SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-19

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...nyuma ya usukani Padri Samson Mcjohn alikuwa akiendesha gari kwa kasi ya ajabu akielekea parokiani kwake.

Endelea

Lile kundi la wachawi lilikuwa imara kuwasubiria mapadri hao. Punde si punde waliliona gari hilo likiwa kwenye kasi ya ajabu likijongea maeneo yao.

Lilipofika mapanda njia lilipunguza mwendo kisha likakunja kushoto na kuikamata barabara iendayo mikoroshoni. Gari lile liliyumba kidogo, lakini kwa ustadi wa dereva lilitulia barabarani kisha akaongeza mwendo.

Lilipofika eneo lililokuwa na dawa liliyumba tena, dereva alipojaribu kuliweka vyema hakufanikiwa. Kwa mbele kulikuwa na gari la mizigo, lililokuwa limebeba shehena za mbao likielekea upande waliokuwa wakitokea wao.

Zile dawa zilikuwa kwenye mvutano, kupitia mvutano huo gari la Padri Samson lililivaa gari hilo la mbao. Kwa kuwa gari la mbao lilikuwa kubwa na lenye uzito kuliko like la Padri, hivyo gari la padri lilijikuta likipaishwa juu mithili ya mbayiwayi na kudondokea mtaroni. Wale wachawi waliwahi haraka kwenye eneo la hatari na kuwatoa wale wazungu ndani ya gari.

Wale vijana watumikiaji hawakuwa na jeraha hata kidogo, wao waliachwa garini humo wakiwa wamezirai. Lilikuwa ni tukio la haraka sana kuwatoa mapadri hao na kuingiza sanamu za mifano yao.

Japo walikuwa chini ya ulinzi wa wachawi,mapadri hao hawakuwa wakijitambua hata kidogo. Ile gari yao ilimwagiwa damu za wanyama haraka haraka na kuwa chepe chepe. Jambo jingine lililofanyika pale kwa haraka, zile sanamu zilifanyiwa matukio mengine ya kuogofya.

Lengo lilikuwa ni kuleta taharuki kwa washuhudiaji wa ajali, sanamu iliyokuwa na sura ya Padri Samson kichwa chake kilibondeka kisha macho yakatokeza kwa nje mithili ya kurunzi la garimoshi.

Kwa mtu wa kawaida asingejaribu kuiangalia hata kidogo maiti hiyo ya kubumba, iliogofya sana kuitama kwa mtu yeyote.

Padri mmoja sanamu yake ilitenganishwa kiwiliwili na kichwa. Wale Mapadri wawili waliosalia, sanamu za miili yao zilionekana kupondeka pondeka mithili ya nyama buchani.

Hapa niseme kidogo, ndugu msomaji zipo ajali za kweli na zingine za kutengeneza. Katika ulimwengu wa giza kuna baadhi ya watu huweza kuchukuliwa kupitia ajali za kutengeneza. Watu hao huchukuliwa wazima wazima, na kupelekwa eneo husika kama walivyokusudiwa.

Mara nyingi ajali za namna hii huwa za kutisha au kuogofya, lengo ni kuwatisha watazamaji wasipate umakini wa kumbaini ndugu yao. Lengo jingine huwa ni kuwafanya ndugu na jamaa wa mtu aliyechukuliwa kutoa maamzi ya kumzika haraka maiti huyo.

Eneo la ajali lilifurika watu, kulikuwa na watu wengi zaidi ya mchanga wa baharini, wengi wao walikuwa wakilia kwa uchungu.

Wapo baadhi walikuwa wakilifahamu gari la Padri Samson, wao walikuwa na imani ya kuwa Padri alikuwa ameaga dunia kupitia ajali hiyo. Lile gari la mbao lilikuwa pembeni limepaki likisubiri vipimo na utaratibu mwingine wa askari wa barabarani.

Baada ya askari wa barabarani kufika, walifanya vipimo vyao kisha wakawaagiza madaktari kuitoa miili ya marehemu iliyokuwa ndani ya gari. Simanzi lilitawala maeneo hayo, miili ya marehemu ilitia hofu kuingalia.

Jambo lililoleta faraja kidogo ni kukuta miili ya vijana wawili wa kiafrika wakiwa salama, madaktari waliwapima haraka na kubaini kuwa walikuwa wamezimia. Haraka vijana hao walichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa matibabu ya haraka ili kuokoa maisha yao.

Wale wachawi hawakutaka kupoteza muda, waliwabeba mateka wao na kuelekea kambini kwao. Ilikuwa ni siku ya furaha kwa wachawi wa kambi hiyo, hatimaye mtu aliyewasumbua kwa muda mrefu alikuwa mikononi mwao.

Kila muda walimwagia sifa kedekede mtoto THE BOMBOM kwa kufanikisha kumkamata mzungu huyo. Kwa upande wa mtoto huyo, alikuwa na furaha ya hali ya juu.

Kilikuwa ni kisasi chake cha kwanza dhidi ya Padri huyo kwa aliyoyafanya kwa bibi yake. Pili lilikuwa ni pigo kubwa kwa makampuni na taasisi za ulaya zilizokuwa na mipango ya kukatisha maisha ya mtoto huyo.

Wakati hayo yakiendelea free massony na illuminati walikuwa na habari za kuchukuliwa kwa mapadri hao. Hizi zilikuwa ni miongoni mwa jamii za siri ambazo zilikuwa zikifanya kazi na wachawi wa ulaya ili kuzuia kuzaliwa kwa nabii wa kiafrika.

Walitoa taarifa haraka kwa taasisi zilizokuwa zikifanyiwa kazi na mapadri hao. Jambo hili lilileta simanzi kuu kwa kampuni na taasisi hizo, kitendo hicho kiliwaongezea hasira wakadhamiria kuisambaratisha kambi hiyo na kumshikisha adabu mtoto THE BOMBOM.

Hatimaye wachawi hao waliwafikisha mateka wao kambini, mara baada ya kuwafikisha waliwamwagia dawa za kuwazindua.

Punde si punde mateka hao walizinduka toka kwenye lindi la usingizi waliokuwa wamewekewa kupitia madawa wakati wa ajali. Hapa niseme kidogo, zipo dawa nyingi za kuleta usingizi kwa mtu yeyote ambazo hutumiwa na wachawi.

Dawa hizo hutofautiana kulingana na malengo ya wachawi, kwa hapa walikuwa wametumia dawa kali ijulikanayo kama Itimbya nh'olo. Mara nyingi dawa hii hutumiwa kuwachukua watu kipindi cha ajali, humfanya mhusika kulala usingizi mzito zaidi.

Mara baada ya kushituka walishangaa kujikuta wakiwa katikati ya kundi kubwa la wachawi ambao walikuwa ni mahasimu wake.

Taarifa za kukamatwa kwa Padri huyo zilikuwa zimezagaa kwa jamii zote za wachawi, hata jamii ya wachawi wa kiafrika iliyokuwa ikifanya kazi na Padri huyo ilikuwa na taarifa hizo.

Wachawi wa kambi hiyo ambao muda huo walikuwa majumbani mwao waliamua kwenda kambini muda huo. Lilikuwa ni tukio kubwa ambalo liliteka nyoyo za kila mchawi wa kambi hiyo, walivutiwa sana na tukio la kumkamata Padri huyo aliyekuwa akiingilia shughuli zao.

Maazimio ya kambi hiyo toka zamani walipanga kuwa siku ambayo wangemtia mkononi mwao Padri huyo wangemla nyama mzima mzima.

Hili lilikuwa ni jambo jema kwao, kwani kumla nyama mbichi mzungu huyo kungewapa nguvu nyingi katika shughuli za kichawi. Nyama za wazungu zilizochemshwa huwa siyo tamu kwa kuwa huwa zinawahi kutepeta.

Walipanga kumla nyama akiwa mzima, walitaka afe huku anajiona ili liwe fundisho pia kwa wazungu wanaofanya shughuli za kishenzi ndani ya Afrika.

Ilipofika muda wa saa tano usiku, kulikuwa na wachawi wa aina mbalimbali kambini hapo. Kila mmoja alionekana kuifurahia siku hiyo, muda wa tukio ulipofika mateka hao waliletwa mbele ya meza kuu. Wazungu hao walikuwa uchi wa mnyama, wakiwa wamefungwa kwa waya kwenye gogo kubwa lililokuwa eneo hilo.

Kiongozi mkuu wa kambi hiyo alisimama na kuhutubia kwa kifupi, baada ya hapo alisogea eneo alipokuwa kafungwa Padri Samson.

Alipofika aliinamisha kichwa chake shafuni kwa Padri huyo na kuling'ata kwa nguvu na kutoka na mnofu wa shavu. Damu za Padri huyo zilichuruzika kwa wingi na kuacha donda kubwa, donda hilo lilionesha mpaka taya zilizokuwa wazi.

Ikafika zamu ya mkuu masidizi wa kambi hiyo, alinyanyuka na kumsogelea Padri huyo. Yeye alikamata vidole viwili vya mkono wa kulia, alivitumbukiza mdomoni mwake kisha akaving'ata kwa nguvu na kuvikata.

Maumivu aliyokuwa akipitia Padri huyo yalikuwa ni siri yake, alilia machozi ya damu lakini hakuwa na msaada wa aina yeyote. Ikafika zamu ya mtoto THE BOMBOM yeye alipofika aling'ata kidevu cha Padri huyo na kukinyofoa.

Maumivu yaaliongezeka mara dufu kwa Padri huyo, alikuwa akilia kwa uchungu, lakini hakuwa na namna ya kuepuka kikombe hicho.

Ikafika zamu ya kila mchawi kufurahia nyama tamu za Mapadri hao, waliendelea kula nyama hizo kwa utaratibu wa kila mmoja kwenda kujikatia kiasi cha nyama kwa mdomo wake.

Utaratibu huu uliendelea mpaka nyama za Mapadri hao zilipotamatika, walikufa kwa kifo kibaya kilichokuwa na maumivu yasiyo na maelezo. Huo ukawa mwisho wa Padri huyo na wenzake watatu.

Ndugu msomaji Padri Samson Mcjohn, ameliwa nyama pasi na huruma na wachawi hao. Unadhani nini kitaendelea kwenye simulizi hii ya kusisimua.

Endelea kufuatilia kisa hiki cha kutisha kilichotungwa na gwiji la simulizi za UHALISIJABU, WILLIAM DAUD BOMBOM.

GW'ABEJA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news