TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-15: Karibu Morogoro, Ni rahisi sana kutajirika

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, wakati Tanganyika inapata uhuru wake Desemba 9, 1961 Mkoa wa Morogoro ilikuwa ni sehemu ya Jimbo la Mashariki. Jimbo hilo lilijumuisha mikoa ya sasa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro.

Aidha, makao makuu ya jimbo yalikuwa Morogoro Mjini ambapo pia mkuu wa jimbo aliweka makazi na ofisi yake hapo. Mbunge wa kwaza Mwafrika kuongoza jimbo hilo alikuwa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Mkoa wa Morogoro ulianza rasmi mwaka 1962 ukiwa na wilaya tatu ambazo ni Morogoro, Kilosa na Ulanga. Ni mkoa wa pili kwa ukubwa hapa nchini kwa sasa ukitanguliwa na Mkoa wa Tabora.

Una eneo la kilomita za mraba 73,039. Eneo hili ni sawa na asilimia 7.7 ya eneo lote la Tanzania Bara, kati ya eneo hili kilomita 2 2,240 ni eneo la maji.

Mkoa umepakana na mikoa ya Pwani na Lindi kwa upande wa Mashariki, Manyara na Tanga kwa upande wa Kaskazini na kwa upande wa Magharibi umepakana na mikoa ya Dodoma na Iringa na upande wa Kusini unapakana na Mkoa wa Ruvuma na Njombe.

Morogoro hupata mvua mara mbili kwa mwaka. Mvua za vuli hunyesha kuanzia mwezi Oktoba hadi katikati ya mwezi Januari, na mvua za masika hunyesha katikati ya mwezi Februari na kuishia mwezi Mei mwishoni.

Kiwango cha mvua ni kati ya milimita 600 katika sehemu za tambarare na milimita 1,200 katika miinuko. Hata hivyo, zipo sehemu zilizo na ukame ambazo hupata mvua chini ya milimita 600 kwa mwaka.

Sehemu hizo ni pamoja na tarafa za Gairo katika Wilaya ya Gairo, Mamboya katika Wilaya ya Kilosa na Tarafa ya Ngerengere katika Wilaya ya Morogoro.

Kiutawala umegawanyika katika wilaya saba ambazo ni wilaya za Morogoro, Mvomero, Kilosa, Kilombero, Ulanga, Malinyi na Gairo. Pia, una halmashauri saba za wilaya na Halmashauri ya Manispaa moja na halmashauri ya Mji wa Ifakara.

Halmashauri za wilaya ni pamoja na Kilosa, Gairo, Kilombero, Morogoro, Ulanga, Mvomero na Malinyi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, karibu mji kasoro bahari. Endelea;


1.Wapi nitapoanzia,
Morogoro kusifia,
Mkoa umetimia,
Ni ghala letu nchini.

2. Morogoro Tanzania,
Baraka zimetimia,
Mito zaidi ya mia,
Yasambaa ardhini.

3. Morogoro fikiria,
Yale inayochangia,
Taifa lajivunia,
Maji hadi milimani.

4. Mabonde yametimia,
Mpunga twajilimia,
Chakula twajipatia,
Twajenga afya mwilini.

5. Morogoro nasifia,
Mwaka mzima sikia,
Mvua yamwagilia,
Tulime mabiringani.

6. Moro kutajirikia,
Ni rahisi nakwambia,
Mashamba kijilimia,
Nakwambia utawini.

7. Mtibwa ukisikia,
Hata Kilombero pia,
Sukari vyatupatia,
Tutumiayo mezani.

8. Wakulima wengi pia,
Miwa wanajilimia,
Viwanda waviuzia,
Pesa zenda mfukoni.

9. Matunda wajilimia,
Hata mbogamboga pia,
Kote kote wauzia,
Hata Dodoma sokoni.

10. Mimi ninafikiria,
Eneo kujipatia,
Muda utapotimia,
Niende lima kondeni.

11. Tena hivi nasikia,
Reli mpya yanukia,
Morogoro kufikia,
Weka tonge mdomoni.

12. Moro kudadavulia,
Siwezi yamalizia,
Ninafanya kugusia,
Ni utajiri nchini.

13. Michezo muziki pia,
Morogoro yatimia,
Walitamba Tanzania,

Na bado wajua fani.

14. Mbaraka Mwinshehe tia,
Tungo zako twasikia,
Salum Abdalla pia,
Moro ndiyo maskani.

15. Wasanii nakwambia,
Dunia tulitambia,
Moro yao asilia,
Walitubeba zamani,

16. Hata na mpira pia,
Wengi tunajivunia,
Mseto ninakwambia,
Walishatamba zamani.

17. Sembuli twakumbukia,
Walivyomshangilia,
Shuti akikupigia,
Wazama nalo golini.

18. Ni wengi kukutajia,
Mwisho siwezi fikia,
Mwanasoka malizia,
Mogella wa Zamoyoni.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news