SIMULIZI YA KUTISHA KATIKA MAISHA-27

NA WILLIAM BOMBOM

Ilipoishia...Walikifungua kiroba hicho kilichokuwa na binadamu mwenye ulemavu wa miguu yaani kiwete. Watu hao walipaswa kuchinjwa ili kuleta upatanisho baina ya mungu wa wazungu hao pamoja nao.

Endelea

Walimshika yule albino wakamkandamiza chini kisha wakaanza kumnyoa nywele zake. Walianza na nywele za kichwani, makwapani na sehemu za siri, wakati hayo yakiendelea wazungu sita walikuwa wakiwazunguka wenzao huku wakicheza ngoma za kichawi.

Walikuwa uchi wa mnyama isipokuwa sehemu za siri tu walipokuwa wamejistiri kwa ngozi ya mnyama fulani.

Waliziweka pembeni nywele hizo kisha wakaanza kumkata kucha zake, walikata kucha za mguu wa kulia kisha mkono wa kulia pekee harafu wakazichanganya na zile nywele.

Mpaka hapo hawakuwa wakijua kulikuwa na kundi jingine la kichawi lililokuwa likishuhudia mambo yao.

Yule mzungu mwenye jambia alisogea eneo hilo akiwa na jambia lake mkononi, aliushika uume wa albino huyo kisha akaukata kwa kasi. Bila aibu aliuchukua na kuung'ata mdomoni kisha akaanza kuutafuna pasi na shaka.

Yule albino aliendelea kugugumia kwa maumivu makali, hakuwa na uwezo wa kupiga kelele maana alikuwa kapakwa dawa za kuondoa sauti.

Damu zilichuruzika mithili ya mwanakondoo aliyechinjwa, hali haikuwa rafiki katika mazingira hayo. Taratibu yule mzungu alimpa kipisi cha uume mchawi mwenzie alichokibakiza aliyekuwa pembeni mwake, bila ajizi mchawi huyo alikipokea na kuanza kukitafuna mfano wa mhogo wa kuchomwa. Damu ziliendelea kuvuja toka eneo la jeraha, baadhi ya wachawi waliinama na kuanza kuinywa damu hiyo.

Baada ya hapo alikuja mzungu mwingine akiwa na jisu kubwa, akamchinja albino huyo akianzia nyuma ya shingo.

Huwezi amini namna albino huyo alivyokuwa akipambana kuokoa maisha yake, hata hivyo kupambana kwake ilikuwa kazi bure. Baada ya kumchinja walitenganisha miguu yake na kiwiliwili, kisha walitenganisha mikono yake.

Walikata sehemu ya nyama ya matako na kuziweka pembeni, waliendelea kumcharanga albino huyo mithili ya nyama ya ng'ombe buchani.

Walipokamilisha walichukua vipande vya mwili huo na kuanza kuvizika kwenye msingi wa jengo hilo lililokuwa linatarajiwa kuanza kujengwa ukuta.

Ndugu msomaji hapa niseme kidogo, asilimia kubwa ya majengo ya namna hiyo lazima huwa yanakuwa na kafara.

Zipo aina nyingi za kafara, kuna kafara za nafaka, kafara za mimea na wanyama. Kwa kawaida kafara ya wanyama hasa binadamu huwa na nguvu kuliko kafara zote, ndiyo maana wazungu hawa walifanya kafara za binadamu.

Ikumbukwe pia mbali ya kuwepo aina nyingi za kafara, lakini kafara hizo zimegawanyika katika makundi makuu mawili, ambayo ni kafara inayoonekana na isiyoonekana.

Kwa upande wa kafara inayoonekana, hii hutokea mchana kweupe huku watu wakishuhudia. mara nyingi kafara ya namna hii huwa iko kwenye mfumo wa ajali katika jengo linalotamatika.

Kwa kafara isiyoonekana hii hufanyika usiku mzito huku kafara mwenyewe akichinjwa, washiriki wakuu kwenye kafara hii ni wahusika tu.

Ndiyo maana wazungu hao walikuwa wakifanya kafara hii usiku huo, mbali ya damu ya kafara kumwagika pia sehemu za mwili wake huchimbia chini.

Tambiko hilo liliendelea kufanyika kwenye jengo hilo, wazungu hao hawakuwa na wasiwasi na mambo waliyokuwa wakiyafanya.

Walimchukua yule kiwete kisha wakamfunga kwenye lailoni jeusi, baada ya hapo walichimba shimo katikati ya chumba kimoja cha jengo hilo wakamzika mzima mzima.

Hawakuwa na huruma hata kidogo, kafara walizokuwa wakifanya zilihusiana na zindiko la kumzuia mtoto THE BOMBOM kufika maeneo hayo na kundi lake.

Pia majengo hayo yangeweza kutumiwa na wachawi wengine toka Ulaya kila watakapozuru Tanzania, hata baada ya kumuua mtoto THE BOMBOM.

Yule mtu mmoja aliyesalia kwa wale watatu , walimchukua na kuondoka naye. Eneo hilo lilibaki kimya kwa muda, mtoto huyo akatumia muda huo kuondoa zindiko lililokuwa limefanywa na wachawi hao wa kizungu.

Walianza kwa kumfukua yule kiwete aliyekuwa kachimbiwa mzima mzima ardhini, walifanikiwa lakini hali yake ilikuwa mbaya sana.

Walimpaka dawa fulani iliyomsaidia kupumua vyema, japo wao walikuwa wachawi lakini suala hili lilikuwa limewakera sana. Waliendelea kufukua maeneo yote yaliyokuwa yamechimbiwa kafara hizo, walizikusanya kafara hizo kisha wakaenda kuzichimbia eneo jingine tofauti na eneo hilo.

Baada ya hapo mtoto THE BOMBOM aligusanisha viganja vya mikono yake kisha akavisugua mara saba, alipoangalia mikononi hapo kulikuwa na video iliyokuwa ikiwaonesha wale wazungu walipokuwa wamekwenda.

Alibaini walikuwa wamekwenda kwenye makaburi ya Igoma, alishauliana na wenzake wakakubaliana kuwafuatilia huko huko makaburini.

Walimchukua yule kiwete na kumkabidhi kwa mchawi mmoja, yule mchawi alimchukua kiwete huyo na kurudi naye kambini Ihushi.

Kundi lililobakia lilielekea makaburi ya Igoma walikokuwa wameelekea wale wazungu, mpaka hapo mtoto THE BOMBOM na kundi lake walikuwa wamefanikiwa sana.

Kitendo cha wao kuwaona wazungu hao na kuzuia kwa upande wao kutoonekana machoni mwa wazungu ilikuwa ni ushindi mkubwa sana.

Kwa kuwa usafiri wao ulikuwa wa kukata, walikwenda kutua standi ya magari madogo Igoma. Wakaamua kutembea kwa miguu kuelekea makaburini huko, walikuwa wamesalia jumla ya wachawi kumi na tisa.

Walikamata njia inayoelekea kanisani, walipofika kwa Hobo, waliachana na barabara iendayo Kishiri wakanyoosha iendayo kanisa la Roman Catholic.

Kabla ya kufika kanisani waliona kundi la vijana walikuwa wamekaa nje ya bucha iitwayo IGOMA BUTCHER.

Hii ni miongoni mwa bucha inayopendwa sana na raia wa mji huo, hii ni kwa sababu ya unadhifu wa bucha yenyewe, huduma safi ya wahudumu na punguzo la nyama.

Bucha hiyo ipo upande wa kushoto kabla ya kufika kanisani ukiwa unapandisha kijimlima. Kwa kuwa mtoto THE BOMBOM na kundi lake wao walikuwa na uwezo wa kuona kila mtu huku wao wakiwa hawaonekani, waliamua kuwasogelea vijana hao ili kuona walichokuwa wakikifanya.

Walipofika eneo hilo walishangaa kuona vichwa vya mbwa vingi vikiwa chini, pia kulikuwa na ngozi za mbwa, mkia na miguu mingi.

Vijana hao walikuwa wakiendelea na kazi yao ya kuchuna mbwa, mzee mmoja aliyekuwa na tumbo kubwa mithili ya kiroba cha unga alikuwa akiwasimamia vijana hao.

Kwa haraka haraka mtoto THE BOMBOM alibaini kuwa mzee huyo ndiye aliyekuwa mmliki wa Bucha hiyo.

Kwa muda mrefu mzee huyo amekuwa akiifanya biashara hiyo, kumbe huwalisha nyama za mbwa wateja wake.

Mbwa wengi walikuwa wakichunwa na kuingizwa kwenye majokofu, ingekuwia vigumu sana kuitofautisha nyama ya mbwa na ile ya mbuzi.

Baadhi ya mbwa walionekana kuvimba, kwa kuwaangalia walibaini hao ni wale waliogongwa na magari au kuuliwa ndani ya jamii.

Mbwa wengine walikuwa wa kawaida kabisa, hawa walikuwa wamechinjwa kawaida. Biashara nyingi za kishirikina huwa namna hii, wapo ambao huuza udongo wa mfinyanzi ambapo machoni mwa mteja huonekana mnofu wa nyama.

Wengine huuza mavi ya mbuzi kwa muonekano wa karanga, wapo ambao huuza vitu vya hovyo kwa kutumia nguvu za giza. Mtoto THE BOMBOM na kundi lake waliachana na watu hao kisha wakaendelea na safari yao.

Walipofika kanisani walishangaa kuona nuru iliyokuwa iking'ara mfano wa nyota ya jaha, nuru hiyo ilizunguka kanisa hilo na kutamalaki eneo zima.

Kwa kuwa safari yao haikuwa kanisani hapo, waliachana na nuru hiyo wakasonga mbele. Walipita kanisani hapo wakatembea hatua chache wakapinda kushoto wakiachana na barabara inayoshuka hadi Four Ways.

Kwa mbele yake walipavuka kwa Mzinza, huyu ni miongoni mwa watu maarufu sana kwa jamii ya Igoma.

Waliendelea na safari yao ya makaburini, walipofika kwa mzee Ikombe walikutana na watu watatu waliokuwa wamebeba kitu mabegani.

Watu hao walikuwa wakitokea makaburini, walipoangalia vizuri waligundua walikuwa wamebeba maiti aliyefungwa sanda.

Kwa kuwa watu hao hawakuwa na uwezo wa kuwaona, waliwaacha wakaendelea na safari yao huku wakiwa na maiti wao.

Hatimaye wakafika kwa mzee Mashikolo, kutoka mji huo kwenda makaburini ni mwendo wa dakika tatu kwa miguu.

Wakati huo walikuwa wamejigawa kwenye makundi ya namba tasa, hii ni kanuni kuu ya kichawi wakati wa kutembea usiku.

Ndugu msomaji hapa nieleze kidogo, unapotembea wakati wa usiku usipende kuwa kwenye namba shufa.

Idadi hiyo husumbuliwa sana na wachawi kwa kuwa kiasili ya nguvu za kichawi inaruhisu kusumbuliwa, kulijua hili fuatilia simulizi yangu ya JICHO LA SHETANI MGONGONI MWA SHEKHE au BUNDI WA GAMBOSHI nimefafanua kwa kina.

Kundi la kwanza lilikuwa na watu watano kundi la pili watu saba na lile la tatu watu saba. Kule makaburini kulikuwa kumekucha, wachawi mbalimbali walikuwa wakishuka na vyombo vyao kufanya shughuli zao.

Ghafla alipita mtu mmoja aliyekuwa akielekea makaburini, mtu huyo alikuwa kapanda fisi aliyekuwa akikimbia kwa kasi.

Usafiri huu ulidhihirisha kuwa mtu huyo hakuwa mwenyeji wa mbali na mji huo, maana usafiri wa namna hii hutumiwa kwenye maeneo ya karibu karibu. Mara nyingi usafiri wa namna hii hutumiwa na wachawi wa kanda ya ziwa, hii ni kwa kuwa fisi hao hupatikana kwa urahisi.

Walipomuangalia vyema walimtambua alikuwa ni Mchungaji wa kanisa la Kiadventis Wasabato , wana mapokeo wa mtaa wa Mandela.

Mchungaji huyo alikuwa akielekea makaburini kufanya shughuli zake za kichawi. Kwa kuwa hakuwa na tatizo dhidi yao waliachana naye, ni miongoni mwa wachungaji waliokuwa na nguvu ya kuponya. Kumbe walitumia nguvu za ziada katika kufanikisha hayo.

Hatimaye walifika makaburini, kulikuwa na idadi kubwa ya wachawi tu. Haukuwa muda wa wanga maana wao hufanya kazi zao mapema, kumbuka mwanga na mchawi ni watu wawili tofauti.

Mmoja ana uwezo wa kuua mwingine hana uwezo wa kuua labda iwe bahati mbaya. Mmoja huloga wakati mwingine huwanga, mmoja hufanya kazi zake usiku na mchana mwingine hufanya kazi zake mapema kuanzia saa mbili hadi saa tano, kwa ufafanuzi zaidi soma simulizi ya VITA VYA MGANGA THE BOMBOM NA WACHAWI.


Walipofika makaburini waliwaona wale wazungu wakifukua kaburi mojawapo. Lile kaburi lilikuwa na siku tano toka mtu huyo azikwe, sijui walikuwa wamedhamiria nini ndani ya kaburi hilo.

Ndugu msomaji hapa niseme kidogo, wachawi wanapofukua kaburi huwa hawatumii jembe au koleo. Kuna fimbo maalumu ambayo hupigwa kaburini kisha yananuiwa maneno fulani, udongo wa kaburi hujiondoa wenyewe na kaburi kubaki wazi.

Mchakato huo huendelea hata kwa upande wa kufungua sanduku, sanda, kulifunga na kulirudisha kaburini.

Ni kazi rahisi sana ambayo haiwezi kumaliza hata dakika moja. Yapo makaburi ambayo hayana maiti, yaani alichukuliwa kwa kazi fulani au aliliwa nyama.

Ishara ya kaburi la namna hiyo ni kutumbukia upande mmoja au kichwani mwa kaburi hilo. Ukikuta mambo hayo kwenye kaburi la namna hiyo tambua hakuna mtu kaburini humo.

Ishara nyingine ni kuwa kaburi hilo huwa kimya sana, ni vigumu kuwakuta wadudu wanapiga kelele hii ni kutokana na dawa ya Ncheyeki ambayo humwagwa eneo hilo kipindi wanamchukua.

Kiashiria kingine ni kuvunjwa kwa vyungu juu au pembeni mwa kaburi au kukatwa ama kung'olewa kwa miti ya kaburi upande wa kulia kama mlipanda. Ukiona mambo hayo mojawapo au yote tambua hakuna mtu kaburini.

Ndugu msomaji mtoto THE BOMBOM amefika makaburini, lengo lake na kundi lake ni kuwafuatilia wazungu hao.

Wazungu hao nao wapo kwenye harakati ya kuchimba kaburi, ni kaburi la nani? Kwa nini wanachimba kaburi hilo? Hebu ungana nami katika simulizi hii ya sisimua sehemu inayofuata. KANISA LA KICHAWI.

BATWENEGI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news