NA MWANDISHI WETU
MAMALAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imependekeza Mkataba wa Ruzuku za Uvuvi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) uzingatie wafanyabiashara na wavuvi wadogowadogo.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Biashara TanTrade, Bw. Freddy Liundi jijini Dar es Salaam akiambatana na Afisa Biashara Mwandamizi, Bi.Magreth Shirima, Afisa Habari Norah Thomas na Daniel Joseph.
Ni katika warsha iliyoandaliwa na Shirika la Biashara Duniani (WTO) wenye lengo la kujenga uelewa kuhusu Mkataba wa Kudhibiti Ruzuku kwenye Sekta ya Uvuvi (WTO- Fisheries Subsidies Agreement) inayofanyika kuanzia Mei 2 hadi 5, mwaka huu jijini humo ikihusisha washiriki kutoka nchi za Afrika zinazoongea Kiingereza ikiwa ni pamoja na Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Lesotho na Misri
Bw. Liundi amesema, TanTrade inapongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Biashara Duniani (WTO) katika kutunza rasimali za Bahari na inaendelea kushirikiana nalo katika kutoa ushauri wa kisera unaozingatia ustawi wa Wafanyabiashara na Wavuvi wadogogo nchini.
Mkataba wa Kudhibiti Ruzuku Sekta ya Uvuvi umejadiliwa takribani miaka 20 kabla ya nchi wanachama wa WTO kufikia makubaliano ya awali mwezi Juni 2022 wakati wa Mkutano wa 12 wa WTO wa Mawaziri unaofahamika kama Twelfth Ministerial Conference -MC12 wenye lengo la kulinda uendelevu wa rasilimali hai zilizoko baharini hususan samaki kupitia kudhibiti ruzuku ambazo zinapelekea wavuvi kuwa na uwezo mkubwa wa kuzunguka bahari zote na kufanya uvivi usio endelevu kwa kuvua kupita kiwango.
Warsha hiyo imefunguliwa rasmi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar Bw. Khamis Mwalimu ambapo ameseama ni muhimu mkataba huo kutoa nafasi ya kisera kwa nchi zinazoendelea kwa kuzipatia upendeleo maalum ili Serikali ziweze kuendeleza Sekta ya Uvuvi na rasilimali hai zilizoko baharini.
Bw. Mwalimu amesema kuwa sekta ya uvuvi ina mchango mkubwa kwa uchumi wa bara la Afrika ambapo kwa Tanzania ina kilometa 223 za eneo la uvuvi katika bahari ya hindi na kutoa ajira, hifadhi ya chakula, kipato kwa watu na Serikali hivyo ni muhimu mkataba huo kuizingatia mahitaji hayo.
Awamu ya pili ya majadiliano ya kuhitimisha mkataba huo yanaendelea WTO ambapo masuala muhimu yanayotarajiwa ni pamoja na kuhakikisha Mkataba huo unajumuisha upendeleo maalum kwa nchi zinazoendelea na wavuvi wadogo (artisanal fishing) na yanatarajiwa kukamilika kabla ya Mkutano wa 13 wa WTO wa Mawaziri (MC13) utakaofanyika Februari 2024.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa WTO, Bi. Angella Ellard ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuandaa warsha hiyo na kwa ushirikiano mzuri na kusema kuwa warsa hiyo ni muhimu ya kwakuwa bahari inakabiliwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya samaki ambayo inaendelea bila kusita.
Aliangazia kwamba serikali nyingi zinaendelea kutoa ruzuku za uvuvi bila kuzingatia athari zake kwa ustahimilivu.
Ruzuku hizo zinakadiriwa kufikia dola bilioni 35 kwa mwaka kote ulimwenguni, ambapo dola bilioni 22 zinahusiana na kuongeza uwezo wa uvuvi.