Serikali yataja tija zaidi uwekezaji mpya wa Twiga Cement kwenye Kiwanda cha Tanga Cement

NA BENNY MWAIPAJA-WFM

SERIKALI imewahakikishia watanzania kuwa uwekezaji mpya wa zaidi ya dola za Marekani milioni 400 utakaofanywa na Kiwanda cha Saruji cha Twiga kwenye Kiwanda cha Saruji Tanga, utaongeza uzalishaji wa saruji, kukuza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi mbalimbali.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa tano kushoto), Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa sita kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement Bw. Reinhardt Swart (wa nne kushoto), Mkuu wa masuala ya Fedha wa Tanga Cement, Bw. Pieter de Jager (wa tatu kushoto) Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu Mwamba (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah (wa tatu kulia), Mtendaji Mkuu wa Tume ya Ushindani wa Biashara, Bw. William Urio (wa pili kulia), Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Tanga Cement, Mhandisi Benedict Lema (wa tano kulia), Mkurugenzi Msadizi Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Zawadi Maginga (kushoto), baada ya kukutana na kufanya mazungumzo, Ofisi za Treasury Square, Jijini Dodoma.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), walipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa kiwanda cha Tanga Cement, Jijini Dodoma.

Dkt. Kijaji alisema kuwa Kiwanda cha Saruji cha Tanga kupata mwekezaji mpya lilikuwa jambo lisilokwepeka kutokana kiwanda hicho kupata hasara kwenye mizania yake ya biashara kwa miaka mitano mfululizo na hivyo kuweka rehani zaidi za ajira za wafanyakazi 3,000 wa kiwanda hicho pamoja na mapato ya Serikali.

Alisema kuwa mtaji huo wa dola za Marekani milioni 400, sawa na zaidi ya shilingi bilioni 930, utakifanya kiwanda hicho kuzalisha saruji kwa wingi itakayokidhi soko la ndani, Afrika Mashariki, na Eneo Huru la Biashara la Afrika kwa ujumla.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (katikati), Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wapili kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement Bw. Reinhardt Swart (wa tatu kushoto), Mkuu wa masuala ya Fedha wa Tanga Cement, Bw. Pieter de Jager (wa kwanza kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni hiyo Mhandisi Benedict Lema, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo, Ofisi za Treasury Square, Jijini Dodoma.

“Tunaamini kuwa Kiwanda cha Tanga Cement kitaongeza uzalishaji kwa kiwango chake cha mwanzo na kuendelea kutoa ajira za watanzania 3,000, pamoja na matarajio ya kiwanda hicho kuanza kulipa kodi Serikalini baada ya mwaka mmoja ujao,” alisema Dkt. Kijaji

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alisema kuwa uamuzi wa Serikali wa kukinusuru kiwanda hicho umechukuliwa kwa umakini mkubwa na kuishauri Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuharakisha uwekezaji huo ili ukamilike kama ilivyopangwa.

Alisema kiwanda hicho kina mchango mkubwa wa kukuza ajira, kutoa kodi Serikalini lakini kikubwa ni kuongezeka kwa uzalishaji wa saruji kunakotarajiwa ambako kutawafanya wananchi wapate saruji kwa bei nafuu ili kujenga makazi bora.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakiwa katika kikao na ujumbe wa Kiwanda cha Saruji-Tanga (Tanga Cement), (hawako pichani), katika Jengo la Treasury Square, Jijini Dodoma, kujadili hatua zilizofikiwa za kuuza hisa za kampuni hiyo kwa Kampuni ya Twiga Cement ili kuongeza uzalishaji wa saruji na pia kulinda ajira za wafanyakazi baada ya Tanga Cement kutetereka kibiashara kwa zaidi ya miaka mitano mfululizo.

“Uzalishaji ufanyike ili wananchi wapate saruji ili wajenge nyumba bora, na watafanya hivyo bei ya saruji ikiwa chini, uzalishaji ukiwa mkubwa, tunauhakika wananchi watapata sementi kwa bei nafuu” alisema Dkt. Nchemba.

Aliwaomba Tanga Cement kuwafikishia wawekezaji wengine taarifa za uwepo wa mazingira bora ya uwekezaji hapa nchini na kuwaomba na wao pia wachangamkie fursa hizo ili waweze kunufaika kibiashara.

Aliitaka timu ya wataalam wa Wizara ya Fedha na Mipango, Tanga Cement na mwekezaji mpya Twiga Cement, kukamilisha haraka ukokotoaji wa hesabu za kodi ya zuio (Capital gain tax) ambayo Serikali inatakiwa kupata kutokana na uwekezaji huo.
Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah kushoto), Mtendaji Mkuu wa Tume ya Ushindani wa Biashara, Bw. William Urio, Kamishna Idara ya Sera, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, Mkurugenzi Msadizi Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Zawadi Maginga na kamishna Msaidizi, Idara ya Mipango ya Kitaifa, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Muhajir Kachwamba, wakiwa katika mkutano kati ya Uongozi wa Kiwanda cha Saruji cha Tanga (Tanga Cement) na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) (wa tano kushoto) pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hawapo pichani), Ofisi za Treasury Square, Jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango-Dodoma).

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho cha Saruji Tanga Bw. Reihardt Swart, aliipongeza Serikali kwa kukamilisha mchakato huo wa kuiwezesha kampuni yake kukabidhi kiwanda chao kwa mwekezaji mwingine-Twaga Cement, ahatua ambayo alisema itaongeza mchango wa kiwanda katika uchumi wa nchi.

Kwa mujibu wa Dkt. Kijaji, Tanga Cement, inatarajia kuachia hisa zake asilimia 68.33 kwa Kampuni ya Twiga Cement ili iwekeze mtaji huo wa zaidi ya dola za Marekani milioni 400 kwa ajili ya kuzalisha saruji itakayosaidia kupunguza upungufu wa bidhaa hiyo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news