Serikali yasisitiza umuhimu wa chanjo katika kuokoa maisha ya watoto,jamii

NA GODFREY NNKO

WIZARA ya Afya kupitia Mpango wa Chanjo wa Taifa imesema kuwa,chanjo ni mkakati mwafaka katika kutokomeza magonjwa na kupunguza vifo vya watoto walio katika familia zetu ikiwemo kupunguza gharama ambazo zingetumika kutibu maradhi hayo ambayo yanaweza kuzuilika.

Hayo yamebainishwa Mei 9, 2023 katika semina ya siku moja kwa wanahabari kutoka vyombo mbalimbali iliyofanyika katika Ukumbi wa Anatoglu-Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.

Lengo kuu la semina hiyo lilikuwa ni kujengewa uelewa ili wanahabari waweze kushiriki kikamilifu kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa chanjo katika kuokoa maisha ya watoto wote na jamii kwa ujumla.

Mgeni rasmi katika semina hiyo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mheshimiwa Omary Kumbilamoto amesema, vyombo vya habari ni daraja muhimu la kuwaunganisha wananchi, hivyo mafunzo hayo kwa wanahabari hao yamekuja kwa wakati mwafaka ikizingatiwa Serikali inaendelea kutoa chanjo mbalimbali nchini.

"Kwa hiyo, mna mchango mkubwa wa kuhakikisha mnapeleka taarifa umuhimu za kuelimisha na kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa jamii katika kujikinga na magonjwa yenye kuzuilika na chanjo ili kuepusha vifo.

"Aidha, kuhimiza familia kuwapeleka watoto wote wanaostahili kwenda kupata chanjo katika vituo vyote vya afya, hospitali na vituo vya watu binafsi ili wapate kuchanjwa.

"Chanjo ni mkakati mwafaka katika kutokomeza magonjwa na kupunguza vifo vya watoto walio katika familia zetu na kupunguza gharama ambazo zingetumika kutibu maradhi haya ambayo yanaweza kuzuilika,"amefafanua Mheshimiwa Kumbilamoto.

Zingatia

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya hapa nchini zinatolewa chanjo 10 ambazo zinatibu magonjwa 14. Aidha, chanjo huokoa maisha ya watoto wengi na huwakinga dhidi ya maradhi, ulemavu na vifo vitokanavyo na magonjwa yanayozuilika kwa chanjo ikiwa ni pamoja na surua, homa ya ini (hepatitisi B), dondakoo, kifaduro, nimonia, polio, kuhara kunakosababishwa na virusi vya rota, rubela na pepopunda.

Aidha, kisayansi chanjo ni kitendo cha kupewa kinga mwili kwa njia ya kuamsha vitoa kinga viwe tayari kupambana na adui ambaye wanamjua tayari.

Watoto waliopata chanjo huwa wamekingwa dhidi ya magonjwa hatari, ambayo kwa kawaida huweza kusababisha ulemavu au kifo.

Watoto wote wana haki ya kupata kinga hii, kwani kinga ya utotoni ni muhimu sana hasa kwa ukuaji wa baadae. Hivyo basi, chanjo kwa mtoto katika mwaka wake wa kwanza na katika mwaka wa pili ni muhimu zaidi.

Vile vile inashauriwa kuwa ni muhimu pia, kina mama wajawazito kupata chanjo ya pepopunda ili kujikinga wao wenyewe na watoto wao wanaozaliwa.

Wazazi na walezi wengine wanapaswa kufahamu sababu za umuhimu wa chanjo, ratiba ya chanjo inayotumika na mahali chanjo inakotolewa kwa watoto popote walipo nchini.

Kumbilamoto tena

"Chanjo zinazotolewa na Mpango wa Taifa wa Chanjo ikiwemo dhidi ya kifua kikuu,donda koo,polio,rubela, pepo punda, kifaduro, homa ya ini, saratani ya mlango wa kizazi, homa ya uti wa mgongo, kuhara, surua,UVIKO-19 na nyinginezo ni muhimu sana.

"Kwani, chanjo huwezesha kuzuia takribani vifo milioni mbili hadi tatu kila mwaka kutokana na maradhi yanayozuilika kwa chanjo duniani.

"Wengi tulishuhudia wodi nyingi zilitengwa na kujaa watoto waliougua surua, pepopunda.Aidha, watoto wengi walibakia na upofu, ulemavu wa kutosikia na utahira kutokana na athari ya ugonjwa wa polio na surua.

"Aidha, husababisha upungufu wa kinga mwilini na kuwaweka watoto katika uhalisi wa kuugua magonjwa mengi ya watoto ikiwemo nimonia, utapiamlo na kusababisha wengi wao kupoteza maisha,"amefafanua Mheshimiwa Kumbilamoto.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa,hapa nchini mafanikio ya chanjo ni makubwa, "kwa mfano, tumeshuhudia wodi za surua zimefungwa katika hospitali zetu miaka ya nyuma, ingawa mwaka jana tulipata mlipuko wa ugonjwa huu na hadi sasa tunamshukuru Mungu mlipuko huo umepungua kwa kiasi kikubwa.

"Tumefanikiwa kutokomeza ugonjwa wa ndui na kudhibiti ugonjwa wa donda koo, polio na pepo punda, mafanikio hayo makubwa yametokana na juhudi za Serikali katika kuwakinga wananchi wake dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika."

Pia,amebainisha kuwa, Serikali kwa kushirikiana na Muungano wa Chanjo Duniani (GAVI) wakiwemo wadau mbalimbali wa maendeleo imehakikisha chanjo inafika katika halmashauri zote hapa nchini.

"Napenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na shirika letu pendwa la GAVI (Muungano wa Chanjo Duniani (GAVI) na wadau wengine wa maendeleo tumefanikiwa kuhakikisha upatikanaji wa chanjo katika halmashauri zote na vituo vyote vya kutolea huduma za serikali na watu binafsi kwa mama na mtoto.

"Chanjo hizo ni ghali kama mwananchi angetakiwa kununua mwenyewe ni shilingi 3,000 na dozi ni takribani shilingi 20,000 au zaidi ya hapo. Kwa mwananchi wa kawaida fedha hizi ni ghali sana.

"Hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha huduma ya chanjo zinazosogezwa karibu na wananchi kwa kununua majokofu ya kutosha na mkakato huu ni endelevu.

"Tunayo changamoto ya mabinti wa miaka 14 ambao hawakukamilisha au kupata chanjo ya kuzuia saratani, mlango wa kizazi mabinti ambao hawajapata au kukamilisha chanjo huwa wako kwenye hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya kuhatarisha afya zao.

"Vile vile kutokana na janga la UVIKO-19 lililotokea mwaka 2019 tumekuwa na watoto wengi ambao ni zero dozi yaani hawajapata kabisa hata chanjo moja na kupelekea nchi yetu kuwa na mlipuko mkubwa wa surua.

"Hivyo tunawahamasisha walengwa,wazazi walezi wa familia kwenda kuwapeleka walengwa kwenye vituo vya kutolea huduma kupata chanjo kama ilivyokuwa kwenye ratiba.

"Kwa mara nyingine, nitumie fursa hii kuwahimiza wazazi na walezi wa familia kuwapeleka watoto hospitali kupata chanjo kituoni ili wapate chanjo stahiki na ratiba iliyopangwa. Kila mmoja anawajibu wa kuhakikisha watoto wake au wa jirani wanapata haki ya kupata chanjo."

Pongezi

Mbali na hayo, Mheshimiwa Kumbilamoto amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha ili kujenga vituo vya afya ndani na nje ya Jiji la Dar es Salaam.

"Nichukue fursa hi kumpongeza Rais wetu mpendwa mama yetu Samia Suluhu Hassan, hivi navyozungumza na ninyi tumepokea takribani shilingi milioni 800, pesa hizo zimeletwa jana kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Kata ya Mzinga, lengo ni kusogeza huduma za afya kwa wananchi kule chini.

"Vile vile tumepokea fedha takribani shilingi bilioni 13, tunajenga vituo vya afya visivyopungua vinane yote ni kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma ya afya kwa ubora na kuwafikia sehemu waliko wananchi.

"Niwaombe waandishi wa habari muwe mabalozi wa kuweza kututangazia huduma hizi anazozitoa Rais Dkt.Samia na kuhamasisha chanjo hizo zinavyotoka ni kwamba mtoto asipopata chanjo anakumbwa na magonjwa ya mlipuko vile vile ana uwezo wa kupoteza maisha."

Kaimu Mganga

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dkt.Milka Masania amesema, lengo la kuwakutanisha pamoja waandishi hao wa habari ni ili, "Tumekuja kuwapa elimu kuhusu chanjo, tunafanya nini tuweze kupambana na magonjwa yanayoweza kuzuilika kwa njia ya chanjo.

"Lengo kubwa ilikuwa ni kuja kuwapa elimu kwa sababu ninyi waandishi wa habari ni wadau wakubwa katika kutoa elimu kwa hiyo mtaitoa kwa jamii.

"Tunasikiliza vyombo vya habari, kusoma magazeti kwa hiyo ninyi ni muhimu sana kutoa elimu. Tumeona ni muhimu muje hapa kupata elimu ambayo ni sahihi na mtakapokwenda kwenye kuhabarisha umma mtoe taarifa sahihi na takwimu sahihi.

"Tumesikia hapa changamoto ya chanjo, umuhimu wake kwa hiyo mkawe wajumbe kutoa elimu kwa jamii. Tumeona kuna watoto hawapati chanjo wengine hawamalizi chanjo. Tumeona magonjwa 14 yanazuilika kwa chanjo, kwa hiyo mtoe taarifa wananchi wajitokeze chanjo zipo na zinatolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma.

"Wasiwe na mila potofu zinazopelekea wasipeleke watoto wao kwenda kuchanja, tuwahimize na kuwapa elimu kupambana na haya magonjwa yanayozuilika kwa njia ya chanjo,"amefafanua Dkt.Masania.
 
Naye Afisa Mpango wa Chanjo Taifa kutoka Wizara ya Afya, Bi. Rotalis Gadau amesema, kuanzia mwaka 2019 mpaka 2020 kiwango cha huduma za chanjo kiliongezeka kwa kiasi kikubwa kwa takribani asilimia 95 ambapo kwa mwaka 2020/2021 kiwango kilishuka na kufikia asilimia 81 kutokana na mlipuko wa UVIKO-19.

"Baada ya mlipuko wa Uviko-19 watu wengi waliogopa kufika kwenye vituo vya afya ili kupata Chanjo wakihofia watoto wao na wao wenyewe kupata UVIKO-19,"amesema Bi. Gadau.

Amebainisha kuwa , kutokana na mdororo huo wa mwitikio wanajamii kuwachanja watoto wao mwaka 2022 kuliibuka mlipuko wa ugonjwa wa surua na watoto Takribani 3,923 walibainika kupata ugonjwa huo.

Bi. Gadau aliongeza kuwa, Mpango wa Taifa wa Chanjo umekuwa ukihakikisha wanajiunga na Kampeni nyingine za Afya ikiwemo, kampeni ya HIV, Malaria na RCH  ili kutoa elimu ya chanjo na chanjo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news