TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-18: Karibu Njombe, Ni mali kutoka shambani

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Njombe ulianzishwa Machi Mosi, 2012 na kutangazwa katika Gazeti rasmi la Serikali Na.9 chini ya agizo Na.72. 

Katika kutekeleza madaraka aliyopewa Rais na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 2(2), mkoa wa Njombe ulianzishwa baada ya uamuzi wa Rais wa kuugawa mkoa wa Iringa kuwa mikoa miwili ya Njombe na Iringa. 

Mkoa umegawanyika katika wilaya nne ambazo ni Njombe, Wanging’ombe, Makete na Ludewa. Pia kuna mamlaka za Serikali za Mitaa sita ambazo ni Halmashauri za Mji wa Njombe na Makambako, Halmashauri za Wilaya za Njombe, Makete, Wanging’ombe na Ludewa.

Mkoa upo katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Njombe na sehemu ya mkoa wa Morogoro. 

Njombe, imepakana na Mkoa wa Iringa upande wa Kaskazini, Mkoa wa Morogoro upande wa Mashariki na Mkoa wa Ruvuma upande wa Kusini. 

Jamhuri ya Malawi kupitia Ziwa Nyasa na sehemu ya Mkoa wa Mbeya inapakana na Mkoa wa Njombe upande wa Kaskazini-Magharibi, wakati upande wa Magharibi mipaka inashirikiwa na Mkoa wa Mbeya. 

Mkoa uko kati ya Latitudo 080 50’ na 10030’ Kusini mwa Ikweta na kati ya Longitudo 330 45’ na 350 45’ Mashariki mwa Greenwich.

Aidha, Mkoa wa Njombe una jumla ya eneo la kilomita za mraba 24,994 kati ya hizo kilomita za mraba 21,172 na kilomita za mraba 3,822 zimefunikwa na ardhi na maji mtawalia.

Hali ya hewa ya ukanda huu inachangiwa na mambo kadhaa ambayo yamesababisha uundaji wa kanda tatu za hali ya hewa ambazo ni, ukanda wa nyanda za juu, kati na chini. 

Kilimo cha chai mkoani Njombe. (Picha na Jackson Fute).

Makabila asilia ni Wabena, Wakinga, Wapangwa, Wamanda, Wanyakyusa, Wanji, Wamagoma, Wamahanji, na Wakisi. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema karibu Njombe, huu ni mkoa pia wenye mengi. Endelea;

1. Njombe ni mkoa pia,
Juzi juzi meanzia,
Lakini unakimbia,
Maendeleo nchini.

2. Kama Mbeya yaanzia,
Njombe yamalizikia,
Baridi ukisikia,
Yagusa na mifupani.

3. Watu wake nakwambia,
Kazi wanajifanyia,
Bidii inazidia,
Matunda tele mitini.

4. Njombe ninawaambia,
Kofia nawavulia,
Navyojilimbikizia,
Mali toka mashambani.

5. Chai tunayotumia,
Njombe watuzalishia,
Viazi navyojilia,
Vyatoka huko jioni.

6. Mkoa unachangia,
Kuilisha Tanzania,
Mbao unatupatia,
Ujenzi tusijihini.

7. Madini twajivunia,
Ya kujenga Tanzania,
Liganga mejichimbia
Mchuchuma pia ndani.

8. Chuma huko chajazia,
Makaa ya mawe pia,
Yanawiri Tanzania,
Kuwa na hayo madini.

9. Viwanda kuanzishia,
Nishati kuzalishia,
Makaa husaidia,
Muumba atupe nini?

10. Miwato tunatumia,
Kwa nguzo na dawa pia,
Miti ya Njombe sikia,
Yatufaa kama nini.

11. Ngano inalimwa pia,
Maandazi kumbukia,
Mikate tunajilia,
Njombe jama iacheni.

12. Wakinga wajuzi pia,
Biashara kuchangia,
Hao wanafanania,
Na Wachaga madukani.

13. Wako kote Tanzania,
Makete ni asilia,
Kimya wanajifanyia,
Biashara mkononi.

14. Ukitaka jipatia,
Maendeleo sawia,
Kwao ukiigizia,
Utatoka naamini.

15. Huwezi kuwakutia,
Hovyo hovyo watumia,
Wajinyima kutumia,
Kwa akiba ya mwakani.

16. Pale walipofikia,
Jaribu kuangalia,
Muda unavyoishia,
Neemeka mfukoni.

17. Na Wapangwa wapo pia,
Mazao wajilimia,
Chakula kujipatia,
Moto uwake jikoni.

18. Anna Makinda sikia,
Njombe alikoanzia,
Siasa kuzifanyia,
Hadi Spika Bungeni.

19. Maspika kitajia,
Wanaume wote pia,
Mmoja aloanzia,
Ni Makinda wa kikeni.

20. Bunge alitushikia,
Sitta alipoachia,
Makubwa litufanyia,
Bungeni Serikalini.

21. Fujo wakimfanyia,
Wabunge lijizalia,
Fimbo aliwachapia,
Marufuku vikaoni.

22. Nidhamu lishikilia,
Akifoka kuwambia,
Muda akamalizia,
Anajilia pensheni.

23. Huko kuna baba pia,
Elimu lishikilia,
Maarufu nakwambia,
Naye yuko penshenini.

24. Makwetta nakutajia,
Waziri tuliringia,
Yale alutufanyia,
Bado yangali hewani.

25. Vile wanasimulia,
Elimu kishikilia,
Ndiye wazo limjia,
Lugha elimu nchini.

26. Vile alisisitizia,
Kiswahili kutumia,
Elimu Juu anzia,
Hadi kufikia chini.

27. Hadi sasa twasikia,
Hilo wazungumzia,
Mwasisi kukumbukia,
Vema ikae kichwani.

28. Japo ametangulia,
Makwetta twakumbukia,
Vile alipigania,
Elimu bora nchini.

29. Njombe nako kwanukia,
Utajiri Tanzania,
Kama ukifwatilia,
Ni baraka za nyumbani.

30. Parachichi mesikia,
Watu wanajilimia,
Mbeya na Njombe pia,
Miti ni mingi shambani.

31. Watu wanajilimia,
Mashamba yanavutia,
Fedha wanajipania,
Za ndani na za kigeni.

32. Masikini lisikia,
Walokuwa metitia,
Parachichi kupitia,
Kwa sasa wako hewani.

33. Kipato kinaingia,
Nao wakifurahia,
Maisha yanavutia,
Mkono wenda kinywani.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news