TANZANIA, BORA KUISHANGILIA-20: Sasa tunaingia Rukwa,chakula cha uhakika

NA LWAGA MWAMBANDE

HISTORIA inaonesha kuwa, Mkoa wa Rukwa ulianzishwa mwaka 1974 kwa kumega sehemu ya Mkoa wa Tabora (Mpanda) na Mbeya (Sumbawanga).

Mnamo mwezi Julai 2010 Serikali ya Awamu ya Nne iliridhia kugawanywa kwa Mkoa wa Rukwa na kuanzishwa kwa Mkoa mpya wa Katavi.

Kijiografia Mkoa wa Rukwa upo kati ya Latitudo 70-90 Kusini ya Ikweta na Longitudo 30-320 Mashariki ya Grinwichi.

Mkoa huu unapakana na mikoa ya Katavi upande wa Kaskazini na Songwe upande wa Kusini Mashariki. Aidha, unapakana na nchi za Zambia upande wa Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa Magharibi.

Eneo la juu sana katika Mkoa wa Rukwa linapatikana Malonje katika Nyanda za Juu za Ufipa ambalo ni mita 2,461 Juu ya Usawa wa Bahari na eneo la chini zaidi ni Ziwa Tanganyika lenye mita 773 Juu ya Usawa wa Bahari.

Aidha, mkoa huu una eneo la kilomita za mraba 27,765, kati ya hizo kilomita za mraba 22,844 (82.3%) ni za nchi kavu na kilomita za mraba 4,921 (17.7%) ni za maji

Mkoa wa Rukwa umegawanyika katika wilaya tatu zenye halmashauri nne.Wilaya hizo ni Sumbawanga, Kalambo na Nkasi.

Mkoa unajumuisha Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Nkasi na Kalambo.

Aidha, ndani ya mkoa kuna Mamlaka za Miji Midogo miwili ambazo ni Namanyere Wilaya ya Nkasi na Laela Wilaya ya Sumbawanga.

Mkoa wa Rukwa una hali ya hewa ya Kitropiki ambapo wastani wa joto ni Sentigredi 13 katika baadhi ya maeneo kwa miezi ya Juni na Julai hadi Sentigredi 27 kwa miezi yenye joto jingi ya Oktoba na Desemba.

Pia, mkoa umebahatika kuwa na mvua za kuaminika kwa miaka mingi, kwani mvua za mkoa huo ni wastani wa milimita 850 kwa mwaka zikinyesha kuanzia mwezi wa Novemba hadi Mei. Kiangazi huanza mwezi Juni mara baada ya majira ya mvua hadi mwezi wa Oktoba.

Kiuchumi, wakazi wa Mkoa wa Rukwa wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ufugaji, sekta ya utalii, madini, uvuvi, viwanda vidogo pamoja na biashara ndogondogo.

Shughuli kuu ya kiuchumi ni kilimo, ambapo mazao ya chakula yanayolimwa kwa wingi ni mahindi, mpunga,viazi vitamu,viazi mviringo,mihogo,maharage na ulezi.

Mazao ya biashara yanayolimwa kwa wingi ni alizeti, ngano, ufuta na michikichi. Aidha, ziada ya mazao ya chakula kama mahindi,mpunga,maharage,ulezi,ngano,shayiri na karanga hutumika pia kama mazao ya biashara.

Ufugaji unabaki kuwa shughuli kuu muhimu ya pili ya uchumi katika Mkoa wa Rukwa. Mifugo inayofugwa kwa wingi ni ng’ombe,mbuzi,nguruwe,kondoo,punda na kuku. Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema karibu mkoani Rukwa uweze kupata chakula cha uhakika. Endelea;

1. Sasa Rukwa naingia,
Haki nitawafanyia,
Siwezi kuahidia,
Yote wafahamisheni.

2. Kilimo ukisikia,
Rukwa inatangulia,
Mahindi tunatumia,
Kusini kaskazini.

3. Kwa mengi twaisifia,
Mengine twaitungia,
Watu wake twasifia,
Kwa mambo wako makini.

4. Madini wajichimbia,
Kwa uchumi kuchangia,
Dhahabu makaa pia,
Yamejaa ardhini.

5. Ziwa Rukwa twasifia,
Kwa samaki kuchangia,
Afya tunajipatia,
Hasa hasa protini.

6. Mpaka watulindia,
Nchi Kongo na Zambia,
Ufugaji upo pia,
Wa ng’ombe na kuku ndani.

7. Kama ulijifungia,
Kitaka kuufikia,
Lami imeshaingia,
Mjini na vijijini.

8. Kienda tajipatia,
Elimu kubwa sikia,
Unaweza kupitia,
Kuogolea ziwani.

9. Sumbawanga fagilia,
Kwa mengi twaisifia,
Na mengi twaizulia,
Ni utajiri nchini.

10. Wale wanafanyizia,
Na watu kuwawangia,
Sumbawanga kiingia,
Utulie kivulini.

11. Fyoko ukiwafanyia,
Jua watakuzukia,
Watavyokufanyizia,
Utaishia porini.

12. Watu huko nakwambia,
Wapole kiwasikia,
Kuishi wakujulia,
Sijui niseme nini.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news