuchumi kutoka kwenye taasisi za fedha kwa kuwa hawatambuliwi rasmi na pia hawana dhamana za kuwawezesha kukopesheka kwenye taasisi hizo;

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Dkt.Dorothy Gwajima (Mb) ameyasema hayo leo Mei 18, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24.

"Zoezi litaendelea katika mikoa mingine iliyobaki na litakuwa ni zoezi endelevu. Aidha, katika kipindi hiki cha mpito kabla ya mfumo huo kuanza kutumika, mfumo wa utoaji vitambulisho vya Machinga kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) utaendelea kutumika,"amefafanua Waziri Dkt.Gwajima.

Wakati huo huo, Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima amelieleza Bunge kuwa,jumla ya shilingi milioni 260 (milioni 10 kwa kila mkoa) zilizoahidiwa Mei 17, 2022 na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan zimetolewa mwezi Oktoba 2022 ili kuwezesha ujenzi wa Ofisi za Machinga ngazi ya mkoa nchi nzima.

Vilevile, amesema mikoa imetoa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi hizo na ujenzi upo katika hatua tofauti ambapo baadhi ya mikoa ujenzi upo kwenye ngazi ya msingi na wengine kwenye uinuaji kuta.

Aidha, kwa mikoa ambayo ujenzi haujaanza, "natoa rai ujenzi uanze ili kuwezesha wafanyabiashara Ndogondogo kupata ofisi za kudumu kwenye mikoa hiyo.

"Hivyo, nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutekeleza ahadi yake ambayo itasaidia upatikanaji wa Ofisi za Wafanyabiashara Ndogondogo katika mikoa yote nchini.

"Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kuwapongeza wakuu wa mikoa kwa kuendelea kushirikiana na wafanyabiashara ndogondogo ikiwemo kupitia Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Taifa katika kuimarisha, kuendeleza na kuwezesha kukua kwa shughuli zao za kiuchumi ili wawaze kuchangia Pato la Taifa.

"Mfano, kwa Mkoa wa Dar es Salaam ushirikishwaji huo umewezesha viongozi 15 wa wafanyabiashara ndogondogo (Machinga) kunufaika na ziara ya mafunzo nchini Rwanda,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima.

Pia, amesema Serikali kupitia halmashauri inaendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kutenga na kuendeleza maeneo rafiki kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo kufanya biashara, ambapo hadi sasa jumla ya masoko 367 yameboreshwa nchini yenye uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara ndogondogo 136,041.

Baadhi ya masoko hayo ni pamoja na Soko la Machinga Complex Bahi Road jijini Dodoma, Soko la Kigogo Fresh na Soko la Bunju B jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema ujenzi wa masoko hayo unaendelea katika Jiji la Tanga, Mbeya, Mwanza, Manispaa ya Morogoro pamoja na Halmashauri ya Mji wa Tunduma.

"Hivyo, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa fedha zinazowezesha ujenzi na uboreshaji wa masoko haya nchini.

"Wizara imetengewa jumla ya shilingi Bilioni 22,925,892,250 kwa ajili ya kutoa mkopo wenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo nchini mwaka 2022/23.

"Hata hivyo, kufuatia maelekezo ya Serikali kuwa fedha zitolewe kupitia mfumo wa kibenki, wizara inakamilisha taratibu zote muhimu zitakazowezesha fedha hizo kuanza kutolewa kupitia mfumo wa kibenki ambao ni salama na rafiki kwa walengwa.

"Mheshimiwa Spika,wizara imeendelea kushirikiana na wafanyabiashara ndogondogo ikiwemo viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) nchini kuhamasisha wafanyabiashara ndogondogo kushiriki katika shughuli mbalimbali za Kitaifa ikiwemo maonesho ya kibiashara,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Dkt.Gwajima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news