TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-16: Karibu mkoani Mtwara, Karibuni Mtwara

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Mtwara ulianzishwa rasmi mwaka 1971 kutokana na Mpango wa Madaraka Mikoani ambao ulilenga kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Aidha, kabla ya hapo mkoa ulikuwa ndani ya Jimbo la Kusini ambalo lilijumuisha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara ambapo makao makuu ya jimbo yalikuwa Lindi.

Mkoa huo ulipoanzishwa ulikuwa tayari na wilaya tatu ambazo ni Masasi iliyoanzishwa mwaka 1928 chini ya ukoloni wa Waingereza, Newala mwaka 1956 chini ya wakoloni wa Kiingereza na Mtwara ilianzishwa mwaka 1961.

Kutokana na ongezeko la watu na kukua kwa Mkoa wa Mtwara ziliongezeka wilaya nyingine mbili ambazo ni Wilaya ya Tandahimba iliyoanzishwa mwaka 1995 kutoka kwenye Wilaya ya Newala na Nanyumbu ilianzishwa mwaka 2006 kutoka Wilaya ya Masasi.

Neno Mtwara limetokana na neno la lugha ya Kimakonde “kutwala” ikiwa na maana ya kuchukua (kunyakua) kitu chochote. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, Mtwara una mambo mengi hususani nishati ya gesi asilia. Endelea;


1. Samaki nchanga sikia,
Hadithi twazisikia,
Mtwara zinaanzia,
Bahari ya Hindi pwani.

2. Bandari tunatambia,
Kweli tunaitumia,
Korosho twajilimia,
Uchumi upate wini.

3. Wasofika nawambia,
Mtwara kuchele pia,
Kienda tajipatia,
Kile roho yatamani.

4. Gesi kujigundulia,
Makubwa metupatia,
Viwanda vinaingia,
Gesi hadi majumbani.

5. Wananchi hao pia,
Vita litupigania,
FRELIMO litumia,
Vita vyao msituni.

6. Hao twawashangilia,
Ukombozi kuchangia,
Msumbiji kufikia,
Uhuru kuwa mezani.

7. Nachingwea wajulia?
Wapiganaji sikia,
Mafunzo lijipatia,
Ya vita vya msituni.

8. Nasi tulisaidia,
Uhuru kupigania,
Wareno kufukuzia,
Uhuru tukauwini.

9. Huku nako nakwambia,
Ukombozi lichangia,
Sasa pia kwachangia,
Maendeleo nchini.

10. Huko tulijipatia,
Rais wa Tanzania,
Mkapa twajivunia,
Kwa utumishi makini.

11. Mengi alitufanyia,
Nchi liposhikilia,
Mengi twamkumbukia
Masasi kwake nyumbani.

12. Uchumi liukutia,
Chini unaning’inia,
Barabara zilivia,
Hali ilikuwa duni.

13. Mkapa hakutulia,
Njuga akauvalia,
Wengi limshambulia,
Hakuyumba asilani.

14. Kodi kujikusanyia,
Tulikuwa twasinzia,
Yeye alipoingia,
Kodi kaipa thamani.

15. Ukweli uwazi pia,
Kauli lisimamia,
Kwayo litutumikia,
Kwa hakika si utani.

16. Kusini ukipitia,
Lindi uweze fikia,
Ulikuwa waishia,
Njiani siyo nyumbani.

17. Sehemu ya kuvukia,
Mto Rufiji sikia,
Ni shida zilizidia,
Kama haiwezekani.

18. Wabunge tulisikia,
Walivyo lalamikia,
Nandonde nakumbukia,
Naye Majogo Bungeni.

19. Wao walipigania,
Daraja wakiwania,
Serikali lisikia,
Haikujali maoni.

20. Mkapa akaingia,
Njia anayopitia,
Daraja katupatia,
Limefungua Kusini.

21. Sasa hapo twavukia,
Mwaka mzima sikia,
Na tena linachangia,
Maendeleo nchini.

22. Mengine alipatia,
Machache alifulia,
Mengi aliyatubia,
Kaandika kitabuni.

23. Mengi alitufanyia,
Kwingi wametutajia,
Ikanona Tanzania,
Nchi yetu ya amani.

24. Kwa Mungu katangulia,
Huko tutamkutia,
Ila alotufanyia,
Yatabaki vitabuni.

25. Bado sijamalizia,
Mtwara kuisifia,
Bila ya kukutajia,
Shimo la Mungu utani.

26. Hili shimo nakwambia,
Newala limetulia,
Wale walolifikia,
Ni maajabu machoni.

27. Pale kama waingia,
Usije dharaulia,
Vinginevyo taishia,
Upotelee shimoni.

28. Maajabu nakwambia,
Ni mengi wasimulia,
Ni vema kulifikia,
Ni shimo la Maanani.

29. Kiufupi nasikia,
Upepo unaanzia,
Ni mkali takimbia,
Watetemesha mjini.

30. Giza la kufunikia,
Mji Newala sikia,
Mwingine kumwangalia,
Humuoni abadani.

31. Utajiri Tanzania,
Ni mwingi ninakwambia,
Ikiwa umepania,
Nenda huko utawini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602


Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news