Serikali yasitisha usajili wa Kanisa la Spirit Word Ministry lililopo Ukonga Dar es Salaam

NA MWANDISHI WETU

WIZARA ya Mambo ya Ndani imesitisha usajili wa Kanisa la Spirit Word Ministry lililopo eneo la Stakishari Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam baada ya kubainika kutoa mahubiri na mafundisho yenye mwelekeo wa kuhamasisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
Hivi karibuni Kanisa la Spirit Word Ministry linaloongozwa na Askofu Dkt.Ceasar Masisi na mkewe Grace huko Ukonga Stakishari Polisi jijini Dar es Salaam lilisitisha huduma zake baada ya kupokea notisi.

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Mhandisi Hamad Masauni ameyasema hayo leo Mei 29,2024 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mhandisi Masauni amesema, katika kudhibiti na kupambana na vitendo vya mmomonyoko wa maadili Ofisi ya Msajili wa Jumuiya imesitisha shughuli za Jumuiya ya kidini iitwayo Spirit Word Ministry iliyopo eneo la Stakishari Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

“Jumuiya hiyo imefutiwa usajili kwa sababu ya kutoa mahubiri na mafundisho yenye mwelekeo wa kuhamasisha vitendo vya mapenzi ya jinsia moja na kutoa ujumbe wenye kuhafifisha jitihada za kupambana na vitendo vya ushoga nchini,”amesema Mhandisi Masauni.

Wakati huo huo Mheshimiwa Masauni amesema, taarifa zimekusanywa zinazohusu idadi ya vituo vya kulea watoto na shule zinazotoa mafundisho ya dini kwa watoto wadogo.

Amesema, lengo ni kutambua idadi ya vituo au shule za bweni zinazotoa mafunzo yenye mwelekeo unaokinzana na maadili ya nchi yetu ikiwemo vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.

Pia, amesema katika mwaka 2023/24 wizara imepanga kuandaa mwongozo wa taratibu za kuabudu na ithibati ya taasisi zinazotoa elimu ya dini, kuimarisha ufuatiliaji na utendaji wa Jumuiya za Kidini na zisizokuwa za Kidini nchini.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni pia amesema, hali ya usalama barabarani imeendelea kuimarika.

“Hali ya usalama barabarani imeendelea kuimarika kutokana na Polisi kuendelea kusimamia Sheria za Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Wadau ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 matukio ya ajali 1,283 yaliyotolewa taarifa ikilinganishwa na matukio 1,731 yaliyotolewa taarifa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22 ikiwa ni kupungua kwa matukio 448 sawa na 25.9%”

“Kupungua kwa matukio ya ajali kunatokana na kuimarisha usimamizi wa sheria, kufanyika kwa operesheni maalum, doria na misako nchi nzima, aidha elimu ya usalama barabarani imeendelea kutolewa kwa makundi yanayotumia barabara, matukio ya ajali yalisababisha watu 1,893 kujeruhiwa katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 ikilinganishwa na watu 2,323 waliojeruhiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22, idadi ya majeruhi imepungua kwa Watu 430, sawa na asilimia
18.5.

“Aidha, matukio hayo yalisababisha vifo 842 katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Mei, 2023 ikilinganishwa na vifo 946 katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22, idadi ya vifo imepungua kwa watu 104, sawa na asilimia 11.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news