Singida kuzaliwa upya asema Waziri Prof.Mbarawa

NA MWANDISHI WETU
Singida


WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema ujenzi wa Barabara za lami unaoendelea na utakaoanza hivi karibuni una lengo la kuufanya Mkoa wa Singida kuwa kiunganishi na kitovu cha biashara kwa mikoa ya kanda ya kaskazini, kati, ziwa na nyanda za juu kusini. 
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila na Mwakilishi kutoka kampuni ya China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO), wakisaini mikataba wa mradi wa ujenzi wa Barabara za Maingilio katika Daraja la Sibiti, Noranga-Doroto na
Itigi- Mkiwa, Mkoani Singida.

Akizungumza mjini Itigi katika hafla ya utiaji saini, mikataba ya ujenzi wa barabara za maingilio katika daraja la Sibiti zenye urefu wa KM 24.83 na barabara ya Makongolosi-Rungwa-Itigi-Mkiwa, sehemu ya Noranga hadi Doroto (KM 6) na Itigi hadi Mkiwa (KM25.569) kwa kiwango cha lami, Profesa Mbarawa amewataka wakazi wa Mkoa wa Singida kujipanga kutumia fursa za miradi hiyo kujikwamua kiuchumi. 
 
“Ujenzi wa Sehemu ya Noranga - Doroto na Itigi - Mkiwa ni Muendelezo wa juhudi za Serikali kuifungua barabara yote ya Makongorosi-Rungwa -Itigi hadi Mkiwa kwa kiwango cha lami, na hivyo kuinganisha Mikoa ya Singida na Mbeya kwa urahisi zaidi,”amesema Profesa Mbarawa.

Aidha, Profesa Mbarawa amewataka viongozi wa Mkoa wa Singida, kuwapa ushirikiano wa kutosha Mkandarasi China Henan International Cooperation Group Co. Ltd. (CHICO) na wataalamu wengine wanaojenga barabara hizo ili zikamilike katika ubora uliokusudiwa na mapema Zaidi. 

“Viongozi wa Mkoa na wa TANROADS, hakikisheni vijana wa mkoa wa Singida wanapata kipaumbele katika kupata ajira kwenye miradi inayoendelea ili kuwawezesha kunufaika kwa kupata utaalamu na kukua kiuchumi”. Amesisitiza Profesa Mbarawa. 
Barabara hizo zitakapokamilika zitaunganisha Kirahisi Mikoa ya Singida, Simiyu, Shinyanga , Arusha, Dodoma na Tabora na kufanya mkoa wa Singida kunufaika na Shughuli za kilimo, utalii na biashara. 

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila amesema kuwa barabara za Maingilio katika daraja la sibiti zitakapokamilika zitaondoaa adha ya usafiri katika daraja la hilo na hivyo kuvutia wasafirishaji wengi kupita njia hiyo. 

Eng. Mativila ameongeza kuwa ujenzi huo utahusisha upanuzi wa makaravati makubwa na madogo na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua kwenye sehemu zenye mmomonyoko wa udongo. 

Naye, Mbunge wa Manyoni Magharibi, Mhe Yahaya Masare akizungumza kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Singida, ameishukuru Serikali kwa namna inavyotekeleza Miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara mkoani humo, 

Barabara ya itigi hadi Mkiwa ni Sehemu ya barabara itokayo Mbeya kupitia Makongorosi-Rungwa-itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa Kilomita 413 ambapo sehemu ya Mbeya- Lwanjilo hadi Chunya (KM 72), na Chunya - Mkongorosi (KM 39), tayari imekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami. 

Katika hatua nyingine, Profesa Mbarawa amesema tayari Serikali imeshapata mkandarasi atakayejenga Barabara ya Handeni-Kibirashi hadi Singida (KM 462) na maandalizi ya kusaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Arusha-Kongwa Junction (KM 438), Mbulu-Hydom (KM 400), na Ifakara-Lupilo-Malinyi hadi Namtumbo (KM.480 ) nyatakamilika Mwezi juni mwaka huu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news