Simba SC yapunguzwa kasi ubingwa Ligi Kuu ya NBC

NA DIRAMAKINI

NAMUNGO FC wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu NBC Tanzania Bara leo katika dimba la Majaliwa lililopo Ruangwa mkoani Lindi.

Mchezo ulianza kwa kasi ya kawaida huku tukishambuliana kwa zamu huku umiliki wa mpira ukiwa zaidi upande wetu.

Jean Baleke aliwapatia Simba SC bao la kwanza kwa shuti la mguu wa kushoto akiwa ndani ya 18 akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Saido Ntibazonkiza dakika ya 27.

Hassan Kabunda aliisawazishia Namungo dakika ya 39 baada ya mlinda mlango Ally Salim kukosea kuondoa mpira wa kona uliopigwa na Shiza Kichuya kabla ya kumkuta mfungaji.

Kwa matokeo hayo, Simba SC inafikisha alama 64 katika mechi ya 27, ingawa wanabaki nafasi ya pili wakizidiwa alama nne na mabingwa watetezi, Yanga SC ambao pia wana mechi moja mkononi.

Aidha, Namungo FC kwa upande wao wanafikisha alama 36, ingawa wanabaki nafasi ya sita wakizidiwa alama moja na Geita Gold baada ya wote kucheza mechi 27.

Wakati huo huo, watani wa jadi Yanga wanaonekana kukabiliwa na ratiba ngumu ya kucheza mechi tatu za mashindano tofauti ndani ya siku saba katika Mkoa wa Singida na Jiji la Dar es Salaam.

Kesho, Yanga itacheza mechi ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara na Jumapili Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) zote dhidi ya Singida Uwanja wa LITI.

Aidha, baada ya hapo watasafiri kurejea Dar es Salaam kwa mchezo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini siku ya Mei 10.

Yanga SC kwa saas imebakiza jumla mechi nne za Ligi Kuu NBC Tanzania Bara pamoja na huo wa Singida Big Stars, nyingine dhidi ya Dodoma Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons zote ugenini na wanatakiwa kushinda mechi tatu ili kutetea ubingwa wao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news