SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-21

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...pale msibani lilibaki gumzo juu ya tukio hilo, waislamu walisilimu na kufuata dini ya mtoto huyo. Wapagani waliamua kuwa wafuasi watiifu wa mtoto huyu, wakirsto ndiyo usiseme walikuwa watiifu zaidi.

Endelea

Kundi la watu walikuwa wakimshangilia mtoto huyo, kwa miujiza aliyokuwa akiifanya kila jamii ilianza kuamini unabii wake.

Kulikuwa na umati mkubwa wa wanaume waliokuwa wakimfuata, watoto na kina mama hawakuwa na idadi.

Muujiza aliokuwa kaufanya mtoto huyo wa kumfufua shekhe mkuu wa kata, uliwafanya waislamu na wakristo kusahau dini zao na kuwa kitu kimoja.

Safari ya kuelekea kwa Mchungaji wa Shika Maneno Tenda Maneno, aliyekuwa amefariki iliwafanya watu kuacha kazi zao na kumfuata mtoto huyo.

Njia ilighubikwa na utitiri wa watu waliokuwa wakimfuata, habari ya miujiza ya mtoto THE BOMBOM ilikuwa ikisambaa kama moto wa petroli nyikani. Hatimaye akawa amefika msibani kwa mchungaji huyo, waombolezaji walikuwa si wengi sana.

Idadi kubwa ya watu waliokuwa wameambatana na mtoto THE BOMBOM iliwafanya waombolezaji wa msiba wa mchungaji kuduwaa.

Hata hivyo, walipiga moyo konde na kuwakaribisha wageni hao, wakati huo mtoto THE BOMBOM alikuwa amezungukwa na kundi lile.

Alipofika karibu yao aliwasalimia kwa lugha ya kisukuma "Kinehe badogo mle mhola?" (vipi ndugu zangu mko salama?). Mtu mmoja aliyeonekana kula chumvi nyingi alijibu "tote mhola gw'anang'wise, ontongeji wi kelesia lise wazumaleka lelo tulenabopena nkoi" akimaanisha ( hatuko salama ndugu yetu, kiongozi wetu wa kanisa amefariki hivyo tuko kwenye majonzi ndugu).

Kabla mtoto THE BOMBOM hajazungumza kitu, alitokea mke wa marehemu na mama wa marehemu wakiwa wamebeba mafuta ya samuli kwenye kibuyu. Mafuta haya hutokana na maziwa ya ng'ombe, mafuta haya ni maarufu sana kwa jamii ya wafugaji hasa ng'ombe.

Wanawake hao walianguka kifudifudi miguuni mwa mtoto THE BOMBOM na kuanza kulia. Uchungu waliouonesha mbele ya mtoto huyo ulikuwa hauna maelezo, walifungua kibuyu hicho kisha wakamimina mafuta miguuni mwake.
Walimpaka miguu yote miwili huku wakimuomba kumfufua mchungaji huyo, wakati huo ndugu wengine wa marehemu walikuwa wamemzunguka mtoto THE BOMBOM.

Vilio vyao mbele yake vilidhihirisha uchungu mzito waliokuwa nao moyoni mwao, hii ikampa imani mtoto huyo na kuamua kutenda miujiza.

Aliwauliza mahali alipokuwa kahifadhiwa marehemu, walimchukua na kumpeleka karibu ya mlango wa chumba alichohifadhiwa.

Alipokaribia mlangoni alipiga magoti na kuibusu ardhi, kisha alisimama na kuwageukia makutano waliokuwa msibani hapo. Aliwauliza kama walikuwa wakisadiki kwa mungu wake, kila mmoja alipiga makofi huku akipasa sauti ya kusadiki juu ya mungu wa mtoto THE BOMBOM.

Akiwa kasimama pale mlangoni ghafla ulitokea upepo mkali wa kisulisuli, upepo huo ulipelekea watu kutoonana katika eneo hilo.

Ndugu msomaji upepo huo haukutokea kwa bahati mbaya, kulikuwa na kundi la wachawi wa eneo hilo walitaka kumuaibisha mtoto huyo.

Hivyo walileta upepo huo ukiwa na nguvu fulani za kichawi, tayari walijua kuwa mtoto huyo alikuwa amekwisha anza kujenga mizizi ndani ya jamii ya kupendwa.

Wachawi hao walikuwa ni masalia ya wafuasi wa Ng'wana Michembe pamoja na Padri Samson. Walikuwa na jakamoyo dhidi ya mtoto huyo, walitamani kulipiza kisasi.

Mtoto huyo aliinama chini na kuchukua mchanga, aliutemea mate kisha akazungumza maneno kadhaa. Baada ya hapo aliurusha mchanga huo hewani, mara upepo ulikoma pakawa shwari.

Watu walibaki wakishangaa tukio hilo, alisogea zaidi mlangoni na kumuita marehemu huyo. Ghafla ilisikika sauti toka ndani ya chumba hicho, mlango ulifungulia akajitokeza mchungaji huyo akiwa hai.

Alikuwa katika mavazi ya kanzu ya kichungaji, watu walipomuona mchungaji huyo walipasa sauti ya kulitukuza jina la mungu wa mtoto THE BOMBOM.

Yalizungumzwa maneno mengi juu ya mtoto huyo, wengine walisema yamkini mtoto huyo alikuwa ni mjukuu wa nabii wa wasukuma aliyejulikana kwa jina la Ng'wana Malundi.

Huyu alikuwa ni miongoni mwa nabii wa kisukuma aliyefanya miujiza mingi, mpaka leo kaburi lake lipo maeneo ya Shinyanga. Watu huenda kuhiji kwenye kaburi hilo, lenye miujiza ya kushangaza.

Wengine walisema mtoto huyo alitokea ukoo wa Bulungute, miongoni mwa manabii wa kisukuma waliofanya miujiza mikubwa ndani ya jamii hiyo.

Nabii huyo kila alipokasirika aliweza kuvimba na kujaa nyumba nzima. Wengine walimfananisha mtoto huyo na Mabula Mchane, huyu naye alikuwa ni nabii wa mungu aliyeletwa katika jamii ya kisukuma ili kuwaokoa watu na matatizo mbalimbali.

Kila mmoja msibani hapo alizungumza maneno yake kulingana na alivyoshuhudia miujiza hiyo, hatimaye mtoto huyo alipasa sauti ya kuwasihi kumsikiliza.

Makutano yote yalikaa kimya kisha akazungumza, aliwaambia kuwa yeye ni nani na anafanya miujiza kupitia nguvu za mungu wake.

Aliwasii makutano wote kutotangaza miujiza aliyokuwa akiitenda kisha akaondoka eneo hilo, wakati anaondoka eneo hilo watu waliamua kumfuata.

Idadi ya watu ilikuwa kubwa iliyosababisha shughuli nyingi kusimama kwa muda kila alipokuwa akipita, hili lilimchukiza OCS wa kituo kidogo cha Polisi cha Ilongo.

Mkuu huyo wa kituo alipenda sana kuzunguka mbuyu, alikuwa ni miongoni mwa askari waliokuwa na ukwasi mkubwa kupitia rushwa alizoziendekeza.

Mkuu huyo alikuwa amechanga vizuri kete zake, alipanga kumkamata mtoto THE BOMBOM ili wafuasi wake watoe hongo ya kumtoa.

Akiwa na polisi wengine walikwenda kumkamata mtoto huyo na kumpeleka kituoni hapo, walipomfikisha kituoni walimuuliza maswali kadha wa kadha ya kuzuga kisha wakamtupa ndani.

Wafuasi wa mtoto huyo walichachamaa dhidi ya hatua zilizokuwa zimechukuliwa na askari hao. Taarifa za kukamatwa kwa mtoto huyo zilimfikia kamanda wa polisi wa Wilaya ya Magu, Mkuu wa Wilaya Bwana Wambali Roho Yawivu pamoja na Mkurugenzi.

Wakati taarifa zinawafikia viongozi hao walikuwa kwenye kikao cha kujadili eneo lipi walilokuwa wakikusudia kulitoa kwa ajili ya kanisa la SURVIVE FROM THE DEATH.

Viongozi hao walitaka kuwa miongoni mwa wafuasi wakubwa wa mwanzo wa nabii mtoto THE BOMBOM. Hata hivyo walikuwa wamepewa maelekezo toka juu, maelekezo hayo yaliwataka kumpatia mtoto huyo eneo la kutosha la kufungua taasisi yake ya kanisa.

Kitendo alichofanya OCS wa Ilongo kiliwaudhi viongozi hao, hawakupenda kwa kuwa kingeleta tafrani zisizo na maana ndani ya jamii.

Endapo wafuasi wa mtoto huyo wangeliamua kujichukulia hatua mikononi, hakuna kituo chochote cha askari polisi wangeweza kuwadhibiti.

Viongozi hao walimpigia simu Mkuu huyo wa kituo akawa hapatikani, walichukua gari haraka wakaelekea kituoni hapo kwa ajili ya kuepusha ghasia hiyo.

Walipofika kituoni walikuta kundi kubwa la watu waliokuwa wamezingira kituo hicho, wengine walikuwa wamebeba mawe mikononi huku wengine wakiwa na marungu.

Waliposhuka ndani ya gari viongozi hao waliwasalimia watu hao, kisha wakawasihi kutochukua sheria mkononi. Waliwahakikishia kumaliza matatizo yaliyokuwa yakiendelea eneo hilo, baada ya hapo waliingia kituoni humo.

Mle ndani walipokelewa vizuri na Mkuu wa Polisi wa kata, walizungumza mawili matatu kisha wakamuagiza kumtoa mara moja mtoto THE BOMBOM.

Askari huyo alikwenda kwenye chumba cha mahabusu na kufungua, jambo la kushangaza hakuna sauti ya mtuhumiwa yeyote aliyosikika. Alipoingia mahabusu humo hakukuwa na mtu yeyote.

Alipiga kelele zilizowashitua hata viongozi waliokuwa wamefika kituoni hapo. Viongozi hao walikimbilia kwenye mahabusu hiyo, walipofika eneo hilo walishangaa kuikuta mahabusu ikiwa tupu.

Wakati huo wafuasi wa mtoto huyo kule nje ya kituo walikuwa wakipiga kelele za kuomba kuachiliwa kwa nabii wao. Mkuu wa kituo hicho kwa mara ya kwanza jasho likamtiririka mithili ya mtu anayepigwa nyungu.

Viongozi hawakutaka kuelewa chochote juu ya majibu mepesi ya Mkuu huyo wa kituo. Haiwezekani mtu umweke ndani harafu apotee kiaina aina ndani ya mahabusu, Mkuu huyo wa kituo alikosa la kujitetea mbele za mabosi wake.

Ndugu msomaji, unadhani mtoto THE BOMBOM na mahabusu wengine wameelekea wapi? Je, wamo ndani ya mahabusu au wametoroka?.

Na kama wametoroka walifanikiwaje kutoroka ndani ya mahabusu iliyo chini ya askari wenye silaha za moto? Na kama wamo ndani ya mahabusu kwa nini hawaonekani? Ungana nami katika simulizi hii, sehemu inayofuata.

N'HUMBELA CHALO

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news